WANAWAKE WAWEZESHWE:Kwenye kazi wawe nguzo, wala si kupata kiki

NA LWAGA MWAMBANDE (KiMPAB)

JUNI 20, Mwaka huu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amemuelekeza kuhakikisha wanawake katika Utumishi wa Umma wanajengewa uwezo kiutendaji ili waweze kushika nafasi za uongozi na kufanya maamuzi kwa maendeleo ya taifa.

Mhe.Mhagama amesema hayo jijini Dar es Salaam, wakati akizindua programu ya wanawake na uongozi katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere.

Amesema, alimueleza Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan juu ya uzinduzi wa programu ya wanawake na uongozi, hivyo miongoni mwa maagizo aliyompatia ni kuhakikisha wanawake wanajengewa uwezo wa kiutendaji kupitia Taasisi ya UONGOZI ili wawe na uwezo wa kushika nafasi za maamuzi.

Waziri Mhagama amesema kwa asili, wanawake wana uwezo mkubwa wa kufanya kazi nyingi kwa wakati mmoja, kwa ufanisi na ni waaminifu, hivyo wakipewa mafunzo na nafasi za uongozi watatekeleza majukumu yao kikamilifu.

“Kama wanawake wengi wamefanikiwa kuongoza makampuni na taasisi za umma na zikafanya vizuri, ina maana tukiwa na wanawake wengi katika nafasi za uongozi ni wazi kuwa taifa litapiga hatua kubwa katika maendeleo,” Mhe. Mhagama amefafanua.

Ameongeza kuwa, ni lazima kuwa na mipango ya kuwaibua wanawake wenye uwezo na kuwajengea hali ya kujiamini ili kuwa tayari kulitumikia taifa kwa bidii na uzalendo.

Mshairi wa kisasa, Bw.Lwaga Mwambande kupitia shairi lake kwa kutambua, kuthamini na kuheshimu mchango wa mwanamke katika maendeleo ya jamii na Taifa kwa ujumla anakazia jambo kupitia shairi lake, unaweza kujifunza kitu, karibu;

1:Kama Rais atiki, kiti anakimiliki,
Wanawake ni mantiki, kuongoza iwe haki,
Tupokee tuafiki, agizo hili la haki,
Wanawake wawezeshwe, waongoze Serikali.

2:Kuwajengea uwezo, Rais amebariki,
Kwenye kazi wawe nguzo, wala si kupata kiki,
Hili kwa wote tangazo, kwa vitendo tubariki,
Wanawake wawezeshwe, waongoze Serikali.

3:Zicheki menejimenti, nyingi kama halaiki,
Wanawake kama senti, silimia hazifiki,
Bora weka hata tenti, wafundishwe wawe laki,
Wanawake wawezeshwe, waongoze Serikali.

4:Serikali yetu sote, jinsia tuimiliki,
Nafasi sote tupate, nchi ipate riziki,
Wake na waume wote, tuwaone tuwacheki,
Wanawake wawezeshwe, waongoze Serikali.

5:Nchi hii yetu sote, Mungu ametubariki,
Na tena jinsia zote, uongozi tumiliki,
Tuiendeleze sote, mbeleni tukale keki,
Wanawake wawezeshwe, waongoze Serikali.

6:Kuwajengea uwezo, kuongoza kwao haki,
Wala kwao siyo dezo, hekima wanamiliki,
Mifumo ndiyo kikwazo, nafasi hawazishiki,
Wanawake wawezeshwe, waongoze Serikali.

7:Taasisi Uongozi, yatenda jambo la haki,
Kufundisha uongozi, wanawake ni muziki,
Wawe wengi kwenye kazi, kama waume watiki,
Wanawake wawezeshwe, waongoze Serikali.

8:Rais Samia wetu, nchi haitetereki,
Huyu kiongozi wetu, tunaona anatiki,
Mwanamke huyu kuntu, anateleza na chaki,
Wanawake wawezeshwe, waongoze Serikali.

9:Kama Rais kaweza, kitini hakamatiki,
Wanawake wanaweza, uongozi kumiliki,
Na wengine waongoza, wengi tunawalaiki,
Wanawake wawezeshwe, waongoze Serikali.

10:Heri tunawatakia, stadi kuzimiliki,
Malengo weze timia, viongozi muwe laki,
Taifa kutumikia, nchi ijae samaki,
Wanawake wawezeshwe, waongoze Serikali.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news