NA DIRAMAKINI
NAIBU Mtendaji Mkuu wa kampuni mpya ya tumbaku Amy Holdings, Bw.Richard Sinamtwa amefanya ukaguzi wa maandalizi ya soko la tumbaku eneo la vyama vya msingi ambavyo msimu huu vilikosa mnunuzi wa zao hilo wa mkataba na kuahidi kuwa kampuni yake itanunua tumbaku yote iliyoko eneo hilo.
Naibu Mtendaji Mkuu wa Amy Holdings, Bw. Richard Sinamtwa akikagua tumbaku iliyoko kwenye ghala la chama cha ushirika cha KACU huko wilayani Mbogwe mkoani Geita.
Awali aliambiwa kuwa, vyama vya msingi hivyo baada ya kukosa msaada kutoka kwa makampuni ya ununuzi tumbaku yaliyopo nchini, maamuzi yalifanyika ili visimamiwe na chama kikuu cha ushirika cha wilayani Kahama mkoani Shinyanga (KACU).
"Vyama hivi vilisimamiwa na Chama Kikuu cha Ushirika (KACU) kama mnunuzi mtarajiwa, kwani vinginevyo wakulima wangeshindwa kulima zao hilo,"alisema.
Kampuni hiyo mpya ambayo tayari imeanza ununuzi wa zao hilo kutoka kwa wakulima imewapongeza KACU kwa maamuzi ya kusimamia vyama vya msingi hivyo kwa kugawa pembejeo na kutoa huduma za ugani kwenye vyama vya msingi na hivyo sasa kampuni hiyo ndiyo itanunua zao hilo.
"Sisi tutanunua zao lote lililolimwa na wakulima hawa, kwani nguvu tunayo,uwezo tunao na ari ipo,"amesema Bw.Sinamtwa.
Kampuni ya kizalendo ya Amy Holdings ndiyo iliyonunua mali za kampuni ya kimarekani ya TLTC ambayo ilifunga shughuli zake hapa nchini miaka mitatu iliyopita.
Miongoni mwa mali za zilizonunuliwa ni pamoja na kiwanda cha TTPL cha Morogoro ambacho nacho kilifungwa, lakini sasa wawekezi wapya wamepanga kukifungua rasmi mwezi ujao.