Waziri Bashungwa awauma sikio watumishi, asisitiza maadili

NA ASILA TWAHA, OR-TAMISEMI

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Mhe. Innocent Bashungwa amewataka watumishi wa ofisi yake kufanya kazi zao kwa kuendelea kusimamia maadili ya usiri katika kutekeleza majukumu yao kwani wizara hiyo inabeba taswira nzima ya nchi.
Waziri Bashungwa amesema hayo Juni 21, 2022 kwenye kikao kazi na watumishi wa Ofisi ya Rais-TAMISEMI ikiwa ni Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma ambapo kila mwaka huadhimishwa kuanzia tarehe 16 hadi 23, Juni.

Amesema, utunzaji wa siri za Serikali kwa watumishi wa TAMISEMI ni lazima na sio hiari kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za utumishi wa umma lakini pia kujua TAMISEMI imebeba maisha ya watanzania, hivyo kuwataka kuzingatia suala la usiri katika utendaji na utekelezaji wa utoaji wa haki kwa watumishi na wananchi.

Waziri Bashungwa ameendelea kuwataka watumishi hao pia kutojiingiza katika masuala ya rushwa aidha, kwa kupokea kwa ajili ya kutoa huduma ama kwa namna nyingine amesema, suala hilio halikubaliki katika wizara hiyo kwani imepewa jukumu la utoaji wa huduma kwa wananchi na si vinginevyo. 

“TAMISEMI tuna jukumu kubwa la kutoa huduma kwa wananchi niwatake watumishi suala la utoaji wa huduma ni ibada, tusimamie katika utendaji wa haki pasina kujihusisha na rushwa. Wizara hii ni kubwa ujue ukiwa humu unatakiwa ufuate maadili ya utumishi wa umma na imani tuwe nayo sababu sisi tunatoa huduma moja kwa moja kwa wananchi wetu,”amesema Waziri Bashungwa.

Amesema,kuna vitendo vinatokea ambavyo si maadili ya utumishi wa umma kwa baadhi ya watu kuharibu taswira na picha ya ofisi hiyo kwa kushiriki kwenye vitendo ikiwemo kugushi barua za uhamisho wa watumishi.

"Nikuelekeze Katibu Mkuu Prof. Riziki Shemdoe kutokana na vitendo hivyo vinavyotokea kwa sasa mtu pekee anayeweza kusani barua hizo ni wewe mwenyewe.

“Ninaelekeza wale wote ambao walipata barua za uhamisho ambazo tumeshafanya uchunguzi na sio halali warudishwe kwenye vituo vyao vya awali na kama kuna stahiki zozote walipatiwa ambapo ni fedha za Serikali zirudishwe na wachukuliwe hatua,”amesisitiza Waziri Bashungwa.
Kwa upande wake Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhe. David Silinde amewashukuru watumishi hao kwa kuendelea kutoa ushirikiano kwa viongozi hao kuweza kutekeleza majukumu yao ikiwa wao ni moja kwa moja wanawajibika kwa wananchi,amewataka kuendelea kuwahudumia wananchi kwani wana imani na wizara hiyo. 

“Imani ya wananchi ni pamoja na kuwa na imani ya Rais wetu Mhe. Samia Suluhu Hassan na sisi TAMISEMI tunawajibika moja kwa moja kwa wananchi nitoe rai watumishi tufanyeni kazi sisi tumeaminiwa hivyo tuaminike,”amesema Mhe. Silinde.
Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Prof. Riziki Shemdoe amemuhakikishia Mhe.Waziri kuwa, maelekezo yote aliyoyatoa anaenda kuyasimamia ili kuendelea kuboresha utoaji wa huduma, amesema wao kama watendaji watahakikisha wanashirikiana na viongozi wa ngazi zote za wizara hiyo ili kuendelea kuwahudumia wananchi.

“Mhe.Waziri tutatekeleza yale yote ulitoyaelekeza ikiwemo uwajibikaji wa watumishi na uendane na upatikanaji wa haki zao, lakini pia tutaendelea kusimamia suala la maadili ya kazi katika wizara hii,” amesema Prof. Shemdoe.

Naye Afisa Utumishi Mkuu, Bi. Namsifu Maduhu akishukuru kwa niaba ya watumishi amesema maelekezo yote ya viongozi wameyapokea na wapo tayari kwenda kuyatekeleza kwa vitendo ikiwa jukumu lao ni kutoa huduma kwa wananchi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news