Waandishi waongeze elimu, wasema wadau kupitia Mkutano wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF)

NA GODFREY NNKO

WADAU mbalimbali wa habari wamesema kuwa, suala la elimu kwa waandishi wa habari nchini halikwepeki kwa kuwa, elimu itawezesha taaluma ya habari iheshimike, kuwa na weledi na kuzingatia maadili kwa manufaa ya taaluma, jamii na Taifa kwa ujumla.
Hayo wameyasema leo Juni 2, 2022 kupitia mkutano ulioandaliwa na Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) kwa njia ya Mtandao wa Zoom kuanzia saa nne asubuhi mpaka saa sita mchana huku mada kuu ikiangazia Mapendekezo ya Mabadiliko ya Sheria ya Habari nchini yaliyowasilishwa serikalini.

Wadau hao wamesema, baadhi ya vituo zikiwemo redio inaonekana watu wengi ambao wanafanya kazi huko, walienda kwa vipaji hivyo kusababisha ule weledi wa uandishi wa habari na utangazaji kukosekana, jambo ambalo halina afya katika tasnia ya habari.

Pia wamesema kuwa,majina mengi ya vipindi unakuta yanafanyika kwa lugha mchanganyiko kwa Kiingereza na Kiswahili, jambo ambalo ni changamoto.

"Suala la elimu ni jambo ambalo linapaswa lisisitizwe, lakini pia wakati wa msisitizo huo nasi waandishi wa habari tutumie muda huo kujiendeleza kielimu, tujisisitize wenyewe wakati tuna mambo mengine tunaomba Serikali ifanye, tunaziomba mamlaka zingine zifanye au taasisi zingine.

"Lakini sisi wenyewe, suala la elimu litusaidie sisi wenyewe, itatusaidia kwa sababu tunahudumia jamii, na hiyo jamii inayohudumia ikipata vitu visivyo maana yake inakuwa ni tofauti, mimi ninaunga mkono sana hoja ya elimu,"amesema mwanahabari Dkt.Tumaini Msowoya.

Naye mwanahabari, Bw.Godfrey Monyo amesema kuwa, elimu kwa wanahabari haikwepeki. "Wakati jitihada mbalimbali zikifanyika za kuhakikisha tunaboresha taaluma ya habari nchini, ninaomba suala la elimu lisisahaulike,watu wahakikishe kwamba maboresho yanakwenda, lakini waandishi wa habari wanasoma.

"Maboresho yawepo lakini, suala la elimu likaziwe mkazo. Mbona taaluma zingine zinajulikana kuwa, kiwango cha elimu ni hiki, naomba suala hili likaziwe mkazo,"amesema Bw.Monyo.

Wakili na mwanahabari, James Marenga akiwasilisha mada katika mkutano huo amesema, Sheria ya Makosa ya Mtandao ya mwaka 2015 ikiwemo Sheria ya Kupata Taarifa ya Mwaka 2016 na Kanuni zake za mwaka 2017 kuna baadhi ya vifungu au vipengele ambavyo vina changamoto ambavyo vikifanyiwa mabadiliko vitawezesha sheria hizo kuleta ufanisi.

"Kuna umuhimu wa kuwa na sheria rafiki za vyombo vya habari kwa maendeleo ya nchi na ni jambo lisilohitaji msisitizo mkubwa sana kwa sababu umuhimu wake unajulikana.

"Hivyo,kutungwa kwa sheria rafiki kwa vyombo vya habari kutawawezesha wadau wote wa habari wakiwemo waandishi wa habari kufanya kazi zao kwa kujiamini bila kukinzana na sheria kwa manufa ya Serikali na umma,"amefafanua.

Amesema, miongoni mwa vifungu ambavyo vina mapungufu katika sheria hiyo ni pamoja na 4 (1), 5 (1), 6(1),7(1), 7(3), 9, 11, 22(1) na 22(2) ambavyo vinazungukwa na neno “Intentionally" (kwa kudhamiria).

"Kuna umuhimu wa kurekebisha sheria na kufuta neno "kwa kudhamiria". Haiwezekani kuthibitisha nia ya kufanya uhalifu kwa maneno ya kubahatisha,"amesema.

Marega ametolea mfano vifungu vya 4(2), 5(2), 6(2), 7(1) (g), 7(2)(b), 7(3)(b), 8(2), 9(b), 10(2), 11(2), 12(2), 13(2),14(2)(a), 14(2)(b), 15(2), 16, 17(2), 18(2), 19(2), 20(2), 21(2), 22(1), 22(2), 23(2), 24 (2)(a), 24(2)(b), 26(3), 27, 29 na 45(3) ambavyo amesema kuwa, vimebebwa na neno "Not Less Than" likimaanisha 'Si Chini Ya' ambavyo kwa tafsri ya haraka vinaonekana kuwa ni changamoto.

"Mapungufu haya ya kutumia 'not less than' yanafungua milango kwa wale ambao wanatoa maamuzi kwa mfano mahakimu au majaji wakati mwingine kuweka adhabu kubwa zaidi na asiweze kutoa adhabu ambayo inalingana na kosa lililotendwa, au adhabu zingine wanazoona, tunasema sheria inapaswa ioneshe ukomo wa adhabu, mfano maneno kama 'not more than' (si zaidi ya) yanaweza kutumika ili kutenda haki na usawa,"amesema.

Pia Wakili Marenga amesema kuwa, muda wa mwandishi kupewa taarifa anazohitaji, unapaswa kupunguzwa kama ilivyo katika nchi zingine ndani na nje ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.

"Hapa Tanzania, mwandishi anapoomba taarifa, anasubiri kwa siku 30 huku Sudan Kusini akisubiria ndani ya siku saba, Rwanda ni siku tatu, Uganda siku 21 na Kenya ni siku 21,"amesema.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Bw.Deodatus Balile amesema kuwa,Juni 28, 2021jukwaa hilo lilipata fursa ya kukutana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan katika mkutano uliofanyikia Ikulu jijini Dar es Salaam.

Amesema, TEF ilimweleza Mheshimiwa Rais Samia umuhimu mkubwa wa kurekebisha sheria zinazohusiana na vyombo vya habari ili kuendana na viwango vya Kimataifa.

Bw.Balile amesema, Rais aliagiza iliyokuwa Wizara ya Habari, Sanaa, Michezo na Utamaduni kukaa pamoja na wadau ili kufanya marekebisho muhimu ambayo yatawezesha sheria kutabirika na kuwa wazi.

Amesema, Mheshimiwa Rais pia alichukua hatua ya kuihamisa Idara ya Habari Maelezo kutoka Wizara ya Habari, Sanaa, Michezo na Utamaduni kwenda Wizara ya Teknolojia ya Mawasiliano na Habari, kwa sasa inajulikana kama Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Bw. Balile amefafanua kuwa, TEF ilishauriana na Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) na kwa kushirikiana na wadau wengine wa habari chini ya Mkataba wa Muungano wa Haki ya Kupata Taarifa (CoRI) ulifanya mapitio ya sheria za vyombo vya habari ambayo yalisababisha mapendekezo ya marekebisho katika maeneo mbalimbali.

Akizungumzia kuhusu Sheria ya Huduma za Habari (Media Services Act), 2016, Bw.Balile amesema kuwa,katika sheria hiyo wanapendekeza maeneo zaidi ya 20 kufanyiwa maboresho.

Miongoni mwa maeneo hayo ni Kifungu cha 3 sheria ambacho kinatoa ufafanuzi usiyojitosheleza kuhusu ni nani mwandishi wa habari kwa kuwatenga wanahabari raia kupitia mchakato wa kibali.

"Ukienda kifungu cha tatu, sheria inatoa tafsri juu ya mwandishi wa habari ambapo inatambua waandishi wa habari ambao wamekwenda vyuoni wakapata mafunzo, lakini haiwatambui wale ambao wanaandika katika media za jamii. Tunapendekeza, sheria itambue waandishi wa habari katika makundi mawili, mosi Waandishi wa habari waliofunzwa nyumbani (kupitia ushauri) na waliofunzwa kitaaluma,"amesema.

Ametaja maeneo mengine ambayo yanahitaji kufanyiwa marekebisho kuwa ni Kifungu cha 5 (e) kinachoangazia utoaji wa leseni za magazeti, Kifungu cha 5 (1) kuhusu Uratibu wa Matangazo kutoka Serikalini.

"Hiki kipengele 5(1) tunapendekeza kifutwe, idara zote za Serikali zinapaswa kuwa huru kutoa matangazo kwa vyombo vya habari pasipo kusubiria kibali kutoka kwa Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo. Serikali inazo halmashauri 185, wizara 23, mikoa 26 ya Tanzania Bara na mitano Tanzania Zanzibar na mashirika zaidi ya 300, ni jambo lisilowezekana kwa matangazo yote ya taasisi za serikali kusimamiwa na mtu mmoja,"amesema.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

1 Comments

Previous Post Next Post

International news