NA OR-TAMISEMI
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Mhe. Innocent Bashungwa amewaagiza wakurugenzi wa hamashauri zote nchini kutumia vyombo vya habari vilivyopo katika maeneo yao kutoa taarifa na kuhabarisha wananchi kuhusu miradi ya maendeleo inayotekelezwa na kueleza hatua na mipango mbalimbali ya Serikali inayopanga kufanya katika maeneo yao.
Bashungwa ametoa kauli hiyo leo Juni 13, 2022 wakati akizungumza na wakuu wa idara na vitengo wa Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe (CMT) na kumtaka Mkurugezi wa halmashauri kushirikiana na wakuu wa idara kutumia redio za kijamii kuhabarisha wananchi kuhusu miradi na hatua mbalimbali za utekelezaji mipango.
Amesema, Serikali imepeleka fedha nyingi kwenye halmashauri zote na imeweka mipango mbalimbali ya kuleta maendeleo, lakini wananchi walio katika maeneo yao hawapewi taarifa wala kujulishwa hatua mbalimbli za utekelezaji wa mipango.
Aidha, Bashungwa ameagiza utoaji wa elimu na kuhamisisha utumiaji wa fursa mbalimbali zilizopo katika maeneo yao kama kulima mazao ya kimkakati vilevile utunzaji wa mazinngira katika maeneo yanayowazunguka.
Wakati huo huo, Waziri Bashungwa ameagiza watendaji wa kata na vijiji kutumia lugha nzuri na za staha wakati wa kuwahudumia wananchi katika maeneo yao na kuondokana na hali ya kutumia nguvu na vitisho kwa wananchi.