NA DIRAMAKINI
KWA upekee bao la winga Pape Ousmane Sakho wa Simba SC alilofunga dhidi ya ASEC kwenye mechi ya Kundi D katika Kombe la Shirikisho Afrika limetwaa tuzo ya Bao Bora la Mwaka Afrika katika Tuzo za Shirikisho la Soka Afrika (CAF).
Hilo lilikuwa bao pekee ambalo lilitembea zaidi ya kilomita 5927 kutoka jijini Dar es Salaam hadi mji wa Giza huko nchini Misri huku likiwapa mshangao vigogo wa CAF.
Pape Ousmane Sakho alifunga bao hilo dhidi ya ASEC kwenye mechi ya Kundi D Kombe la Shirikisho Afrika .
Katika sherehe za utoaji wa tuzo hizo za Shirikisho la Soka Afrika (CAF) jana usiku mjini Rabat nchini Morocco, Sakho alishinda dhidi ya Gabadinho Mhango wa Malawi na Orlando Pirates na Zouhair El Moutaraji wa Morocco na Wydad Athletic alioingia nao fainali.
Winga huyo alifunga bao hilo dakika ya 12 tu akimalizia krosi ya beki wa kulia, Shomari Kapombe katika ushindi wa 3-1 dhidi ASEC Mimosas ya Februari 13, mwaka huu Uwanja wa Benjamin Mkapa uliopo Halmashauri ya Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam.
Aidha, washindi wengine wa tuzo za CAF mwaka huu ni nyota wa Senegal aliyejiunga na Bayern Munich akitokea Liverpool, Sadio Mane ambaye amebeba tena Tuzo ya Mwanasoka Bora wa Afrika mbele kipa Edouard Mendy wa Chelsea na Mohamed Salah wa Misri na Liverpool.
Wasenegal wengine waliobeba tuzo ni Aliou Cisse akichukuwa ya Kocha Bora wa Mwaka na Pape Matar Sarr wa Tottenham Hotspur akiondoka na ya Mwanasoka Bora Chipukizi.
Asisat Oshoala wa Nigeria alishinda kwa mara ya tano ya rekodi Tuzo ya Mwanasoka Bora wa Kike, huku Senegal ikishinda tuzo ya timu Bora ya Taifa na Wydad Athletic ikibeba Tuzo ya Klabu Bora ya Wanaume na Mamelodi Sundowns Klabu Bora ya Wanawake.
Pia mchezaji bora wa kike wa klabu ni Evelyn Badu (Ghana & Sekondi Hasaacas Ladies/Alvaldsnes), mchezaji bora wa kiume wa klabu, Mohamed El Shenawy (Egypt & Al Ahly), mwanasoka bora chipukuzi wa kike,Evelyn Badu (Ghana & Sekondi Hasaacas Ladies/Alvaldsnes).
Wengine ni mwanasoka kocha bora wa mwaka mwanamke,Desiree Ellis (Afrika Kusini), klabu bora ya mwaka ya wanaume,Mamelodi Sundowns (South Africa), klabu bora ya mwaka ya wanaume ni Wydad Athletic Club (Morocco),timu bora ya Taifa ya wanaume,Senegal.