NA FRESHA KINASA
MWENYEKITI wa Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi Tanzania (UWT), Gaudencia Kabaka ameitaka jumuiya hiyo kuwa mfano bora kwa kuendela kufanya chaguzi zake kwa haki na kuwachagua viongozi waadilifu na wenye maono na uwezo wa kuongoza jumuiya hiyo kwa ufanisi kuanzia ngazi za chini.

Amesema kuwa, jumuiya hiyo inapaswa kuendelea kufanya chaguzi za kuwapata viongozi wake kwa haki na kwamba kila mmoja ana haki ya kugombea nafasi ndani ya UWT na pia amesema upendo na mshikamano ndani ya jumuiya hiyo unapaswa kushamiri kwa kiwango cha juu. Huku akijivunia kupungua kwa makundi ndani ya UWT hivi sasa tofauti na miaka ya nyuma.

"Chaguzi zisitusambaratishe, zisitutenganishe, zisitugawe tuzithamini hizi chaguzi ili tupate uwezo wa kumchagua Rais Samia Hassan 2025 tunaenda kumpigia kura sasa Rais wa Awamu ya Sita mama yule ametubeba Kama wanawake, kwanza tukumbuke alivyopokea nchi katika hali ngumu,"amesema Kabaka.

Aidha, Kabaka amesisitiza wanawake wa jumuiya hiyo, kujisajili kwa mfumo wa kielekitroniki sambamba na kushiriki kikamilifu katika zoezi la Sensa ya watu na makazi itakayofanyika mwezi Agosti, mwaka huu ili kuiwezesha Serikali kupanga mipango yake kwa ufanisi ya Maendeleo kwa Watanzania.

Wegesa Hassan ni Mwenyekiti wa UWT Mkoa wa Mara ambapo amesema Rais Samia Hassan amewaheshimisha wanawake na Watanzania kiujumla kwa uongozi bora na kuwa kinara kwa kufanya mambo mengi ya manufaa kwa Wananchi.

Katika kikao hicho, (UWT) Mkoa wa Mara imempa tuzo ya uongozi bora Mwenyekiti wa Jumuiya ya Umoja wa Wanawake Tanzania Gaudencia Kabaka kwa kutambua na kuthamini uongozi wake thabiti Katika kuiongoza jumuiya hiyo kwa mafanikio makubwa.