NA MWANDISHI WETU
SERIKALI imesema inaboresha vituo vya walimu kwa lengo la kuendelea kutoa fursa kwa walimu kupata mafunzo wakiwa kazini ili kuwajengea uzoefu.
Hatua hiyo inakwenda sambamba na maboresho ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014 pamoja na mabadiliko ya mitaala ili kuwa na wahitimu wenye ujuzi na maarifa ya kuweza kujiajiri ama kuajiriwa.
Hayo yamesemwa jijini Dar es Salaam na Mhe.Prof.Adolf Mkenda, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia wakati wa semina ya utambulishaji wa mjadala wa wazi juu ya kitabu cha wasifu wa Mwalimu Julius Nyerere ambapo kumekuwa na mazungumzo juu ya ubora wa elimu na ndio maana maboresho hayo yanafanyika ili kuhakikisha elimu inayotolewa inakuwa bora, lakini pia inahakisi hali halisi ya maisha.
“Nashukuru tumeanza kuongeza idadi ya walimu, na kwa mara ya kwanza tumeanza kutoa mafunzo kwa walimu. Tumechukua walimu wa kilimo na sayansikimu nchi nzima kwa lengo la kubadilishana uzoefu na tumetenga bajeti kwa ajili ya kuendeleza mafunzo kazini,”amesema Waziri Mkenda.
Waziri Mkenda ametumia fursa hiyo kuwaomba wadau kuendelea kutoa maoni ya kuboresha mitaala na kwamba kwa kuwa sheria ya elimu nayo itafanyiwa mapitio itasaidia kupunguza mabadiliko ya mara kwa mara kwenye elimu yanayotokana na mabadilko ya viongozi wa elimu.
Akizungumzia juzuu ya wasifu wa Hayati Mwalimu Nyerere amesema, kwa kuwa Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliagiza zitafsiriwe kwa lugha ya Kiswahili ni vizuri Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) ikarejesha Kavazi ya Mwalimu ili kusaidia katika kutekeleza kazi hiyo.
Naye Mkurugenzi Mkuu Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia, Dkt. Amos Nungu amesema atahakikisha juzuu hizo zinatafsiriwa ikiwa ni pamoja na kurejesha Kavazi ya Mwalimu.
Kwa upande wake, Prof. Issa Shivji amesema mapinduzi ya elimu yanatakiwa kuanzia Wizara ya Elimu kwa kutambua elimu bora inatokana na walimu bora. Amewataka Watanzania kusoma juzuu hizo ili kujenga uzalendo.
Akizungumza katika mjadala huo, Mwalimu mstaafu Fauster Sokiri amesema usalama wa nchi hii unategemea pamoja na mambo mengine Wizara ya Elimu hivyo ni vizuri kuendelea kufanya maboresho ya sifa za kuajiri walimu kwa lengo la kuendelea kuboresha elimu.