Wakulima wa Pamba wakiri kuheshimishwa kupitia 'Simiyu Model',yatoa azimio la pongezi kwa Rais Samia

NA DIRAMAKINI

HALMASHAURI Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Simiyu imempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kukubali Mfumo Maalum wa Ununuzi wa Pamba mkoani Simiyu (Simiyu Model).
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Bi. Shamsa Mohammed wakati akitoa azimio la pongezi kwa niaba ya wajumbe katika kikoa kazi cha kutathimini mfumo wa ununuzi wa pamba kilichohudhuriwa na Bodi ya Pamba nchini na Sekretarieti ya Mkoa na kusema mfumo huo utakuwa endelevu.
Kikao hicho cha Juni 13, 2022 ambacho kilifanyika Mjini Bariadi, wadau walisema kuwa, hapo awali mkulima hakupata nafasi ya kushirikishwa katika udhibiti wa ubora wa pamba, hivyo kukosa faida ikilinganishwa na msimu huu.

Baadhi ya wakulima wa zao la pamba mkoani Simiyu wameeleza kiridhishwa na mfumo huo jumuishi wa ununuzi wa pamba baina ya wakulima, Serikali vyama vya msingi vya ushirika, wanunuzi wa pamba na wadau wengine.

Wakulima wamekiri wazi kuwa, mfumo huo, licha ya kuwa wa uwazi umedhibiti unyonyaji ulipokuwa unafanyika kipindi cha nyuma kwa wakulima.

Pia wamesema kuwa,mfumo huo umekuwa na tija tofauti na mwaka jana kwa kuwa,ununuzi wa pamba umekuwa wazi ambapo kila mtu anakuwa anaelewa ushindani uliopo katika soko pamoja na mabadiliko ya bei.

Wameongeza kuwa, kwa sasa wakulima hao wanakabiliwa na changamoto ya wizi wa pamba inapokuwa shambani pamoja baadhi ya wakulima kuficha pamba wakisubiri kuuza pamba kwa kuchelewa ili wauze kwa bei ya juu.

Aidha, wamesema Simiyu Model ni mfumo jumuishi kati ya wadau wapamba na wakulima pamoja na vyama vya ushirika ambapo maazimio ya kikao hicho yaliazimia kuwa, mfumo umeleta ushindani katika soko.

Hali iliyosababisha ongezeko la bei ya ununuzi wa pamba isipokuwa tahadhari zichukuliwe ili kudhibiti ubora wa pamba inayoingizwa sokoni pamoja na kudhibiti mianya ya unyonyaji wa jasho la wakulima na rushwa.

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mheshimiwa David Kafulila amesema, msingi mkubwa wa mfumo huo ni kutengeneza mnyororo na kumfanya mkulima aweze kunufaika kupitia jasho lake.

Amesema,bahati mbaya katika kufikia dhima hiyo kuna baadhi ya viongozi wa Serikali kwenye wilaya wamekuwa wakitumia mianya hiyo kula jasho la wakulima, jambo ambalo haliwezi kukubalika.

Mheshimiwa Kafulila amesema,mfumo uliopo umechangia vyama vya msingi vya ushirika kwa maana ya AMCOS kufanya vizuri hadi sasa kwenye ununuzi wa pamba.

Amesema, changamoto pekee anayowapa wakuu wa wilaya ni kuhakikisha kila siku wanajua kilo za pamba zilizonunuliwa pamoja kujua changamoto zilizojitokeza katika ununuzi wa pamba.

Pia ameongeza kuwa, maofisa wanaohusika na mizani wahakikishe wanajua idadi ya mizani inayotumika katika ununuzi wa pamba ifikapo leo Juni 17, 2022 ili kudhibiti matumizi ya mizani isiyokidhi vigezo na matamanio ni kuona AMCOS zinakuwa bora zaidi ili watu wasione sababu ya kununua nje ya AMCOS.

Kwa upande wake, Naibu Mrajisi wa Vyama vya Ushirika, Udhibiti wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika, Bw.Collins Nyakunga amesema katika ukaguzi uliofanyika tangu kufunguliwa kwa msimu mwaka huu amebainisha kuwa baadhi ya AMCOS hazitoi stakabadhi za malipo.

Amesema, hali hiyo inawapa wasiwasi kwa sababu stakabadhi ni haki ya mkulima anayekuwa ameuza pamba na yote ni kwa sababu kuna watendaji wanajisahau kusimamia majukumu yao ipasavyo ili kila jambo liende vema.

Nyakunga amevishauri vyama vya ushirika kuhakikisha vinakuwa na vitabu kwa ajili ya kutunza kumbukumbu maana vyama hivyo ni taasisi, hivyo lazima ziwe na taarifa zake na sio makampuni na baadhi ya mikataba ya makumpuni na vyama vya ushirika huku akiwataka watendaji waende wakasimamie vizuri jambo hilo.

Mkurugenzi wa Bodi ya Pamba nchini, Marco Mtunga amesema kuwa, ukitaka kutatua tatizo lazima ujue kuwa tatizo lipo.

"Kimsingi Bodi ya Pamba inakubali kwamba kulikuwa na matatizo na ni kweli kwamba mwaka jana wakulima hawajatendewa haki na tangu kuanza kwa msimu huu AMCOS wapo vizuri kwa sababu vitu walivyokuwa wanafanya nyuma havipo ndio maana kwa sasa ushindani umekuwa mkubwa sana,"amesema Bw.Mtunga.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news