NA MWANDISHI WETU-PSC
KATIBU wa Tume ya Utumishi wa Umma, Bw. Mathew M. Kirama amewataka watumishi wa tume hiyo kufanya kazi kwa uadilifu, kuzingatia sheria na kulinda haki za watu ambao wanawahudumia ili uamuzi unaotolewa katika rufaa na malalamiko yanayowasilishwa tume uwe ni uamuzi wa haki na haki tupu wakati wote.
Bw. Kirama amesema hayo wakati anafungua mafunzo kuhusu usimamizi wa mfumo wa vihatarishi katika Taasisi kwa ngazi ya Menejimenti ya Tume, Wakuu wa Sehemu na Wajumbe wa Kamati ya Ukaguzi ya Tume ya Utumishi wa Umma, mafunzo yaliyofanyika jana katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi jijini Dodoma.
"Watumishi wa Tume mnayo dhamana ya kumsaidia Mheshimiwa Rais kutekeleza majukumu yake. Ni dhamana kubwa, na kwa sababu hiyo ni lazima muilinde dhamana hiyo mliyopewa kwa kuhakikisha wakati wote mnafanya kazi kwa bidii. Hakikisheni wakati wote mnafanya kazi kwa uadilifu, mnazingatia maadili, Sheria na mnalinda haki za watu ambao mnawahudumia ili uamuzi unaotolewa katika rufaa na malalamiko yao wanayowasilishwa Tume uwe ni uamuzi wa haki na haki tupu.
“Akitokea mteja wetu mrufani amekata rufaa, akate rufaa kwa sababu anatumia haki yake ya msingi na uamuzi ukitolewa, haki hiyo ionekane imetendeka mbele ya macho ya Sheria. Hili ni jambo ambalo kila mmoja wetu anapaswa kuliona na kulisimamia kwa nguvu zetu zote na ndio maana tupo hapa," amesema Bw. Kirama.
Akizungumzia kuhusu umuhimu wa mafunzo hayo amesema, tume ni rekebu inatakiwa kuwa juu katika viwango vya uzingatiaji wa Sheria, Sheria ya Utumishi wa Umma Sura 298 [marekebisho ya mwaka 2019] na Sheria nyingine zinazotuongoza katika utekelezaji wa majukumu yetu. Aliishukuru Ofisi ya Mkaguzi wa Ndani Mkuu wa Serikali kwa kuipatia Tume mwezeshaji na alisema kuwa Tume inakusudia kuwa na mfumo mzuri zaidi wa usimamizi wa vihatarishi katika mwaka ujao wa fedha wa 2022/2023.
"Tukiweza kuainisha vizuri vihatarishi vilivyo katika Tume yetu maana yake malengo tuliyojiwekea tutayafikia. Kushindwa kufanya hivyo tutabaki tunazungumza tu katika daftari ambalo halina matokeo. Ni lazima kuwe na matokeo kwa sababu kuna watu tunaowahudumia ndio watakaotupima ama tumefanikiwa au hatujafanikiwa. Ni matarajio yangu kuwa baada ya mafunzo haya tutakwenda kutekeleza, ili wenzetu wanaotupima waone usimamizi wa vitaharishi katika Ofisi ya Rais, Tume ya Utumishi wa Umma unatekelezwa ipasavyo," alisisitiza Bw. Mathew M. Kirama.
Kwa upande wake, mwezeshaji kutoka Ofisi ya Mkaguzi wa Ndani Mkuu wa Serikali, Bw. Onesmo Mbekenga, alisema ni muhimu kwa kila Taasisi ya Umma kuwa na mfumo wa vihatarishi ambao unasimamiwa, unatekelezwa na kufanyiwa tathmini vizuri ili kuisaidia Taasisi kuweza kufikia malengo yake.