Ukigusa fedha za chakula shuleni, makazi yako ni jela asema Diwani wa Mzimuni Dar

NA ANNETH KAGENDA

MTU yeyote atakayebainika anafanya ufisadi au wizi wa aina yoyote kwenye fedha ya chakula inayochangwa na wazazi kwa ajili ya chakula cha watoto wao wa shule tatu za Mzimuni Sekondari, Msingi na ile ya Mikumi ataburuzwa mahakamani.
Hayo yamesemwa jijini Dar es Salaam na Diwani wa Kata ya Mzimuni, Manifred Lyoto, wakati wa uzinduzi wa tukio hilo la wanafunzi wa shule hizo kuanza kupata chakula ambapo Diwani huyo ndiye aliahidi kufanya hivyo wakati wa kampeni zake za kuomba ridhaa ya kuchaguliwa kuwa Diwani.

Amesema, awali wazazi walisuasua kuchanga fedha za chakula kwa ajili ya watoto wao kwa kuhofia kudhulumiwa na baadhi ya watu wasiokuwa waaminifu na kusema kuwa sasa hakuna mzazi atakaye zulumiwa badala yake fedha hiyo itakuwa inaingia kwenye akaunti ya benki moja kwa moja.
"Kwa hiyo wazazi wawe na amani, fedha zao zipo salama zitakuwa zinatolewa kwa utaratibu ambao umepangwa na shule na kwenda kununua chakula moja kwa moja, hivyo wazazi wajitahidi kuchangia hicho kiasi kidogo ili watoto wapate uhakika wa chakula na ikumbukwe wakila akili itatulia darasani na amani itakuwepo,"amesema.

Amesema, jambo lingine ni kwamba wanafunzi na wazazi wanatakiwa kuendelea kuwathamini walimu kutokana na kwamba kila mtu kwa nafasi yake kazini kwake amefundishwa na Mwalimu.

Afisa Elimu Sayansi Kimu Afya na Lishe aliyemwakilisha Afisa Elimu Msingi na Sekondari, Martha Kusaga amesema kuwa, watoto kupata chakula shuleni ni jambo la msingi sana na kwamba linaleta afya kwa watoto pamoja na utulivu darasani jambo litakalo saidia kuwepo na ufaulu mzuri na mkubwa pamoja na kazi ya Mwalimu kuwa nyepesi.

"Kama Mwakilishi wa nipende kumpongeza Diwani kwa kazi kubwa aliyoifanya kuhakikisha watoto wetu wanapata chakula lakini pia ni wakati wa wazazi nao kuhakikisha mtoto anatoka na tunda nyumbani," amesema Afisa huyo na kuongeza;

"Lakini pia wazazi hao hao wanatakiwa kuhakikisha watoto wanapata sehemu ya kukaa kula chakula chao vizuri iwe sehemu ya kivuli na ikiwezekana wazazi hao walete hata mikeka watoto wasile wamesimama wala kwenda kula madarasani,"amesema.

Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Mzimuni, Juma Lighton amesema kuwa, kwenye ufundishaji watoto shuleni chakula ndio mwafaka wa mwanafunzi kuwa na usikivu zaidi kwa mwalimu wake.

"Hivyo tunampongeza Diwani Lyoto kwa jambo hili kwani wanafunzi wetu tunaamini sasa wanaenda kufanya vizuri kwani mtoto bila kula afundishiki lakini pia ni zuri kiafya,"amesema Lighton.

Hata hivyo, Diwani huyo alishiriki kuwagawia chakula watoto kama ishara ya kuzindua huduma hiyo kwa wanafunzi hao.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news