Balozi Kayola afungua mafunzo ya wanahabari kuhusu SADC, aelezea mikakati ya Serikali

NA GODFREY NNKO

SERIKALI ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imesema kuwa, itaendelea kushirikiana na makundi mbalimbali katika jamii vikiwemo vyombo vya habari ili kuhakikisha wanayafahamu malengo na mikakati ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) waweze kuibua fursa mbalimbali zilizopo katika nchi wanachama kwa lengo la kuwashirikisha Watanzania waweze kuzitumia kujiendeleza.

Hayo yamesemwa leo Julai 25, 2022 na Balozi Agnes Kayola wakati akimwakilisha Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Joseph Sokoine katika ufunguzi wa mafunzo ya siku mbili kwa wanahabari mjini Bagamoyo mkoani Pwani yanayoratibiwa na Wizara ya Mambo ya Nje kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Ujerumani (GIZ).

Lengo la warsha hiyo ni kuwajengea uelewa wanahabari kuhusu Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) ili waweze kushiriki kikamilifu kutoa taarifa chanya ambazo zitakuwa na hamasa kwa Watanzania waweze kuzitambua fursa zilizopo katika jumuiya hiyo.

"Tanzania ni miongoni mwa nchi waanzishi wa SADC ambayo ina umri wa miaka 40. Waandishi wa habari mna mchango mkubwa kuhakikisha kundi la vijana linafahamu ipasavyo umuhimu wa SADC ili waweze kushiriki na kuzitumia fursa zilizopo katika jumuiya hii ya kikanda kwa manufaa,"amesema Balozi Kayola.

Amesema, licha ya fursa nyingi zilizopo katika nchi wanachama wa jumuiya hiyo, pia Tanzania inazo huduma nyingi ambazo zikitumika ipasavyo zitaweza kuwa na mchango mkubwa katika uchumi wa jamii na Taifa kwa ujumla.

"Pia kutokana na fursa zinazopatikana tutaendelea kutumia lugha yetu ya Kiswahili kama bidhaa, hivyo jukumu kubwa ambalo mnapaswa kulifahamu ni kuhakikisha mnakitumia Kiswahili ipasavyo katika kutoa taarifa zenu,"amesema.

Amefafanua kuwa, malengo ya SADC kama ilivyoelezwa katika Kifungu cha 5 cha Mkataba wa SADC (1992) ni kufikia maendeleo ya kiuchumi, amani na usalama, na ukuaji, kupunguza umaskini, kuimarisha kiwango na ubora wa maisha ya watu wa Kusini mwa Afrika.

Sambamba na kusaidia watu wasiojiweza kijamii kupitia Ushirikiano wa Kikanda. "Malengo haya yanapaswa kufikiwa kwa kuongezeka kwa Mtangamano wa Kikanda, unaojengwa kwa misingi ya kidemokrasia, na maendeleo yenye usawa na endelevu,"amesema.

Mikakati

Balozi Kayola amesema kuwa, kupitia SADC wana mikakati mbalimbali ikiwemo kuwaenzi viongozi waanzilishi akiwemo Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

"Kwa kuzingatia hilo sanamu ya Mwalimu Nyerere itajengwa kwenye jengo la amani na usalama huko Addis Sababa nchini Ethiopia, mkakati huo unaendelea,"amesema.

Pia amesema, jukumu lingine walilonalo ni kuhamasisha jamii ya Watanzania waaweze kufahamu kuhusu majukumu, malengo na fursa zinazopatikana kwenye jumuiya ya SADC.

"Lengo lingine ni kuhamasisha umoja na ushirikiano katika nchi wanachama, kwa kulizingatia hilo Mheshimiwa Dkt.Jakaya Kikwete,Rais mstaafu waa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Jopo la Wazee wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), linaloshughulikia migogoro katika nchi wanachama wa jumuiya,"amesema Balozi Kayola.

Amesema, lengo lingine ni kutoa elimu kuhusu mtangamano wa jumuiya hiyo na ushiriki wa sekta ya habari katika kuhakikisha wanashiriki kikamilifu kufikisha taarifa chanya.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news