CCWWT watoa ombi serikalini huku wakiwaita wajane kujumuika pamoja

NA DIRAMAKINI

MWENYEKITI Chama cha Wanawake Wajane Tanzania (CCWWT), Bi.Rabia Ally Moyo ameiomba Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kuwawezesha kiuchumi kwa kuwapatia mikopo itakayowawezesha kufanya shughuli mbalimbali za maendeleo.
Katibu wa Chama cha Wanawake Wajane Tanzania (CCWWT), Bi. Sabrina Tenganamba (kushoto), Mwenyekiti wa chama Taifa,Bi. Rabia Ally Moyo (katikati) wakiwa katika picha ya pamoja na mmoja wa wajane hivi karibuni katika maadhimisho ya Siku ya Wajane Duniani.

Amesema, iwapo wajane ambao ni kundi kubwa nchini watajengewa uwezo kiuchumi wataweza kukabiliana na changamoto mbalimbali ambazo wanazipitia.

"Tunaamini kuwa, Serikali ikitujengea uweze ikiwemo kupata kipaumbele katika fursa mbalimbali za mikopo na hata ruzuku ya TASAF itatuwezesha kuendesha miradi mbalimbali ambayo itakuwa chanzo cha kuinua vipato vyetu ili tuweze kuziendesha familia na kutimiza mahitaji,"amesema.

Naye Katibu wa Chama cha Wanawake Wajane Tanzania (CCWWT), Bi. Sabrina Tenganamba ametoa wito kwa wajane nchini kujiunga na chama hicho.

Amesema, hapa nchini kuna kundi kubwa la wajane ambalo lisipokuwa na ushirikiano wa pamoja ni vigumu kuweza kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazowakabili.

"Sisi kama wajane tuna majukumu mbalimbali ambayo yanatukabili, baada ya waume zetu kufariki si kwamba maisha yanasimama, maisha yanaendelea hivyo lazima tushikamane ili tuweze kuwa na nguvu ya pamoja katika kutatua changamoto zinazotukabili ikiwemo kuhakikisha tunapambana ili tuweze kutimiza ndoto za kielimu na mahitaji mengine kwa watoto tulio nao,"amesema.

CCWWT kikiwa ni chama chenye usajili kutoka Wizara ya Mambo ya Ndani Na. S.A 22697 kinaamini kuwa, umoja baina ya wanawake wajane nchini ni nguvu na silaha kubwa ya kuzikabili changamoto mbalimbali ambazo wanazipitia kila siku.

Amesema kuwa, uundwaji wa chama hicho umelenga kuwaunganisha wanawake wote wajane nchini ili kurahisisha kushughulikia changamoto zinazowakabili Wanawake wajane hasa zile za kisheria.

“’Wanawake wajane wengi wetu wanakabiliwa na changamoto kubwa katika familia zao ikiwemo ya kunyang’anywa mali na kunyanyapaliwa hivyo chama hiki kitakuwa na jukumu hilo la kuangalia chamgamoto hizo na kuzikabili,”amesema. 

Pia amesema, wajane wengi wamekuwa wakifariki kutokana na changamoto mbalimbali hasa ya msongo wa mawazo baada ya kupitia manyanyaso mengi na kuishi maisha magumu ukilinganisha na alipokuwa akiishi na mmewe kabla ya kufariki. 
Amefafanua kuwa, chama hicho kitakuwa na jukumu la kuwajengea uwezo wanachama wake katika kuona wanapata elimu ya ujasiriamali na kuendesha shughuli za kujikimu kimaisha ikiwa ni pamoja na kuona kuwa wananufaika na mikopo mbalimbali hasa ile inayotolewa na serikali. 

Kwa mawasiliano au swali lolote usisite kuwasilisha kupitia 0719541483 au +255 762 291 395.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news