NA SHEILA KATIKULA
WAVUVI wametakiwa kuacha kujisaidia kwenye vyanzo vya maji, na badala yake watumie vyoo bora ili waweze kuepuka ugonjwa wa kichocho.
Hayo yamesemwa na Mwezeshaji kutoka kwenye Mradi wa Afya ya Jamii na Maendeleo (CHADF), Meshack Makojoji wakati akitoa elimu juu ya kujiepusha na ugonjwa wa kichocho uliyotolewa kwa wavuvi wa mwalo wa Igombe Beach uliopo wilayani Ilemela jijini hapa.
Amesema, ni vema wavuvi kutumia choo kwa usahihi ,kuepuka kuogelea kwenye maji yaliyotuama, kuepuka kujisaidia kwenye vyanzo vya maji.
Hata hivyo, ameongeza ni vema kunywa maji yaliyochemshwa yenye dawa ,kuosha mikono kabla ya kula ,baada ya kutoka chooni na kutumia dawa elekezi kutoka kwa madaktari sanjari na kutunza vyanzo vya maji.
"Ili kuepuka maambukizi ya ugonjwa huo ni vema kufuata ushauri wa wataalamu wa afya kwa kutumia vyoo bora,kuchemsha maji ya kunywa,kuepuka kuogelea kwenye maji yaliyotuama.
"Kichocho ni ugonjwa unaosabanishwa na minyoo na unaweza kuwa wa muda mfupi au sugu na maambukizi yake hutokea endapo mtu ataogelea kwenye maji yenye konokono wanaobeba vimelea vya ugonjwa huo na mtu aliyeambukizwa akijisaidia kwenye maji hayo,"amesema.
Naye muelimishaji kutoka kwenye mradi wa Chadf, Abdulkarim Nyambi amesema dalili za ugonjwa huo ni kuwashwa ngozi,kukohoa,maumivu ya kichwa,tumbo,misuli kuwasha,maumivu ya maungio na mifupa,maumivu wakati wa kukojoa,kupata homa,kukojoa damu.
Kwa upande wake mvuvi wa mwalo wa Igombe Beach,Kalenga Kalenga ameiomba Serikali kutoa elimu kwa wavuvi ili waweze kujikinga na ugonjwa huo.
Naye msimamizi wa kambi ya wavuvi ya Malando iliyopo Igombe beach,Kulwa Mayala amesema elimu waliyoipata kupitia Mradi wa Afya ya Jamii na Maendeleo (CHADF) itawasaidia kuacha kujisaidia kwenye vyanzo vya maji ili kuepuka ugonjwa huo.
"Tunawashukru wataalamu wa afya kwa kuona umuhimu wa kutembelea mwalo huu na kutoa elimu hii lakini tuna changamoto ya vifaa kinga kama viatu vya mpira (Rain boots) visipopatikana bado tatizo litabaki kwani kazi zetu tunafanya kwenye maji na tunatembea bila viatu tukiwa hapa mwaloni,"amesema Mayala.