NA DIRAMAKINI
KAIMU Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Bw.Mafutah Bunini ameongoza kikao cha dharura cha wakuu wa taasisi zinazounda Mfumo wa Mahala Pamoja (NIFC) kwa ajili ya kupitia utekelezaji wa Mradi wa Dirisha (Mfumo) la Pamoja wa kuwahudumia wawekezaji.
Ni kupitia kikao kazi kilichofanyika mkoani Morogoro Juni 7, 2022 na kuwakutanisha pamoja wawakilishi wa taasisi mbalimbali za Serikali ambazo TIC inafanya nazo kazi.
Taasisi hizo ni Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA),Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA),Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC).
Nyingine ni Shirika la Viwango Tanzania (TBS),Idara ya Uhamiaji,Ardhi,Idara ya Kazi,Shirika la Umeme nchini (TANESCO),Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) na Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba nchini (TMDA).
“Serikali katika kuhakikisha inaboresha huduma ya uwekezaji hasa kwa kutumia mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) imeandaa mfumo wa pamoja ambao utawezesha taasisi zinazotoa huduma kwa wawekezaji kusomana (Interface),” amesema Bw. Bunini.
Kikao hicho kimepitia taarifa za mfumo ulipofikia, kuwaonyesha wakuu wa taasisi mfumo unavyofanya kazi, kujadili usalama wa mfumo ikiwemo kupitia hati za makubaliano za kubadilishana taarifa (data sharing agreement).
Aidha, utekelezaji wa mradi huo umefikia asilimia 90 ambapo.Meneja Mradi wa Mfumo wa Kidijitali wa kuwahufumia Wawekezaji, Bw. Robert Mtendamema amesema, “majadiliano ya leo yamelenga kukubaliana kuanza matumizi ya mfumo huo hivi karibuni”.
Taasisi ambazo zitaanza kutumia mfumo huo kwa awamu ya kwanza ya mradi huo ni BRELA, TRA, NIDA, Uhamiaji, Ardhi, Idara ya Kazi na Kamishina wa Kazi.
Aidha, matarajio ya Serikali ni kwamba dirisha au mfumo huu utakapozinduliwa utasaidia kutoa vibali kwa wakati.
Pia utasaidia kuondoa urasimu, kutoa huduma za haraka kwa wawekezaji na utatunza taarifa za wawekezaji.