NA MWANDISHI WETU
WAZIRI wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mohammed Mchengerwa amesema watazitumia tuzo za BET za mwaka 2022 kuona maeneo ya kuboresha zaidi katika usimamizi wa sekta ya sanaa nchini Tanzania.
Waziri Mchengerwa ameyasema hayo baada ya kushuhudia Tuzo za BET za mwaka huu 2022 mjini Los Angeles, California, usiku wa kuamkia leo.
“Tumeshuhudia tuzo hizi ikiwa pia ni maandalizi ya sisi kuandaa tuzo kubwa kwa upande wa Afrika za MTV, ambapo sehemu ya waandaaji wake ni hawa hawa wa tuzo za BET na kuna maeneo ya kisera na kimageuzi tu tutaendelea nayo baada ya hapo,” alisema Waziri Mchengerwa.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara hiyo aliyeambatana na Mhe Waziri katika tuzo hizo, Dkt. Hassan Abbasi amesema tuzo za BET pia zitaisaidia Tanzania kuboresha tuzo zake za ndani na usimamizi wake kwani nazo zinaweza kuwa kubwa kama za BET.