Wizara ya Ardhi yataja sababu kuu za Sensa ya Majengo (Makazi) 2022

NA GODFREY NNKO

WIZARA ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imesema kuwa, Sensa ya Watu na Makazi Agosti 23, 2022 nchini imebeba uzito wa kipekee ikizingatiwa kwamba, kwa mara ya kwanza tangu tupate Uhuru tunakwenda kufanya sensa ya makazi (majengo) nchini.
Deogratius Kalimenze ambaye ni Mkurugenzi wa Maendeleo ya Makazi kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ameyasema hayo Juni 4, 2022 wakati wa kikao kazi kati ya Waziri Dkt.Angeline Mabula na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari nchini kupitia Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF).

Kupitia kikao kazi hicho ambacho kilifanyikia katika Ukumbi wa Millenium Tower, Kijitonyama jijini Dar es Salaam, Bw.Kalimenze alikuwa akiwasilisha mada ya Sensa ya Majengo na Urasimishaji wa Makazi.

"Lengo la sensa hii ni kutaka kufahamu gharama za ujenzi zinazotumika kuendelea majenzi nchini na mchango wa Serikali na sekta binafsi katika uwepo wa nyumba za makazi na matumizi mengineyo.

"Na jambo la pili msingi wake unajikita kwenye Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambayo sisi sote tunaitekekeza ibara ya 76 ( d) ambayo kimsingi inaitaka wizara kutambua na kuandaa kanzi data ya nyumba zote nchini kwa kushirikiana na wadau na kuweza kuimarisha uhusiano kati ya wapangaji na wamiliki wa majengo nchini.

"Kwa hiyo, huo ndio msingi ambao umesukuma Serikali kuweza kufanya kwa mara ya kwanza tangu tupate uhuru Sensa ya Majengo nchini.Yako mambo mbalimbali ambayo ni faida zitakazotokana na faida ya sensa.

Faida

"Kwanza kabisa kupata takwimu ambazo zitasaidia sisi kuwa na kanzi data ya majengo yetu nchini na aina mbalimbali za matumizi ya hayo majengo, pili kuiwezesha Serikali kufanya mapitio na maboresho ya sheria, kanuni, sera na programu mbalimbali ambazo zinasimamia sekta ya uendelezaji wa nyumba na makazi nchini.

"Tatu, kuiwezesha Serikali kupata taarifa za matumizi ya majengo mbalimbali nchini kama ni mangapi yanatumika kwa makazi, biashara, huduma mbalimbali za jamii ikiwemo shule, vituo vya afya, hospitali, vituo vya polisi na kadhalika.

"Jambo la nne ni kuiwezesha Serikali kujua mchango wake katika upatikanaji wa nyumba za makazi nchini kama inavyoelekezwa na Sera ya Maendeleo ya Makazi.

"Na hapa tunafahamu kwamba ujenzi wa nyumba au majengo nchini unafanywa na taasisi za Serikali, Serikali yenyewe pamoja na watu binafsi, lakini hatuwezi kusema kwa uhakika mchango wa Serikali katika ujenzi wa nyumba ni kiasi gani, lakini kutokana na mchango wa sensa tutaweza kutambua na kujua mchango wa Serikali katika majenzi ni kiasi gani,"amesema Mkurugenzi huyo.

Amefafanua kuwa, jambo la tano, ni kuiwezesha Serikali kufanya tathmini ya kiwango cha nyumba zilizojengwa maeneo yaliyopangwa, maeneo ambayo hayajapangwa na uwiano wa upatikanaji wa huduma za jamii katika majengo hayo.

"Na hapa kwa kipindi kirefu tumekuwa tunasema kwamba Tanzania zaidi ya asilimia 70 ya wakazi wake wanaishi katika maeneo yasiyopangwa, lakini kuna programu ya urasimishaji imefanyika karibu nchi nzima na kuna faida nyingi zimejitokeza kwa hiyo katika zoezi hili tutakwenda sasa kutambua ni kiwango gani makazi yetu yapo yaliyopangwa na ambayo hayajapangwa mpaka sasa," amesema.

Bw.Kalimenze anataja jambo la sita kuwa ni kuiwezeaha Serikali kutambua hali ya uendelezaji wa miji katika ujenzi uliopo kama maghorofa, majengo ya kawaida na mambo mengine, na kujua sifa za hayo majengo yanayozungumziwa ni ya aina gani.

"Ambapo katika utekelezaji wa sensa ya majengo tunakwenda kupata viashiria mbalimbali vya utekelezaji wa malengo endelevu ambayo lengo namba 11 linataka tuwe na miji ambayo ni jumuishi,salama na stahimilivu na endelevu katika nchi zote ulimwenguni na katika kutekeleza sensa hii kuna viashiria vingi ambavyo tunaweza kupata majibu yake na kujipima utekelezaji wa malengo haya endelevu,"amesema.

Aidha, jambo la nane, Bw.Kalimenze amesema ni kusaidia tafiti mbalimbali ambazo zinafanyika nchini katika masuala ya nyumba na uendelezaji wa miji.

Hatua

"Mheshimiwa Waziri napenda kutoa taarifa ya maandalizi ya sensa ya mwaka huu ambayo itaanza tarehe 23 Agosti mwaka huu kuwa,hatua ya kwanza kabisa ilikuwa ni uandaaji wa nyenzo kwa maaana ya madodoso na miongozo mbalimbali ya usimamizi ya makarani na wakufunzi kwa ajili ya kuendesha zoezi la Sensa ya Majengo na hili lilifanyika kuanzia Julai, mwaka jana na limeendelea mpaka mwezi huu ndipo tumekamikisha kuboresha nyenzo hizo baada ya kuwa tumefaya sensa ya majaribio na pre-test tena nyingine mwezi uliopita mwishoni,"amesema.

Anasema, hatua ya pili ilikuwa ni mafunzo kwa makarani ambao waliwatumia katika zoezi la sensa ya majaribio ambayo inatakiwa kwa mujibu wa sheria ya takwimu ifanyike mwaka mmoja kabla ya sensa haijafanyika na zoezi hilo lilifanyika.

"Hatua ya tatu, ni uandaaji wa mikakati ya uelimishaji na mkakati huu ulizinduliwa na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kule Dodoma mwaka jana na sisi wote kama wanahabari tunao wajibu wa kutumia mwongozo huu katika uhamasishaji na uelimishaji wa jamii kuhusiana na maandalizi ya sensa na sensa yenyewe,"amesema.

"Lakini sensa ya majaribio ilifanyika mwaka jana mwezi Septemba tarehe 8 hadi 19 na matokeo yake yakachambuliwa na kupata tathmini ya nyenzo zilizotumika na ubora wa nyenzo ili kupata takwimu sahihi kwa ajili ya sensa kuu ambayo itafanyika mwezi wa nane mwaka huu.

"Kazi zilizofanyika baada ya sensa ya majaribio na kuandaa rasimu sasa ni kuboresha miongozo na kuandaa majedwali ambayo yatatumika kutoa taarifa au uchambuzi wa takwimu zinazotokana na sensa ya majengo.

Usimamizi

"Usimamizi wa sensa ya majengo na sensa nyingine mbili ambazo nimezitaja ukoje? Kwanza tunayo Kamati Kuu ya Kitaifa ya Sensa ya Watu na Makazi ambayo Mwenyekiti wake ni Waziri Mkuu Kassim Majaliwa huku Mwenyekiti mwenza wa Kamati Kuu ya Kitaifa ya Sensa ya Watu na Makazi akiwa ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Hemed Suleman Abdulla

"Pia tunayo Kamati ya Ushauri ya Kitaifa ambayo inaongozwa na Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu ambaye ndiye Mwenyekiti wa kamati hiyo," amesema.

"Tunazo ofisi zetu za Takwimu ya Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar, nne tunazo kamati za sensa za kila mkoa ambazo zinaongozwa na waheshimiwa wakuu wa mikoa, hao ndio wasimamizi wakubwa wa zoezi hilo na pia tunazo kamati za sensa za wilaya na mwisho kabisa tunazo kamati za kata, mitaa,vitongoji na shehia kwa upande wa Zanzibar,"amesema Deogratius Kalimenze ambaye ni Mkurugenzi wa Maendeleo ya Makazi.
Ameongeza kuwa, "pia tuna makamisaa wawili wa sensa Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar, lakini hapo katikati kuna sekretarieti ya Kitaifa ambayo inaongozwa na zile Kamati Kuu mbili ya Mawaziri na makatibu wakuu, lakini tuna kamati ya taifa ya uhamasishaji Kitengo cha Uhamasishaji na Uelimishaji na Kamati ya Wabunge,"amesema.

Dodoso

Deogratius Kalimenze ambaye ni Mkurugenzi wa Maendeleo ya Makazi anasema kuwa, "Dodoso lina maswali 23 kwa ufupi nitazungumzia tu aina za majengo, jinsi ya umiliki, sifa za majengo, urefu wa majengo, aina za uniti, idadi za uniti zilizopo kama jengo linakaliwa na wakazi zaidi ya mmoja au ghorofa, hali ya ujenzi, kama majengo yaliyokamilika ni mangapi, yanayoendelea na ujenzi, yalivyo katika hatua za msingi na kadhalika,"amesema.

"Hali ya ukaazi ikoje, sababu ya majengo kutotumika, ubora wa majengo, hali ya ujenzi nani anamiliki jengo, aina ya umiliki aidha ni serikali au mtu binafsi, matumzi makuu ya jengo, nyaraka za kisheria wanazomiliki watu, vifaa vya ujenzi wanavyotumia watu, maeneo gani yamepimwa na maeneo gani hayajapimwa kama nilivyosema tunataka tupime, vifaa vya ujenzi vinavyotumika, huduma zinazopatikana, na gharama za ujenzi na vyanzo vya mapato." amesema.

Bw.Kalimenze anasema, hayo yote yataisaidia Serikali kufanya tathmini ya namna gani sekta ya uendelezaji sekta ya majenzi nchini inavyofanya kazi na baadhi ya viashiria vitatumika kupima hali ya umasikini usiokuwa wa kipato.

"Nitoe mfano wa maswali machache kwenu Wahariri mnapokuwa mnazungumzia jambo fulani ni vizuri mkawa na uelewa mpana mnamaanisha nini? Kwa mfano swali linalouliza jengo hili ni la aina gani? Sisi tunafahamu kuna aina kuu mbili za majengo, majengo ya kawaida na majengo ya ghorofa, lakini tumeongeza aina ya tatu aina nyingine ni hatua ya majengo ambayo yanajengwa hayajafikia utimikifu wake,"amesema.
"Haya tutayachukukulia ni aina nyingine ya kihatua kwamba jengo hili lipo katika hatua ya kwanza kabisa, labda kama ni msingi kwa hiyo ni vizuri sana tunapotoa taarifa na takwimu zinazotakiwa kuchukuliwa wananchi wafahamu, watoe taarifa gani katika hali fulani,"amesema.

"Lipo swali linauliza kwamba jengo hili lina sifa gani, tunapozungumzia sifa za majengo kuna aina kuu tatu nyumba iliyo peke yake iliyojengwa kuanzia msingi hadi paa bila kuungana na nyumba nyingine. Lakini tunazo nyumba mbili za aina moja ambazo zimeungana, ni nyumba mbili zilizokamilika, lakini zimeungana zinashare ukuta. Na tuna Nyumba tunasema safu za nyumba, nyumba zaidi ya tatu zimeungana, lakini zote zinaishi watu tofauti tofauti," amesema.
"Swali jingine muhimu ambalo ni vizuri mkalifahamu ni hali ya ujenzi wa jengo lililokamilika hapa tunataka kupata taarifa ya jengo lililokamilka, limeezekwa kuta zote na lina madirisha na milango na limesakafiwa haijalishi limepakwa rangi au halijapakwa rangi, lakini hatua zote hizo zimekamilika tunasema jengo limekamilika.

"Yapo majengo ambayo yamejengwa upande na watu wanaishi na upande mwingine ujenzi unaendelea. Kuna majengo ya muda, haya ni majemgo ambayo hayawezi kudumu kutokana na hali aidha uchakafu au kutokana na madhumuni yake, au vifaa vikivyotumika si vya kudumu, majengo haya tunayaona katika maeneo mbalimbali ambako ujenzi unaendelea na vijijini watu wengi tunayaita (full suit) hizi ni nyumba, lakini ni nyumba za muda . Ukienda kule kwa Wahandizabe utakuta nyumba zao katika hali hiyo.

"Swali jingine muhimu nini hali ya uhitaji wa ukarabati wa jengo, ambalo lipo katika hali nzuri hilo halihitaji ukarabati mdogo, unahitajika ni jengo linalohitaji ukarabati mdogo mfano rangi imeharibika, baadhi ya bati zina kutu, madirisha au milango inahitaji ukarabati mdogo au nyufa kidogo tunasema, lakini ukarabati mkubwa unahitajika ni majengo ambayo yanahitaji utengenezaji mkubwa sana mfano paa zima limeezuliwa, au nyufa kubwa ambayo inahatarisha usalama wa wakazi, milango imeondoka kabisa halifai kabisa kwa matumizi ni jengo ambalo haliko katika hali nzuri kabisa,"amesema.

Changamoto

Mkurugenzi wa Maendeleo ya Makazi anasema kuwa,changamoto waliyokutana nayo katika zoezi la sensa ya majaribio ni kukosa kwa taarifa hasa kwa majengo ambayo hayajakamilika kutokana na maeneo hayo kukosekana wakazi wanaoishi.
"Hivyo ndugu zangu wahariri na wanahabari tunawaomba mshiriki kikamilifu katika uhamasishaji wa wananchi ili wananchi hao wanaomiliki majengo ambayo hayajakamilika labda ni msingi, boma waache taarifa zao kwa wenyeviti wa mitaa wa maeneo husika ili karani atakapokwenda katika zoezi la kuhesabu majengo basi tayari viongozi wa mitaa wawe na taarifa za jengo husika.

"Pia mwezi huu tutakuwa na mafunzo kwa ajili ya wakufunzi kwa siku 21, sasa wakufunzi hawa watatawanywa kwenda kufundisha kuanzia mwezi wa saba, kufundisha makarani wote zaidi ya 200,000 ambao watatumika katika zoezi la Sensa ya Watu na Makazi,"amesema Deogratius Kalimenze ambaye ni Mkurugenzi wa Maendeleo ya Makazi

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news