NA DIRAMAKINI
WAKAZI wa Tarafa ya Ngorongoro iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro mkoani Arusha ambao wameamua kuhama kwa hiyari yao kwenye eneo la hifadhi wamesema, wanamshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa upendo mkubwa aliouonesha kwao kwa kuhakikisha nao wanakuwa na makazi ya kudumu eneo la Msomela wilayani Handeni mkoani Tanga.

Mkazi wa Kijiji cha Kimba wilayani Ngorongoro Beatrice Soka amesema amefurahi sana kwasababu kwa muda mrefu walitamani mchakato huo ufanyike lakini ulichelewa.
“Kwa hiyo tamko hili lilipoletwa kwa kweli mimi ni miongoni mwa watu tuliojiandikisha kwa hiyari yangu pamoja na familia yangu kwa ajili ya kwenda huko Msomela".

“Kuna shule, huduma ya maji , miundombinu yote na kuna mabwawa ya kutosha, nyumba, mzunguko wa nyumba kuna ekari tatu mbali na mashamba yalipo nje ya pale ekari tano na mama Samia ametuwezesha tuliotoka hapa tuweze kwenda kuendelea na kasi kwani tumepoteza muda".

Akizungumza baada ya kushuhudia zoezi hilo Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. John Mongela amesema, zoezi hilo ni la hiyari na waliyoamua kuondoka wamefikia hatua hiyo baada ya kujadilina na familia zao na kuafiki mpango huo bila kulazimishwa.