NA GODFREY NNKO
SERIKALI ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imeibua shangwe kwa wazazi na walezi baada ya Waziri wa Fedha na Mipango, Mheshimiwa Dkt.Mwigulu Nchemba kupendekeza kufutwa ada kwa wanafunzi wa Kidato cha Tano na Sita ili kuwapunguzia gharama za masomo nchini.
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) akimuonesha Mkoba wa Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka 2022/23 Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa, Bungeni, jijini Dodoma.
"Napendekeza kufuta ada kwa wanafunzi wa kidato cha tano na sita. Kwa hatua hiyo, elimu bila ada ni kuanzia shule za msingi mpaka kidato cha sita,”amesema Mheshimiwa Waziri Dkt.Nchemba.
Mheshimiwa Waziri ameyasema hayo leo Juni 14, 2022 bungeni jijini Dodoma wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya Bajeti Kuu ya Serikali ya mwaka 2022/2023.
Amesema, kwa sasa wanafunzi wa Kidato cha Tano ni 90,825 na kidato cha Sita ni 56,880 na mahitaji ya fedha ni shilingi Bilioni 103.
Pia Mheshimiwa Waziri amesema,Serikali itajipanga kuangalia namna ya kusaidia vyuo vya kati kadiri hali ya uchumi itakavyotengemaa. Ili kuwapunguzia gharama watoto hao kama Rais alivyoielekeza wizara.
Mikopo magari
Aidha, Mheshimiwa Waziri amependekeza Serikali kubadili utaratibu uliopo ili kuwakopesha magari watumishi wa umma wenye hadhi ya kuwa na gari la Serikali ikiwa ni mkakati wa kubana na kuondoa matumizi yasiyo ya lazima.
Amesema kuwa utaratibu huo alioupendekeza utasaitda kuokoa gharama za matumizi ya magari kwa zaidi ya shilingi Bilioni 500 za Serikali.
“Kwa upande wa hatua za muda wa kati na muda mrefu, napendekeza Serikali kubadili kabisa utaratibu uliopo kwa kuwakopesha magari watumishi wenye hadhi ya kuwa na gari la Serikali wawe na magari yao wenyewe, wafanye matengenezo wenyewe.
"Wanunue vipuri wenyewe na masuala ya mafuta yaangaliwe kwa utaratibu utakaoonekana unafaa.Kwa sasa Serikali ina magari zaidi ya 15,742, pikipiki 14,047 na mitambo 373 na inatumia zaidi ya shilingi Bilioni 558 kwa mwaka.
"Gharama kwa ajili ya ununuzi wa magari, ununuzi wa mafuta ya uendeshaji, ununuzi wa vipuri na matengenezo ambapo kwa sasa ni zaidi ya shilingi bilioni 500,ukiondoa vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na Mahakama, upande wa Serikali.
"Wabaki viongozi wakuu wa wizara, mashirika, wakala, mikoa, wilaya na miradi ambao wasimamizi watakuwa eneo la mradi muda mwingi,kwenye makundi haya hawatazidi watano kwa taasisi.
"Wengine wote wenye stahili ya gari la Serikali wakopeshwe, watumie magari yao, watasimamia vizuri matumizi, matengenezo, mafuta na vipuri,”amefafanua Mheshimiwa Waziri.
Aidha,amesema kuwa hali hiyo pia itaondoa utaratibu uliopo sasa ambapo dereva anasafiri na gari huku kiongozi wake akisafiri kwa ndege.
“Tutaondoa utaratibu uliozoeleka, dereva na gari anapitishwa chini, bosi anapanda ndege mpaka Mwanza au Mbeya kutoka Dar es Salaam na kurudi hivyo hivyo.
Kwa nini?
"Kuna utafiti wa siri ulifanywa, kwa siku moja yalibainika magari ya Serikali yaliyotoka Dodoma kwenda Dar es Salaam yalikuwa 132, na yaliyokuwa yanatoka Dar es Salaam yakipishana kuja Dodoma yalikuwa 76, na mengine nane yalikuwa yamepinduka. Je? Kwa mwezi ni gharama kiasi gani,"amesema.
Mheshimiwa Waziri amesema kuwa, utaratibu huo alioupendekeza utasaidia Serikali kuokoa gharama za matumizi ya magari kwa ajili ya kutekeleza shughuli zingine za maendeleo.
“Utaratibu huo gharama za matumizi ya magari serikalini zitakuwa takribani shilingi 50,508,038,843.09. Zaidi ya shilingi billion 500 zitaokolewa na kuelekezwa kwenye ununuzi wa dawa muhimu hospitalini, kutoa mikopo kwa wanafunzi wanaosoma vyuo vya kati, na kutekeleza miradi ya maendeleo. Tumezidi kupenda ubosi, magari 17 makubwa kwa kila mtu serikalini, matumizi ya starehe, wakati katika nchi yetu bado kuna watu wanapata shida kupata mlo mmoja.
"Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Mungano wa Tanzania
ameielekeza Wizara ya Fedha na Mipango ifanyie kazi jambo hili la kuelekeza fedha kwenye matumizi ya msingi tu,"amefafanua Mheshimiwa Waziri.
Mifumo ya malipo
Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Waziri Dkt.Nchemba amesema, Serikali inatarajia kufanya marekebisho kwenye sheria ya mifumo ya malipo ya Taifa kwa kupunguza tozo ya miamala wa huduma za fedha katika simu za mkononi.
“Napendekeza kupunguza tozo ya muamala kutoka kiwango kisichozidi shilingi 7, 000 hadi kiwango kisichozidi shilingi 4,000 katika kila muamala wa kutuma au kutoa pesa.
“Punguzo hili ni sawa na asilimia 43 ya kiwango cha sasa. Sambamba na hilo, napendekeza kuongeza wigo wa tozo hiyo ili kuhusisha miamala yote ya kielektroniki,"amesema Mheshimiwa Waziri.
Amefafanua kuwa,lengo la hatua hiyo ni kupunguza makali ya maisha kwa Mtanzania hasa katika kipindi hiki cha changamoto kubwa ya kiuchumi na kuweka usawa katika utozaji wa tozo hiyo nchini.
Forodha
Kwa upande mwingine,amesema nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) zimekubaliana kuongeza Ushuru wa Forodha kutoka asilimia 25 hadi asilimia 35 kwenye nywele bandia zinazotambulika kwa Heading 6704.
“Nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki zimekubaliana kuongeza Ushuru wa Forodha kutoka asilimia 25 hadi asilimia 35 kwenye nywele bandia zinazotambulika kwa Heading 6704,"amesema Mheshimiwa Waziri.
Amebainisha kuwa, hatua hiyo inalenga kulinda wazalishaji wa ndani wa bidhaa hizo ili kuongeza ajira pamoja na kuongeza mapato ya Serikali.
"Pamoja na hayo yamefanywa mabadiliko mbalimbali ya sheria kwa kufutwa kifungu cha 5 (1) (l) cha Sheria ya Chakula, Dawa na Vipodozi na. 1 ya mwaka 2003 ili jukumu la viwango vya Kitaifa libaki kwenye sheria ya viwango na. 2 ya mwaka 2009, mahitaji ya viwango ya TMDA yatawasilishwa Shirika la Viwango Tanzania,"amesema.
Ujenzi
Pia amesema, Serikali imekamilisha ujenzi wa madarasa 15,000 katika shule za sekondari na vituo shikizi na mabweni 50 kwa ajili ya wanafunzi wenye mahitaji maalumu.
“Ujenzi wa miundombinu hii umewezesha wanafunzi wote 907,803 waliofaulu mtihani wa darasa la saba mwaka 2021 kupata nafasi ya kuanza kidato cha kwanza Januari 2022 bila kusubiri chaguo la pili,"ameeleza Mheshimiwa Waziri Dkt.Nchemba.
Aidha, amesema Serikali imekamilisha maboma 560 ya vyumba vya madarasa katika shule za sekondari kutokana na tozo za miamala ya simu ambapo shilingi bilioni saba zilitolewa.
Mikopo Elimu
Waziri amesema kuwa, pia Serikali imetoa mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 569 kwa wanafunzi 177,777 wa elimu ya juu.
Dkt.Nchemba amefafanua kuwa, katika mwaka 2022/23 Serikali itaenda kutekeleza mradi wa Higher Education for Economic Transformation (HEET) wenye thamani ya dola za Marekani milioni 425.
Amesema, mradi huo utahusisha ujenzi wa miundombinu katika vyuo vikuu mama na katika mikoa kadhaa ambayo haina vyuo vikuu.
Amesema, miongoni mwa mikoa hiyo niLindi, Kagera, Rukwa, Katavi, Manyara na kukamilisha ujenzi wa Institute of Marine Science Zanzibar na kujenga chuo kipya cha Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) jijini Dodoma.
Afya
Katika hatua nyingine amesema, Serikali inaendelea kuimarisha huduma za afya kwa kuboresha huduma za uchunguzi wa magonjwa ambapo hadi sasa katika hospitali mbalimbali nchini kuna jumla ya mashine 11 za CT Scan, mashine saba za MRI na mashine 105 za digital X Ray zinazofanya kazi.
Amesema, kati ya hizo mashine 42 za digital X Ray zipo katika hospitali za ngazi ya taifa, kanda na rufaa za mikoa na mashine 63 zipo katika hospitali zilizo chini ya Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI).
Mheshimiwa Waziri amesema kuwa, Serikali itaendelea kutoa kipaumbele katika eneo hilo ambapo ununuzi zaidi wa vifaa vya uchunguzi wa magonjwa umekamilika na vifaa hivyo vitasimikwa katika hospitali na taasisi mbalimbali nchini.
Amesema, vifaa ambavyo vimeshaagizwa ni pamoja na, MRI 4, CT-Scan 31; Digital X Rays 130, Mini Angio Suite moja na Echo Cardiography saba.
Pia amesema, Serikali inaendelea na usimikaji wa vinu ya kuzalisha na kujaza hewa tiba ya oksijeni ambapo hadi sasa vinu 13 vimesimikwa katika hospitali zetu mbalimbali na hivyo kusogeza huduma za kitabibu kwa wananchi.
Sanaa
Wakati huo huo, Serikali sasa imeitambua rasmi sekta ya sanaa na burudani kuwa ndiyo iliyoongoza kwa ukuaji wa asilimia 19 kwa mwaka ikifuatiwa kwa mbali na sekta za umeme kwa asilimia 10 huku madini ikifuata kwa asilimia tisa.
Mheshimiwa Waziri amesema, kwa sasa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ameagiza kuanzishwa kodi maalum (blanktape levy/private remuneration levy) ya asilimia 1.5 katika baadhi ya vifaa vitakavyoingia nchini vinavyoweza kutumika kudurufu kazi za sanaa (sehemu ya mapato ya fedha hiyo itaenda kwenye mirabaha na shughuli nyingine za kuendeleza sanaa nchini).
Pia amesema, Serikali imebadilisha sheria kuruhusu watu binafsi au taasisi (collective management offices, CMOs), kuanzishwa na kusaidia kukusanya mirabaha ya wasanii na hesabu zao kukaguliwa na COSOTA huku lengo ni kuwaongezea wasanii wigo wa kunufaika na kazi zao.
Kodi ya Zuio
Amesema,Serikali imeshusha kodi ya zuio katika biashara ya filamu kutoka asilimia 15 hadi 10 ili kuyapa unafuu makampuni yanayohusika na masuala ya filamu nchini na imetenga asilimia mbili ya fedha zitakazotengwa kwa ajili ya CSR katika makampuni kupelekwa katika maendeleo ya michezo nchini.
Bahati Nasibu
Wakati huo huo amesema, Serikali inarejesha Bahati Nasibu ya Taifa na itakarabati viwanja vitano na kuviwekea nyasi za kisasa miongoni mwa mambo mengine ya kuendeleza michezo.
Pia amesema, Mheshimiwa Rais ameelekeza msamaha wa mwaka jana wa kusamehewa kodi ya asilimia 18 kwa nyasi bandia sasa mwaka huu ujao wa fedha msamaha huo uliokuwa unahusu viwanja vya majiji na manispaa tu ushuke hadi chini kabisa katika viwanja vya ngazi ya halmashauri.
Amesema,engo ni kusaidia uwekezaji wa miundombinu ya michezo kwa ngazi zote nchini huku ikielekezwa kumbi mbalimbali nchini kuwa na vifaa vya ukalimani wa lugha ya Kiswahili ili hata pale inapolazimika kutumika lugha yoyote ya kigeni huduma za ukalimani kwenda na kutoka Kiswahili ziwepo.
Lengo la kufanya hivyo, ni kuwezesha kuikuza lugha ya Kiswahili lakini pia kutoa ajira kwa wakalimani na wafasiri na saili za kazi zifanyike kwa kutumia Kiswahili.
TIN
Wakati huo huo, Mheshimiwa Waziri amesema Serikali inakusudia kutoa Namba ya Utambulisho wa Mlipakodi (TIN) kwa kila Mtanzania mwenye umri wa kuanzia miaka 18 kuanza kulipa kodi.Amesema, ili kufikia azma hiyo wataanza kutoa TIN kwa kila mtanzania kuanzia umri wa kuanzia miaka 18 kwa utaratibu wa usajili wa Namba ya Utambulisho wa Taifa (NIDA) unaomtaka kila mwananchi mwenye umri huo wa au zaidi kujisajili.
“Napendekeza kuwa wale wote wenye NIDA kwa sasa wapatiwe namba ya TIN na itumike kwenye miamala yote inayofanyika katika ununuzi na mauzo yanayofanyika ndani ya nchi,”amesema Mheshimiwa Waziri.
Ving'amuzi
Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Waziri amesema, amesema Serikali ina mpango wa kuanzisha utaratibu wa kutoza ada ya shilingi 1,000 hadi shilingi 3,000 kwenye ada ya matumizi ya king’amuzi kulingana na kiwango cha matumizi nchini.Pia amependekeza kuanzishwa tozo ya asilimia 1.5 kwenye vifaa vinavyotumika kuzalisha, kusambaza, kudurufu na kutunza kazi za sanaa, uandishi na ubunifu mwingine kama vile muziki, filamu, vitabu, picha na aina nyingine za kazi za ubunifu.
“Vifaa hivi ni Radio/ TV set enabling recording; Analogue audio recorders; Analogue video recorders; CD/DVD Copier; Digital Jukebox na MP 3 Player. Hatua hii inatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha Sh9.6 bilioni,"amesema.
Waziri Dkt.Nchemba amesema, Shirika la Viwango Tanzania (TBS) lina mpango wa kupunguza tozo ya kuthibitisha ubora wa shehena za sukari zinazoingizwa nchini kutoka shilingi sita kwa kilo hadi 2.5.
Mheshimiwa Waziri amesema, lengo la hatua hiyo ni kupunguza gharama kwa waingizwaji wa bidhaa hiyo na kutoa unafuu kwa Watanzania.
Vibali
Aidha, Mheshimiwa Waziri amesema anpendekeza kuondoa tozo ya vibali vya ukaazi kwa wanafunzi wa elimu ya juu kutoka nchini Msumbiji.
Amesema, lengo la hatua hiyo ni kutekeleza matakwa ya makubaliano kati ya nchi hiyo na Tanzania kuondoleana tozo hizo ambapo Msumbiji imeshaanza kutekeleza makubaliano hayo.
“Mwaka wa fedha 2021/22 Serikali ilipitisha uamuzi wa kuondoa ada ya kibali cha kuingia nchini kwa wanafunzi wa elimu ya juu kutoka nchi ya Msumbiji kwa ajili ya Mpango wa kubadilishana wanafunzi wa elimu ya juu baina ya Tanzania na Msumbiji,”amebainisha Mheshimiwa Waziri.
Ufundi
Mheshimiwa Waziri amesema Serikali itaendelea kuimarisha elimu ya ufundi hususani katika vyuo vya kati kwa lengo la kuwajengea uwezo wa kujiajiri ama kuajiriwa.
“Mpaka sasa wilaya 77 zina vyuo vya Ufundi VETA kati ya wilaya 138 nchini kote. Tuna mikoa 25 ina Vyuo vya Ufundi kati ya mikoa 26.
"Bado Mkoa wa Songwe hauna kabisa Chuo cha VETA na wabunge wa mkoa wa Songwe wamekuwa wakishinda Ofisini wakifuatilia ahadi waliopewa na Mheshimiwa Rais.
“Bado kuna wilaya 36 ambazo hazina vyuo wala vyuo vya Mkoa. Napendekeza kutoa bilioni 100 kwa ajili ya ujezi wa vyuo vya ufundi kwa Mkoa wa Songwe na wilaya 36 ambazo hazina vyuo ili kufanya wilaya zote 138 kuwa na chuo cha Ufundi (VETA). Waheshimiwa wabunge, Huyo ndio Samia,”amesema Waziri Dkt. Nchemba.