NA DIRAMAKINI
MKUU wa Mkoa wa Simiyu, Mheshimiwa David Kafulila amesema kuwa, katika mwaka wa fedha unaoanza mwezi Julai, 2022 anataka kwa kutumia nafasi ya Skauti wajipange ili waweze kutengeneza mazingira ambayo vijana wa skauti wanaweza kuzalisha alizeti kwa eneo lisilopungua hekari 10,000.
Ameyasema hayo Juni 17, 2022 wakati wa tukio la ugawaji wa vyeti vya heshima kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa vijana 16 wazalendo wa Kikosi Maalum ambao walishiriki kupanda Mlima Kilimanjaro kwa siku tatu Desemba 2021.
"Katika mwaka huu wa fedha ambao tunakwenda kuuanza mwezi wa saba, nataka kwa kutumia nafasi ya Skauti tujipange, tujipange ili kusudi tutengeneze mazingira ambayo vijana wa Skauti wanaweza kuzalisha alizeti kwa eneo lisilopungua hekari 10,000 kila mmoja akimiliki heka moja tu, eneo la heka 10,000 tuseme hili ni shamba la Skauti, na hii ndiyo shukurani yetu kwa Mheshimiwa Rais kama Skauti, kama mheshimiwa Rais anavyotupa heshima,lazima tushukuru;
Katika hafla hiyo ambayo ilifanyikia katika viwanja vya makao makuu ya Jeshi la Polisi wilayani Bariadi, Mheshimiwa Rais Samia aliwakilishwa na Skauti Mkuu wa Chama cha Skauti Tanzania, Hajjat Bi.Mwantum Bakari Mahiza.
Wageni wengine walioudhuria mbali na mkuu wa mkoa pia alikuwepo Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Mheshimiwa Lupakisiyo Kapange, Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Simiyu, ACP Blacius Chatanda na viongozi mbalimbali.