NA PAMELA MOLLEL
ZAHANATI ya Kikatiti iliyopo Kata ya Kikatiti ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Meru mkoani Arusha ambayo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan alitoa shilingi milioni 10 mwezi Oktoba, mwaka jana kuchochea ujenzi wake inatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi huu.
Rais Samia wakati akiwa njiani kuelekea mkoani Arusha alisimama eneo la Kikatiti na kisha kusikiliza changamoto ya kukwama kwa ujenzi wa zahanati hiyo tangu mwaka 2013 ambapo alichangia fedha hizo na kuagiza mara moja ujenzi uendelee.
Akizungumza na waandishi wa habari, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Meru,Mwalimu Zainab Makwinya amesema kwamba, baada ya Rais Samia kutoa fedha hizo wao kama halmashauri kupitia mapato ya ndani walitoa shilingi 10 kusukuma ujenzi huo.
Mwalimu Zainab amesema kwamba kitendo cha Rais Samia kutoa fedha hizo kimewatia chachu ya kukamilisha ujenzi huo kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo.
"Bila Rais Samia hii kazi ingeendelea kubaki ilivyo kwa kuwa tusimgefanya lolote toka mwaka 2013 ilikuwa imekwama hakika tunamshukuru Mheshimiwa Rais,"amesema Mwalimu Zainab.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Meru,Mwalimu Zainab Makwinya akimuonesha mjumbe wa Kamati ya Siasa, Robert Kaseko,namna ujenzi unavyoendelea katika Zahanati ya Kikatiti iliyopo wilayani humo mkoani Arusha.
Alisisitiza kwamba, wamejitahidi kutafuta wadau wa maendeleo kupitia shirika la misaada la CTSI la nchini Korea na benki ya NMB ambapo kwa kiasi kikubwa wamewasaidia kukamilisha ujenzi huo.
Hata hivyo,alisema kuwa kwa kuwa eneo la zahanati hiyo wamelipima na ni kubwa hivyo wanaiomba serikali ibadilishe zahanati hiyo na kuwa kituo cha afya.
"Tumeongeza vyumba viwili chumba kimoja cha akinamama wajawazito kupumzikia wakati wakisubiri kujifungua na kingine cha kujifungulia, hivyo kazi tunatarajia kuikamilisha mwishoni mwa mwezi huu tungeomba hiki kiwe kituo cha afya na sio zahanati maana ni kubwa na ya kisasa,"ameongeza Mwalimu Zainab.
Katibu wa shirika la misaada la CTSI, Justine Mwaisemba akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani).
Naye Katibu wa shirika la misaada la CTSI ,Justine Mwaisemba amesema kuwa wao kama wadau wa maendeleo wameamua kumuunga mkono Rais Samia kwa kukamilisha hatua zote za ujenzi wa zahanati hiyo.
Mwaisemba amesema kuwa, mpaka sasa shirika lao limeshatumia jumla ya zaidi ya kiasi cha shilingi milioni 99 na wanatarajia kuongeza fedha zaidi kwa kuwa kazi bado haijakamilika.
"Sisi tumeamua kumuunga mkono Mheshimiwa Rais Samia kwani eneo la Kikatiti halina zahanati ni jambo jema watu wa hapa wakipata huduma ya afya kwa kuwa huu ujenzi ulikwama tangu mwaka 2013,"amesema Mwaisemba
Mjumbe wa Kamati ya Siasa mkoani Arusha,Robert Kaseko amesema, kitendo cha Rais Samia kutoa shilingi milioni 10 kilikuwa ni chachu ya kuchochea ujenzi unaoendelea na kumwagia sifa kiongozi huyo kwamba ni mpenda maendeleo.
Kaseko alisema kuwa kamati ya siasa mkoa wa Arusha imeridhishwa na kazi nzuri inayofanywa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Meru,Mwalimu Zainab kwa kuwa ni mfuatiliaji na msimamizi mzuri wa miradi ya maendeleo.
"Tunamshukuru Rais Samia kwa kutuchagulia viongozi wapenda maendeleo kamati ya siasa mkoa wa Arusha hakika tumeridhishwa na kazi inayofanywa mkurugenzi kwa kufuatilia na kusimamia vyema miradi ya maendeleo,"alisema Kaseko.