Waona nuru kupitia elimu ya kutokomeza ukatili wa kijinsia wilayani Serengeti

NA FRESHA KINASA

IMEELEZWA kuwa, hatua ya Shirika la Hope for Girls and Women in Tanzania (HGWT) linalojishughulisha na mapambano ya vitendo vya ukatili wa kijinsia na kutetea haki za binadamu lenye makao makuu yake Mugumu Wilaya ya Serengeti Mkoa wa Mara kwa kushirikiana na Dawati la Jinsia na Watoto (Polisi), Maendeleo ya Jamii na Ustawi wa Jamii kuunda klabu za wanafunzi za kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia na kutoa elimu ya madhara ya vitendo hivyo katika shule za msingi 48 wilayani humo hivi karibuni kutaongeza ufanisi katika kutokomeza vitendo hivyo. 
Hayo yamesemwa na baadhi ya wananchi wa wilaya hiyo wakati wakizungumzia mtazamo wao kuhusu namna ambavyo zoezi la utoaji wa elimu kwa wanafunzi linavyoweza kusaidia katika kupambana na vitendo vya ukatili wa kijinsia ikiwemo ukeketaji, ndoa za utotoni na aina mbalimbali za ukatili wa kijinsia. 

Neema Wambura mkazi wa Mugumu ameiambia DIRAMAKINI kuwa, elimu ndio njia sahihi na muhimu ya kutokomeza ukeketaji na ndoa za utotoni kwani wanafunzi waliopata ufahamu wa madhara yake msukumo wao na ushiriki wao katika kupambana unakuwa mkubwa na kwamba hawawezi kuona mtu akifanya ukatili wamfumbie macho. 

"Hope for Girls pamoja na Dawati la Jinsia, Maendeleo ya Jamii na Ustawi wameendelea kufanya ushirikiano mzuri kupeleka elimu katika shule zetu wakiwa kma timu. Wanafunzi hao ndio mabalozi wa kufichua watu wanaoendeleza mila ya ukeketaji. Wameambiwa ukeketaji unasababisha kutokwa damu nyingi, kuathirika kisaikolijia, magonjwa ya kuambukiza, lazima watakuwa mstari wa mbele kupinga vitendo hivyo kwa sababu madhara wanayatambua hili ni Jambo la muhimu katika kufanikisha.

"Mwangu anasoma darasa la pili ni mdogo siku moja ameniambia alipofika nyumbani shuleni tumefundishwa ukatili ni kosa kisheria, kuwakeketa mabinti ni kosa na anataja madhara ya ukeketaji kumbe elimu hiyo waliyofundishwa inawaingia akilini. Mtoto anakuwa akifahamu madhara ya mila hii tegemea kwamba huyo tayari amekuwa na ufahamu na atakua akitambua vyema madhara. Mimi anadiriki kuniambia shuleni tumeambiwa watoto wa kike wasomeshwe sio kukeketwa huyo tayari amekuwa balozi wa kutoa elimu kwa wengine,"amesema Naomy Paul. 
Naye Amina Petro Mkazi wa eneo la misitu Mugumu amesema kuwa, zamani hapakuwa na juhudi kubwa za kupambana na ukeketaji kama sasa na kwamba ukeketaji ulikuwa kama fasheni, huku baadhi ya mabinti waliokeketwa walipata madhara makubwa sana na baadhi yao kupoteza maisha lakini bado ulifanyika lakini kwa sasa unafanyika kwa kificho na usiku na wakati mwingine wanaokeketwa hulazimishwa kwa nguvu kwani tayari wanafahamu madhara yake. 

"Kutokana na elimu kuendelea kutolewa wapo Wazazi na walezi wanatumia nguvu kukeketa, lakini unakuta tayari binti ameshafundishwa madhara na pia hataki kukeketwa. Uwepo wa Shirika la Hope for Girls and Women in Tanzania limesaidia sana wasichana kuendelea na masomo yao kwani wengi hukimbilia katika Kituo cha Hope Mugumu Nyumba Salama' kinachomilikiwa na shirika hilo kupata hifadhi na huendelezwa kielimu Jambo ambalo lina tija kwa manufaa ya mtoto wa kike," amesema. 
Paulo Fabian ameshukuru Serikali wilayani Serengeti na Mkoa wa Mara kwa ujumla kwa kuendelea kulaani vikali ukeketaji na kumchukua hatua kali za kisheria kuwafikisha mahakamani wale wanaofanya ukeketaji. Ambapo pia ameomba wazee wa Kimila kuisaidia Serikali kukomesha vitendo hivyo sambamba na kuwafichua wanaofanya kwa Siri mbele ya sheria. 

"Mimi naungana na Serikali pamoja na Shirika la Hope kupinga ukeketaji kwa sababu hauna tija. Bali unadidimiza Maendeleo na mafanikio ya mtoto wa kike kwa siku za usoni. Tutambue kuwa elimu pekee ndio urithi wa thamani kwa Watoto wa kiume na Watoto wa kike, tuweke mkazo na usawa katika kusomesha na kuwaandaa kuwa Viongozi na waleta maendeleo kwa siku za usoni katika Jamii yetu na Taifa letu. Najua msimu wa ukeketaji unakuja niombe Serikali ikiwakamata wanaofanya kitendo hicho iwape adhabu kali,"amesema Nelda Yusto. 

Costantine John pia amesema kuwa, jamii inayokumbatia mila hiyo inatambua fika kuwa ni kosa kisheria lakini bado inafanya hivyo kama sehemu ya kujipatia kipato na hivyo anashauri kazi mbadala zifanywe hususani ngariba wafanye kazi ya ujasiriamali biashara, Kilimo, ufugaji na kuachana na kitendo hicho ambacho ni kinyume Cha sheria za nchi na haki za binadamu.

"Halmashauri inatoa mikopo kwa hiyo ngariba ambao wanadhani watakosa kipato wanachopata kutonana na ukeketaji niwashauri wajiunge kwenye vikundi Kama ambavyo Serikali imekuwa ikisisitiza inazofedha za kuwakopesha kinamama, vijana na wenye ulemavu waachane na kitendo hicho ambacho kitawatia hatiani bure," amesema Costantine John.
"Wapo wasichana ambao walikimbia kutoka katika familia zao wakapata hifadhi Kituo cha Hope Mugumu Nyumba Salama na kuendelea na masomo yao leo hii baadhi yao wamegeuka kuwa lulu katika familia zao wakizisaidia na wazazi wanafurahia kwa wamesahau kwamba wasingepata hifadhi na kuendelezwa wasingefikia hatua husika. Nishauri elimu iwe ndio kipaumbele kwa Watoto wetu haijalishi wa kiume au wa kike tuwape fursa sawa ya kusoma kwani hao ndio Madaktari wetu, wanasheria, mapolisi, Wauguzi na Wabunge kwa miaka ijayo,"amesema Jesca Anthony.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news