Twendeni na kasi kubwa ya hamasa Sensa Agosti 23 asema DC Makilagi

NASHEILA KATIKULA

VIONGOZI wa dini wameombwa kuhamasisha waumini wao kujitokeza kwa wingi kwenye zoezi la Sensa ya Watu na Makazi ambalo linatarajiwa kufanyika Agosti 23, mwaka huu.
Wito huo umetolewa na Mwenyekiti wa Sensa ya Watu na Makazi ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Amina Makilagi kwenye mkutano wa wadau wa maendeleo wenye lengo la kuhamasisha watu wajitokeze kwenye zoezi hilo.

Makilagi amesema, ni vema viongozi wa dini kuhamasisha waumini wao ili waweze kutambua umuhimu wa sensa ya watu na makazi kwani lengo la serikali na kuhakikisha kila wananchi anahesabiwa kwenye zoezi hilo.
"Tunaomba viongozi wa dini baada ya ibada muwe mnatoa elimu ya Sensa ya watu na makazi kwa waumini wenu ili waweze kuona umuhimu wa zoezi hili.

Hata hivyo, ameongeza kuwa karani wa Sensa atafika katika kaya akiwa na kitambulisho na sare maalumu inayomtambulisha pia ataambatana na kiongozi wa serikali za mtaa na kitongoji.

Amesema, sensa la watu na makazi itasaidia serikali kutimiza wajibu kwa wananchi kulingana na idadi ya watu wa eneo husika pamoja na kupata ufumbuzi wa mahitaji ya watu wenye ulemavu.

Makilagi amesema, sensa ya watu na makazi itasaidia kupata taarifa ya kujua idadi ya wanaume na wanawake,umri,hali ya ndoa(kidemographia),kujua taarifa za kijamii, uchumi, na hali ya mazingira kwa lengo la kupata takwimu sahihi ambazo zitawezesha serikali na wadau wengine kupanga maendeleo ya watu katika sekta mbalimbali za elimu,miundo mbinu,afya, hali ya ajira na Taifa kwa ujumla.

"Itakapofika saa sita na dakika moja usiku wa kuamkia Agisti 23 mwaka huu watu wote watakaokuwa wamelala ndani ya mipaka yetu ya nchi ya Tanzania wote tutawahesabu naomba mtowe ushurikiano kwa mawakala wa sensa ambayo watawatembelea kwenye maeneo yenu,"amesema Makilagi.
Ameongeza kuwa sensa itasaidia kupata taarifa za maendeleo,kisiasa,uchumi, hali ya kibiashara pamoja na serikali kuandaa bajeti na kuleta mahitaji kwa wananchi.

Naye Mratibu wa sensa ya watu na makazi wa Wilaya ya Nyamagana, Luhinda Constantine amesema taarifa zote zitakazo chukuliwa na karani wa sensa zitakuwa za siri na zitatumika kwa madhumuni ya kitakwimu.

"Kwa kujibu wa sheria ya takwimu Sura ya 351 taarifa zote zitakazo chukuliwa na karani wa Sensa zitakuwa za siri na zitatumika kwa madhumuni ya kitakwimu pekee kwani sensa ya mwaka huu niya sita kufanyika nchini Tanzania,"amesema Constantine.

Amesema watahakikisha wanatoa elimu ya Sensa kwa wananchi kwa njia mbalimbali ikiwamo mikutano, kwenye vyombo vya habari na vipeperushi
Amesema zoezi hilo litafanywa na makarani wa sensa ambao watatembea kaya zote na kufanya mahojiano na Mkuu wa kaya ambao watawasaidia kupata taarifa sahihi ili kukamlisha zoezi hilo.

Kwa upande wake Meya wa Jiji la Mwanza, Constantine Sima amesema kuwa sensa ni muhimu kwa jamii pia itasaidia serikali kufahamu namna ya kufanya maendeleo.

Kwa upande wake Makamu mwenyekiti wa Shirikisho la Walimu na Makada wa Chama Cha Mapunduzi Wilaya ya Nyamagana,Michael Lyimo amesema atahakikisha anatoa elimu kwa wanafunzi ili waweze kuona umuhimu wa zoezi hilo na kupeleka ujumbe kwa wazazi wao ili washiriki zoezi hilo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news