Vigezo vilivyotumika kuwapa ajira Watanzania 16,676 kati ya waombaji 165,948 Sekta ya Afya na Elimu

NA GODFREY NNKO

OFISI ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) imetangaza majina 16,676 ya watumishi wapya waliopangiwa vituo vya kazi katika Sekta ya Elimu na Afya nchini.

Orodha hiyo inatokana na waombaji wenye sifa waliokidhi vigezo baada ya Aprili, 2022 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan kutoa kibali cha ajira kwa kada za Ualimu na Afya, kwa ajili ya kuajiri walimu 9,800 wa shule za msingi na sekondari na wataalam wa afya 7,612.ORODHA YA MAJINA SOMA HAPA>>>

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mheshimiwa Innocent Bashungwa amesema, baada ya kupata kibali cha ajira, Ofisi ya Rais-TAMISEMI ilitoa tangazo kwa wahitimu mbalimbali wa Ualimu na Kada za Afya, kuwasilisha maombi ya kazi, kupitia mfumo wa kielektroniki wa kupokea na kuchakata maombi ya ajira, kuanzia Aprili 20 hadi Mei 8,2022.

Mheshimiwa Bashungwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma leo Juni 26, 2022 amesema, jumla ya maombi 165,948 yakiwemo ya wanawake 70,780 na wanaume 95,168 yaliyopokelewa kwenye mfumo, ambapo maombi ya kada za afya ni 42,558, na kada ya Ualimu ni 123,390.

Amesema, kwa upande wa kada za ualimu,waombaji wenye sifa waliokidhi vigezo na kupangiwa vituo vya kazi ni 9,800 ambapo jumla ya walimu 5,000 wamepangwa shule za msingi na walimu 4,800 Shule za sekondari, wakiwemo walimu wenye ulemavu wa shule za msingi na sekondari 261.

Waziri Bashungwa amesema, kwa upande wa kada za Afya,waombaji wenye sifa waliokidhi vigezo na kupangiwa vituo vya kazi ni 6,876 wanawake ni 3,217 sawa na asilimia 46.8 na wanaume ni 3,659 sawa na asilimia 53.2 wakiwemo wenye ulemavu 42 sawa na asilimia 0.61.

Walifanyaje?

Mheshimiwa Waziri Bashungwa amesema, ili kufanikisha mchakato wa ajira, Ofisi ya Rais-TAMISEMI iliunda Timu Maalum, ya kufanya Uchambuzi wa Maombi ya Ajira, iliyohusisha taasisi mbalimbali.

Taasisi hizo amesema, ni pamoja na Ofisi ya Rais Ikulu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA), Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Ufundi Stadi (NACTVET), Sekretarieti ya Ajira, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), na Mabaraza ya Kitaalamu katika Sekta ya Afya.

Kuna vigezo?

Waziri Bashungwa amesema, kutokana na idadi ya waombaji kuwa kubwa, Timu ya Uchambuzi wa Maombi ya Ajira ilipewa vigezo vilivyoandaliwa kama mwongozo wa kutoa ajira kwa waombaji, kwa lengo la kuhakikisha uwepo wa haki na uwazi katika zoezi hili.

Amesema, katika kuhakikisha usawa wa kijinsia unafikiwa, katika vigezo vilivyotumika kupata waajiriwa wapya kwa mwaka 2022, kila kigezo kilizingatia uwiano wa kijinsia.

Miongoni mwa vigezo vilivyotumika Mheshimiwa Bashungwa amesema ni mwaka wa kuhitimu ambapo katika kigezo hiki, kipaumbele kimetolewa kwa waombaji wenye sifa waliotangulia kuhitimu kwa mfuatano wa mwaka, kulingana na hitaji la kada,kozi au kiwango cha elimu, na pia mwaka wa kozi ilivyoanza kutoa wahitimu.

Akizungumzia upande wa umri wa kuzaliwa, Mheshimiwa Waziri Bashungwa amesema kuwa,waombaji wenye sifa waliopangwa kwa mujibu kigezo cha mwaka wa kuhitimu walipangwa kulingana na umri wa kuzaliwa.

"Lengo ni kuwawezesha waombaji wenye umri unaokaribia miaka 45 kuingia katika utumishi wa umma kwa masharti ya kudumu, kwa mujibu wa Sera ya Ajira Menejimenti na Ajira katika Utumishi wa Umma toleo la Pili la mwaka 2008,"amesema.

Mheshimiwa Waziri Bashungwa akizungumzia kuhusu waombaji Wenye Ulemavu amesema, uchambuzi wa maombi ulizingatia vigezo vyote vya mwaka wa kuhitimu na umri wa kuzaliwa.Soma hapa Waziri akitangaza waliopangiwa kazi>>>

"Hata hivyo, vigezo hivi vilitumika kuwashindanisha waombaji wenye ulemavu peke yao, kwa kuzingatia takwa la Sheria ya Watu Wenye Ulemavu Na. 9 ya mwaka 2010, kifungu cha 31 (1)-(3). Uchambuzi huu ulifanywa kwa ushirikiano na Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu,"amesema Mheshimiwa Waziri Bashungwa.

Taratibu zilizofuatwa

Mheshimiwa Waziri amesema, mchakato wa uchambuzi wa maombi ya ajira ya Kada za Afya na Ualimu ulizingatia utaratibu ufuatao:-

Mosi ilihusisha uchambuzi wa moja kwa moja kutoka kwenye mfumo wa maombi. Waziri Bashungwa amesema, mfumo huu umewezesha waombaji wote wenye sifa kupata ajira kwa haki na usawa,kama yalivyo maelekezo ya Rais wa Serikali ya Awamu ya Sita, Mhe. Samia Suluhu Hassan, kwamba Watanzania wote wenye sifa wapate ajira bila upendeleo.

"Hivyo mfumo huu uliwachuja waombaji awali kwa kuzingatia mahitaji ya kibali cha ajira kilichotolewa, ukamilifu wa viambata vilivyohitajika kwa mwombaji, na mwaka wa kuhitimu waombaji; na

"Pili, uchambuzi wa kina ulifanyika ukihusisha pia uhakiki wa nyaraka za maombi yaliyopata uzito wa juu, kulingana
na vigezo vilivyowekwa,"amesema Mheshimiwa Waziri.

Mahitaji

Amesema, upangaji wa watumishi wa Kada za Afya na Ualimu katika vituo vya kutolea huduma za afya na shule, umezingatia mahitaji ya watumishi katika mikoa husika.

Waziri Bashungwa amesema, kutokana na juhudi za Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Sita, Mhe. Samia Suluhu Hassan, katika kufanya maboresho makubwa ya Sekta ya Afya, upangaji wa watumishi wapya umezingatia mahitaji ya watumishi katika halmashauri zenye hospitali mpya,vituo vya afya vipya,na zahanati mpya zilizokamilika ambazo zimeshindwa kutoa huduma za msingi, kutokana na kukosa watumishi wenye sifa, pamoja na halmashauri zenye upungufu mkubwa wa watumishi hao.

Aidha, amesema kwa upande wa kada za ualimu, utaratibu wa upangaji ulizingatia mgawanyo wa nafasi kwa kila somo, na kiwango cha elimu kulingana na hitaji la kibali.

Waziri Bashungwa amesema, mchakato huu wa ajira umetoa fursa kwa waombaji kutoka mikoa yote ya Tanzania, hivyo upangaji wake umezingatia uzalendo na utamaduni wetu, kuwa kila mtanzania anaweza kufanya kazi mahali popote nchini.

Waliokidhi vigezo

Mheshimiwa Waziri Bashungwa amesema, kwa upande wa kada za Afya,waombaji wenye sifa waliokidhi vigezo na kupangiwa vituo vya kazi ni 6,876 wanawake ni 3,217 sawa na asilimia 46.8 na wanaume ni 3,659 sawa na asilimia
53.2 wakiwemo wenye ulemavu 42 sawa na asilimia 0.61 kutokana na uchache wa waombaji wenye sifa wa kundi hilo.

Aidha, nafasi 736 kada za afya zilikosa waombaji wenye sifa. Kada hizo ni Daktari wa Meno (50), Tabibu Meno (43), Tabibu Msaidizi (244), Mteknolojia Mionzi (86) na Muuguzi ngazi ya cheti (313).

Mheshimiwa Waziri amesema, kada hizi zitarudiwa kutangazwa ili kupata waombaji wenye sifa watakaojaza nafasi

Kada za Ualimu

Kwa upande wa kada za ualimu,Mheshimiwa Waziri amesema,waombaji wenye sifa waliokidhi vigezo na kupangiwa vituo vya kazi ni 9,800 ambapo jumla ya walimu 5,000 wamepangwa shule za msingi na walimu 4,800 Shule za sekondari, wakiwemo walimu wenye ulemavu wa shule za Msingi na Sekondari 261.

"Kati ya Walimu 5,000 wa shule za Msingi wanawake ni 2,353 sawa na asilimia 47.06 na wanaume ni 2,647 sawa na asilimia 52.94.

"Kwa upande wa walimu 4,800 wa Shule za sekondari wanawake ni 1,289 sawa na asilimia 26.85 na wanaume ni 3,511 sawa na asilimia 73.15. Aidha, walimu wenye ulemavu 261 wa shule za Msingi na Sekondari walioajiliwa ni sawa na asilimia 2.66 ya walimu wote walioajiriwa wakiwemo wanawake 84 na wanaume 177.

"Napenda ieleweke pia kuwa, kwa walimu wa sekondari tumetoa ajira za walimu wa sayansi kwa asilimia 76 ya nafasi 4,800 tulizopewa,"amesema Mheshimiwa Waziri Bashungwa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news