Asante Simbu, Asante Simbu! umetuheshimisha sana Simbu

NA LWAGA MWAMBANDE (KiMPAB)

MWANARIADHA wa Mbio Ndefu Marathon (42KM),Bw. Alphonce Felix Simbu amenyakua Medali ya Fedha (Silver Medal at Commonwealth) kwa kukimbia muda (2:12:29) nyuma ya raia wa Uganda, Victor Kiplagat (2:10:55) na Mkenya,Michael Githae wa tatu kwa muda (2:13:16).
Ni kwenye Mashindano ya Jumuiya ya Madola yaliyofanyika jijini Birmingham nchini Uingereza jana Julai 30,2022.

Lilikuwa miongoni mwa tukio ambalo liliwapa furaha kubwa Watanzania, kutokana na ukame wa muda mrefu wa kutotwaa medali za Kimataifa kupitia mashindano hayo.

Kwa ushindi huo, Simbu amejihakikishia bonusi ya dola 7000 ambayo ni ahadi ya Serikali kwa kila mchezaji atakayeshinda medali ya fedha kwenye michezo hiyo, huku shaba ikiwa dola 5000 na dhahabu dola 10,000.

Mshairi wa kisasa, Bw.Lwaga Mwambande anakushirikisha jambo kutokana na hatua hii muhimu ya Simbu, karibu uendelee;

1:Simbu katuheshimisha, tunang'ara Tanzania,
Pazuri katufikisha, sote tunafurahia,
Madola ametingisha, kumbukumbu yaingia,
Mwanariadha hongera, timu Madola kongole.

2:Ukame ulitutisha, Madola tukiingia,
Wa kwetu kuwakilisha, vila juu kufikia,
Mteja umeshakwisha, ni furaha Tanzania,
Mwanariadha hongera, timu Madola kongole.

3:Mungu katuneemesha, mwaka tunapitia,
Makubwa tumefikisha, inatujua dunia,
Timu tatu kufikisha, mashindano ya dunia,
Mwanariadha hongera, timu Madola kongole.

4:Warriors lianzisha, kwenda kombe la dunia,
Mabinti soka watisha, India tawakilisha,
Simbu moto kauwasha, medali kutushindia,
Mwanariadha hongera, timu Madola kongole.

5:Kule COSAFA twatisha, jinsi tunajipigia,
Mabinti waaminisha, kazi wanaijulia,
Heko tunazifikisha, Serikali Tanzania,
Mwanariadha hongera, timu Madola kongole.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news