NA DIRAMAKINI
KATIKA kuunga mkono kauli ya Rais Samia Suluhu Hassan kuwa Tanzania ni mahali sahihi pa Biashara na Uwekezaji,Chuo Kikuu Mzumbe kimebuni ubunifu wa mkojo wa sungura kwa ajili kuondoa wadudu waharibifu katika kilimo cha matunda na mbogamboga.
Akizungumza katika Maonesho ya 46 ya Kimataifa ya Biashara yanayofanyika katika Viwanja vya Sabasaba,Mwanafunzi wa Sayansi ya Uzamili Chuo Kikuu cha Mzumbe, Nelson Kissanga amesema katika kufanya tafiti zake,waligundua kuwa mkojo wa Sungura una harufu kali.
Amesema, harufu hiyo sio rafiki kwa wadudu hasa wale waharibifu katika mboga zenye jamii ya maua na matunda.
Kissanga amesema, mkojo wa sungura ni mbadala wa utumiaji wa kupuliza madawa katika mbogamboga na matunda ambapo yanakuwa na madhara kwa watu wengi.
"Mkojo huu wa sungura ni fursa kwa watu wengi kwani unapowafuga sungura na kupata mkojo wao,mfugaji anapaswa kujenga banda la juu (gorofa)kidogo hivyo wanapokojoa kunakuwa na kinga zinazokuwa zinakinga mkojo wao,”amesema Kissanga.
Amesema, mkojo huo hauna shida yoyote kwa watumiaji kwani hauna kemikali yoyote, unakuwa ni mkojo halisi unaotoka kwa Sungura.
"Wadudu ni waharibifu katika mbogamboga na mboga zenye jamii ya maua pamoja na matunda kwani wanapenda kuvutiwa sana na mvuto wake katika kufuata harufu nzuri ya maua hasa yanapochanua,”amesema.
Na kuongeza kuwa,"Tumeongeza mnyororo wa thamani wa mfumo huu wa mkojo wa sungura ni rafiki wa mazingira na rahisi kutumia tunaomba watu wawe tayari kuupokea na kuutumia waone kama fursa,”amesema.