NA GODFREY NNKO
WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt.Angeline Mabula amesema kuwa, Serikali kuanzia sasa haitakuwa tayari kukubali wananchi kuthaminiwa ardhi yao kwa ajili ya kuhama kama anayehitaji hatakuwa na fedha mkononi.
Ameyasema hayo Juni 4, 2022 katika kikao kazi na wahariri mbalimbali wa vyombo vya habari kilichofanyika katika Ukumbi wa Millenium Tower, Kijitonyama jijini Dar es Salaam.
Dkt.Mabula amesema, wanafanya hivyo kwa kuwa hilo limekuwa moja ya sababu za kuongezeka kwa kesi za migogoro ardhi licha ya sheria kueleza muda wa kuwalipa watu tangu uthamini ulipofanyika kuwa ni miaka miwili.
"Hili la uthamini nalo ni eneo jingine lenye kuchangia migogoro ya ardhi, niwaeleze tu leo ambao mnahitaji ardhi ya wananchi kwa ajili ya kufanyia shughuli zozote mhakikishe mnakuwa na hela mkononi ndio tuingie kwenye uthamini.
"Sheria ya Ardhi ya mwaka 2017 imeeleza wazi kwamba, anayefanyiwa uthamini anatakiwa kulipwa ndani ya miaka miwili tangu amefanyiwa uthamani,lakini badhi ya watu hawafanyi hivyo,"amesema.
Pia amesema, wanaotakiwa kulipwa ndani ya miaka miwili ni wale waliochukuliwa maeneo yao kuanzia mwaka wa 2017 ambapo sheria hiyo ilianza kutumika rasmi baada ya kufanyiwa marekebisho mwaka 2016.
"Awali kabla ya kufanyiwa marekebisho Sheria ya Ardhi ilitaka mthaminiwa kulipwa ndani ya miaka 10, lakini baadaye ilifanyiwa marekebisho na kuanza kutumika rasmi Januari 2017,"amesema Dkt.Mabula.
Katika hatua nyingine, Dkt.Mabula amevitaka vyombo vya habari kusaidia kuibua na kuripoti habari zinazohusu changamoto kwenye Sekta Ardhi kwa lengo la kuisaidia Serikali kuharakisha kuzipatia ufumbuzi.
Mheshimiwa Waziri Dkt.Mabula amesema, katika sekta ya ardhi kuna migogoro na changamoto mbalimbali hivyo ni wajibu kwa vyombo vya habari kuibua kero hizo ili kutoa fursa kwa serikali kuweza kuzipatia ufumbuzi.
Amesema, kama inavyoelezwa kuwa vyombo habari ni mhimili wa nne usio rasmi na wahariri pamoja na waandishi wa habari kupitia vyombo vyao watumie hiyo nafasi kutoa elimu na kuibua changamoto hizo.
“Hivyo nichukuwe fursa hii kuwaomba ndugu zangu wahariri pamoja na waandishi wa habari kutumia fursa ya kikao hiki kwenda kuripoti habari nyingi zinazohusu changamoto zilizopo kwenye sekta ya ardhi.
"Ni imategemeo yangu kuona baada ya kikao hiki nitaona na kusoma habari nyingi zinazohusu sekta ya ardhi ili kutoa nafasi ya kuzishughulikia sisi kama Serikali na maofisa wangu wamejipanga kwa ajili ya kutatua changamoto hizo,"amesema Dkt.Mabula.
Mbali na hayo amesema, wizara yake imejipanga kikamilifu kupitia maofisa wake kwenda kuazisha kliniki za kutatua kero zilizopo kwenye sekta ya ardhi hapa nchini ambapo kliniki hiyo itakwenda maeneo husika ili kutatua migogoro ya ardhi ambayo wanakabiliana nayo wananchi.
Dkt.Mabula akizungumzia madeni amesema kuwa, wizara hiyo inadai shilingili bilioni 78 kwa mashirika na umma na binafsi.
"Fedha hizo ni nyingi sana na hizo zote ni changamoto ambazo vyombo vya habari zina mchango mkubwa wa kuzungumzia kwa maslahi mapana kwa maendeleo ya taifa letu,"amesema Dkt.Mabula.
Heshima
"Katika wadhifa wangu kwa nafasi za uwaziri, natambua na kuheshimu sana nafasi na umuhimu wa vyombo vya habari. Nafahamu kwamba vyombo vya habari vina umuhimu mkubwa katika kuijenga na
kuimarisha sekta ya ardhi.
"Mafanikio katika sekta ya ardhi yanategemea sana kuwapo kwa taarifa sahihi kwa wananchi katika wakati mwafaka, zinazofuata misingi ya utawala wa sheria na uhuru wa vyombo vya habari.Ni dhahiri kuwa ustawi wa sekta ya ardhi, pamoja na mambo mengine kwa kiasi kikubwa unategemea kuwapo kwa vyombo vya habari kwa kufikishia wananchi taarifa sahihi na kufikisha taarifa za wananchi serikalini.
"Kwa muktadha huo, ni wazi wananchi wanategemea sana upatikanaji wa Habari sahihi kupitia vyombo vya Habari,"amefafanua Waziri Dkt.Mabula.