NA DIRAMAKINI
KAMPUNI ya Kichina ya utengenezaji magari ya BYD imeuza magari 641,400 ya umeme katika nusu ya kwanza ya mwaka huu.
Hilo ni ongezeko la asilimia 315 kwa mwaka, matokeo ambayo yanaifanya kampuni hiyo kuipita Kampuni ya Tesla kwa kuwa bingwa wa mauzo ya magari ya umeme duniani.
Hayo ni kwa mujibu wa takwimu za mauzo kutoka BYD ambapo Tesla iliuza magari 568,600 katika nusu ya kwanza ya mwaka huu.
Kampuni hiyo imejivunia rekodi hiyo ya kipekee, licha ya changamoto zinaoendelea zinazosababishwa na kufungwa kwa hivi karibuni kwa shughuli mbalimbali za uzalishaji nchini humo kutokana na UVIKO-19.
Aidha, kampuni sasa iko tayari kufikia lengo lake la mauzo ya magari milioni 1.5 kwa mwaka huu. Kwa kulinganisha na Tesla ambayo iliwasilisha magari 564,743 kuanzia Januari hadi Juni 2022.
BYD ni kampuni kubwa ya kutengeneza magari ya Kichina iliyoko Shenzhen, Mkoa wa Guangdong. Inauza magari chini ya chapa ya BYD.
Ilianzishwa mwaka 1995, BYD ilianza kama mtengenezaji wa betri na iliingia katika biashara ya magari mwaka 2003.
Kampuni hiyo imejikita katika maeneo mbalimbali kama vile kuunganisha simu za mkononi na utengenezaji wa mifumo ya nishati jua.