Mapato Stendi Kuu ya Magufuli Mbezi yapaa, agizo la Waziri Bashungwa lafungua njia

NA DIRAMAKINI

SIKU chache zikiwa zimepita tangu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Innocent Bashungwa kutoa siku saba kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla kukutana na LATRA, Wadau na Wamiliki wa Mabasi kuweka uratibu mzuri wa kusimamia maelekezo ya Serikali kwa mabasi yote kushusha na kupakia abiria ndani ya Kituo Kikuu cha Mabasi cha Magufuli jijini Dar es salaam, hatimaye kuna mafanikio yameanza kuonekana.
Kwa mujibu wa Ofisi ya Rais-TAMISEMI,mapato ya Kituo Kikuu cha Mabasi cha Magufuli yameongezeka kutoka shilingi 7,165,100  hadi shilingi 8,244,100 kwa siku.

Hii ni sawa na ongezeko la Shilingi 1,079,000 kwa siku na limetokana na ziara ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhe. Innocent Bashungwa alipofanya ziara yake Mei 30,2022 na kutoa maelekezo mahususi kuhusu uboreshaji wa mapato ya Stendi hiyo.

Maeneo yanaonekana kufanya vizuri ni  viingilio vya getini, ushuru wa choo pamoja na adhabu mbalimbali.

Wakat ihuo huo Ofisi ya Rais - TAMISEMI wameielekeza  Manispaa hiyo kuboresha usimamizi na kuboresha huduma katika kituo hicho ili mapato yanayopatikana yaende sambamba na huduma bora na usimamizi makini.
Waziri Bashungwa alitoa maelekezo hayo wakati akikagua mradi wa Kituo Kikuu cha Mabasi cha Magufuli (Magufuli Bus Terminal) kilichopo Wilaya ya Ubungo jijini Dar es Salaam.

Alisema, Serikali imetumia kiasi cha shilingi bilioni 50 kujenga kituo hicho, hivyo Serikali haitakubaliana na watu ambao hawazingatii utaratibu uliowekwa katika kituo hicho.

“Ninafahamu kuwa Mkuu wa Mkoa, Amos Makalla ameshapokea changamoto ya Mabasi kutoingia ndani ya kituo hiki cha Magufuli na mimi nimekuta changamoto bado iko pale pale, sasa kwa sababu ameshanza kulifanyia kazi nampa siku saba awe amekutana na LATRA pamoja na wadu wa mabasi (TABOA) kuangalia utaratibu wa mabasi yote kuingia ndani ya kituo kushusha na kupakia abiria,”amesema Bashungwa.

Pia Mheshimiwa Bashungwa alimuagiza Mkuu wa Wilaya Ubungo, Kheri James kuweka utaratibu wa kukutana mara kwa mara na Wadau wa Kituo cha Magufuli, Mawakala na Makalani ili kusikiza na kuweka utaratibu wa kutatua changamoto ambazo zimekuwa zikijitokeza katika kituo hicho na kuzifanyia kazi kwa ushirikiano.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news