NA GODFREY NNKO
WADAU wa vyombo vya habari kwa kushirikiana na Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) wamesema kuwa, Serikali inapaswa kuiangalia kwa namna ya kipekee Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016 ili baadhi ya vipengele ambavyo vinaonekana kuwa kikwazo vifanyiwe maboresho, kwa kuwa kufanya hivyo watasaidia Sekta ya Habari kustawi kwa kasi.
Hatua ambayo itawezesha kuchangia kukuza pato la Taifa, kufungua fursa za ajira kwa makundi mbalimbali zikiwemo rasmi na zisizo rasmi nchini.
Hayo wameyasema kwa nyakati tofauti wakati na baada ya mkutano ulioandaliwa na Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) kwa njia ya Mtandao wa Zoom Juni 2, 2022 huku mada kuu ikiangazia Mapendekezo ya Mabadiliko ya Sheria ya Habari nchini yaliyowasilishwa serikalini.
Wamesema, dhamira ya Serikali ya kutunga sheria na kanuni za kusimamia sekta ya habari ina nia njema kwa lengo la kuongeza ufanisi na ustawi bora, lakini kupitia sheria nne zinazosimamia habari zinahitaji maboresho katika baadhi ya vifungu ili kuepuka migongano ya maslahi, upendeleo, urasimu na wakati mwingine manyanyaso kwa wadau wa habari nchini.
Sheria hizo ni pamoja na Sheria ya Huduma ya Habari ya mwaka 2016, Sheria ya Mawasiliano ya Elektroniki na Posta (EPOCA) ya 2010 ambayo inasimamia radio, TV na Mitandao ya Kijamii, Sheria ya Haki ya Kupata Habari ya mwaka 2016 na Sheria ya makosa ya Mtandao ya 2015 zikiwemo kanuni za maudhui mtandaoni za mwaka 2018 ziliyogawanywa katika vipengele mbalimbali.
Deodatus Balile, Mwenyekiti wa TEF.
"Kwa leo tunazungunzia Kifungu cha 5 cha Sheria ya Huduma ya Habari ya mwaka 2016, kipengele hiki kina vifungu viwili ambavyo vinaleta shida kidogo. Kuna kifungu cha 5( l) na kifungu cha 5 (e) kifungu cha 5(e) kinampa Mamlaka Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo kusajili magazeti na hapa tumeona tatizo kubwa katika kusajili magazeti.
"Tulisema mwaka 2014, 2015 na mwaka 2016 wakati sheria hii ipo kwenye mchakato wa kupitishwa kwamba kifungu hiki kina nia ovu hatukueleweka. Lakini tumeshuhudia jinsi magazeti ya Mawio, Mwanahalisi, Mseto na Tanzania Daima yalivyofungiwa na wakati mwingine kunyang'anywa leseni kabisa yasifanye biashara na hapa tunasema kwamba kifungu hiki kifutwe kirejeshwe kama ilivyokuwa zamani ambapo mtu akisaji gazeti linakuwa la kudumu isipokuwa asipochapisha ndani ya miaka mitatu ndipo leseni yake inakuwa inajifuta.
"Sasa kwa kufanya hivi unapofuta leseni au unasitisha unakuta unaathiri mawasiliano kati ya wasomaji na chombo cha habari kilichofungiwa, lakini sio hiyo tu kuna wafanyakazi wengi ambao wanfanya kazi kwenye magazeti kwenye radio na kwenye TV nao pia wanaathirika,"anasema Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF),Bw.Deodatus Balile.
Bw. Balile anasema kuwa, leseni inapokuwa imeondolewa inaletata shida kwa sababu wale watu ambao walitegemea chombo husika kama sehemu ya ajira wanataabika.
"Wengine wanaishi maisha ya dhiki sana. Lakini kunakuwepo mikataba mbalimbali mikataba ya matangazo, mikataba ya huduma kwa jamii, gazeti linaponyang'anywa leseni au ikafutwa kwa utaratibu huu wa kusajiliwa linakuwa linashida.
Kifungu cha 5 (1)
Pia Bw.Balile anasema, katika maboresho hayo kuna umuhimu wa kipekee wa Serikali kukifuta Kifungu cha 5 (l) ambacho anasema pia kina kasoro.
"Kifungu hicho nacho kifutwe kwa maana kinaweka mamlaka au madaraka ya kukusanya, kuchakata na kusambaza kwa vyombo vya habari matangazo yoote ya Serikali na taasisi zake kwa mtu mmoja ambaye ni Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo.
"Kifungu hiki, kinaleta urasimu na kinaleta hatari ya mtu mmoja kuwa na madaraka makubwa ambayo ama kitaleta urasimu ama mazingira ya rushwa, kwamba kama mtu atakuwa hafahamiani naye atakuwa hajazungumza naye vizuri atajikuta kwamba ananyimwa matangazo,"amesema Bw. Balile.
"Kama alivyoelekeza Mheshimiwa Rais Samia tarehe 28 Juni,2021 kwamba vyombo vya habari vipewe matangazo kwa njia ya ushindani, tunapenda sana vyombo vya habari vipewe matangazo kwa njia ya ushindani na sio kwa njia ya upendeleo au kwa njia ambazo zinaleta mashaka kwa hiyo tutaendelea kuzungumza.
"Na tunamshumuru waziri mwenye dhamana na masuala ya habari, Waziri wa Habari Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mheshimiwa Nape Nnauye amesema mara zote tutaendelea kuzungumza, tutaelewana mpaka vifungu vipi vifike hatua ipi kwa ajili ya kuwa na sheria iliyo bora kabisa, sheria zilizo bora kabisa zinazo ruhusu uburu wa vyombo vya habari, lakini zinaweka wajibu kwa watendaji na waandishi wa vyombo vya habari kwa maana kwamba kila uhuru, kila haki inakuja na wajibu wake."amesema Balile.
Wakili
Naye Wakili na mwanahabari, James Marenga akiwasilisha mada katika mkutano huo amesema, Sheria ya Makosa ya Mtandao ya mwaka 2015 ikiwemo Sheria ya Kupata Taarifa ya Mwaka 2016 na Kanuni zake za mwaka 2017 kuna baadhi ya vifungu au vipengele ambavyo vina changamoto ambavyo vikifanyiwa mabadiliko vitawezesha sheria hizo kuleta ufanisi.
"Kuna umuhimu wa kuwa na sheria rafiki za vyombo vya habari kwa maendeleo ya nchi na ni jambo lisilohitaji msisitizo mkubwa sana kwa sababu umuhimu wake unajulikana.
"Hivyo,kutungwa kwa sheria rafiki kwa vyombo vya habari kutawawezesha wadau wote wa habari wakiwemo waandishi wa habari kufanya kazi zao kwa kujiamini bila kukinzana na sheria kwa manufa ya Serikali na umma,"amefafanua.
Amesema, miongoni mwa vifungu ambavyo vina mapungufu katika sheria hiyo ni pamoja na 4 (1), 5 (1), 6(1),7(1), 7(3), 9, 11, 22(1) na 22(2) ambavyo vinazungukwa na neno “Intentionally" (kwa kudhamiria).
"Kuna umuhimu wa kurekebisha sheria na kufuta neno "kwa kudhamiria". Haiwezekani kuthibitisha nia ya kufanya uhalifu kwa maneno ya kubahatisha,"amesema.
Marega ametolea mfano vifungu vya 4(2), 5(2), 6(2), 7(1) (g), 7(2)(b), 7(3)(b), 8(2), 9(b), 10(2), 11(2), 12(2), 13(2),14(2)(a), 14(2)(b), 15(2), 16, 17(2), 18(2), 19(2), 20(2), 21(2), 22(1), 22(2), 23(2), 24 (2)(a), 24(2)(b), 26(3), 27, 29 na 45(3) ambavyo amesema kuwa, vimebebwa na neno "Not Less Than" likimaanisha 'Si Chini Ya' ambavyo kwa tafsri ya haraka vinaonekana kuwa ni changamoto.
"Mapungufu haya ya kutumia 'not less than' yanafungua milango kwa wale ambao wanatoa maamuzi kwa mfano mahakimu au majaji wakati mwingine kuweka adhabu kubwa zaidi na asiweze kutoa adhabu ambayo inalingana na kosa lililotendwa, au adhabu zingine wanazoona, tunasema sheria inapaswa ioneshe ukomo wa adhabu, mfano maneno kama 'not more than' (si zaidi ya) yanaweza kutumika ili kutenda haki na usawa,"amesema.
Waandishi
Kwa nyakati tofauti, waandishi na wadau mbalimbali katika mkutano huo walisema kuwa, panapotokea tofauti baina ya wamiliki wa vyombo vya habari na Serikali, hadi kusababisha vyombo husika kufungiwa, waathirika wakubwa ni wafanyakazi ambao sehemu hiyo imekuwa ikiwapa kipato cha kuendesha familia zao.
"Awali ya yote, nichukue nafasi hii kuipongeza Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais mama yetu, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa namna ambavyo ameonesha kutujali sana wanahabari na tasnia hii kwa ujumla, ule moyo tu wa kuonesha utayari wa tasnia hii kuthaminiwa zaidi katika Serikali yake inatupa majibu kuwa, hata kasoro ndogo ndogo ambazo zinaonekana katika vifungu vya sheria hizo zitafanyiwa maboresho na tutafanya kazi kwa uhuru na vyombo vya habari thamani yake itarudi kwa kasi,"anasema mmoja wa wadau wa habari kutoka mkoani Mara.
Amefafanua kuwa,panapotokea hatua ya vyombo vya habari kukosa biashara au kunyimwa matangazo kunachangia wamiliki wengi kuamua kusitisha biashara na hata wakati mwingine wanashindwa kulipa malimbikizo ya madeni ya wafanyakazi na kodi mbalimbali za Serikali.
"Ni shauku yetu kuona siku moja kila chombo cha habari ambacho kina leseni halali nchini, kinapewa biashara na taasisi yoyote ya umma au binafsi bila kujali ukubwa au udogo wake, hii inamaanisha nini? Wakipata biashara inachochea kasi ya uwekezaji, fursa za ajira na hata kuwa na mwamko wa kulipa kodi kwa wakati serikali, hivyo kuwezesha ustawi wa uchumi wetu. Sekta ya habari ni muhimu sana,"amesema.