NA GODFREY NNKO
SHIRIKA la Ndege Tanzania (Air Tanzania) limeendelea kutanua wigo wake wa kutoa huduma katika mataifa mbalimbali duniani ambapo leo Julai 17, 2022 limeanza rasmi kufika Guangzhou nchini China.
Safari zingine ni ile ya Johannesburg nchini Afrika Kusini,Lusaka nchini Zambia, Harare nchini Zimbabwe, Mumbai nchini India, Entebbe nchini Uganda, Comoros, Bujumbura nchini Burundi na hivi karibuni safari mpya zinatarajiwa kuanza za Ulaya.
"Leo (Julai 17, 2022) tumeanza rasmi safari za moja kwa moja kutoka Dar es Salaam kwenda Guangzhou. Safari zitakuwa kila Jumapili na tiketi kwa sasa zinapatikana makao makuu ya ofisi zetu,"imeeleza sehemu ya taarifa fupi iliyotolewa na Air Tanzania.
Kwa nyakati tofauti,baadhi ya wakazi wa Jiji la Dar es Salaam wameieleza DIRAMAKINI kuwa, hatua hiyo ya Air Tanzania kupanua wigo wa kutoa huduma za usafiri wa anga ndani na nje ya nchi inafaa kupongezwa huku wakiwataka watumishi wote ambao wameaminiwa kutoa huduma kuzingatia ukarimu, hekima na ubunifu ili kuliwezesha shirika kuaminiwa zaidi.
"Ukarimu, hekima na ubunifu ndiyo siri ya biashara ya usafirishaji, hivyo ni ombi langu kwa watumishi wa Shirika la Ndege Tanzania kuzingatia hayo, tunatarajia kuliona shirika letu linatoa huduma si Mashariki ya Kati tu au Afrika tu bali kila kona ya Dunia mfano Ulaya, Amerika na Amerika ya Kusini, hiyo ndiyo shauku ya Watanzania.
"Yaani ifike mahali, badala ya watalii kukodisha ndege za makampuni au kutumia za mashirika mengine huko nje, Chaguo lao la kwanza liwe ni ndege za Tanzania, kwa kuwa tutakuwa tumesambaa kote duniani,"amesema Idrissa Hussein ambaye ni mjasiriamali jijini Dar es Salaam.
Kwa upande wake Julieth Robert mkazi wa jiji la Dar es Salaam amesema, safari za Air Tanzania kutoka Dar es Salaam kwenda Guangzhou si tu kwamba zina manufaa kwa shirika hilo bali ni hatua moja wapo inayodhirisha kuwa,uhusiano kati ya Tanzania na China umeimarika zaidi.
"Hii ni ishara kwamba,uhusiano wetu wa kidplomasia na mataifa mengine duniani ikiwemo China yamezidi kuimarika zaidi, tunapoimarisha uhusiano wa kidplomasia na mataifa mengine kuna matunda mengi ambayo tunayapata mfano leo watu wanatoka Dar moja kwa moja kwenda China kwa ndege ya Taifa, hii ni hatua njema ambayo inastahili kupongezwa sana, kikubwa kila mmoja aliyeaminiwa aonyeshe uaminifu, bidii na ubunifu kazini,"amesema Robert.
Miongoni mwa sababu kuu zilizochochea Serikali kufufua Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) ni kujenga heshima na kulinda hadhi ya Taifa kupitia ndege zake.
Pia ilikuwa ni kuimarisha na kuboresha huduma za usafiri wa anga nchini ili kuwawezesha wakulima na wafanyabiashara kuyafikia masoko ya kimataifa kwa urahisi na kukuza sekta ya utalii nchini.