NA FRESHA KINASA
WATOTO wa Mfalme wa Saudi Arabia,Salman bin Abdulaziz Al Saud wametembelea Kituo cha Hope Mugumu Nyumba Salama kilichopo Mugumu Wilaya ya Serengeti Mkoa wa Mara kinachotoa hifadhi kwa wasichana waliokimbia aina mbalimbali za ukatili wa kijinsia kutoka katika familia zao.
Kituo hicho, kinamilikiwa na Shirika la Hope for Girls and Women in Tanzania (HGWT) linalojishughulisha na mapambano ya ukatili wa kijinsia na kutetea haki za binadamu chini ya Mkurugenzi wake, Rhobi Samwelly.
Wamefanya ziara ya kutembelea kituo hicho leo Juni 29, 2022 ambapo wamepongeza juhudi thabiti zinazofanywa na shirika hilo katika kuhakikisha watoto wa kike linawasaidia kuwalinda na kuwaendeleza kielimu na kifani kusudi wafikie ndoto zao.
Aidha, wameahidi kuendelea kushirikiana na shirika hilo ikiwemo kuliunga mkono kwa kulisaidia liweze kufanya vizuri zaidi katika mapambano ya vitendo vya ukatili wa kijinsia kutokomeza ukeketaji, ndoa za utotoni na aina mbalimbali za ukatili.
Kwa upande wake Mkuu wa Kituo cha Hope Mugumu Nyumba Salama, Daniel Misoji amewashukuru kwa kufika katika kituo hicho ambapo amesema kuwa, shirika hilo kupitia kituo hicho limeendelea kuwapa hifadhi wasichana ambao hukimbia makwao kupata hifadhi kituoni hapo.
Pia limekuwa likihakikisha wanaosoma wanaendelea na masomo yao na kwa wale ambao huwa wamehitimu huwatafutia vyuo mbalimbali na kuwagharamia kusudi watimize ndoto zao na wajikwamue kiuchumi.