NA DIRAMAKINI
BENKI ya CRDB na Shirika la Fedha la Kimataifa (IFC) wameingia mkataba wa uwezeshaji utakaongeza upatikanaji wa fedha kwa wajasiriamali wadogo na wakati nchini Tanzania na Burundi, na kusaidia kuimarisha uchumi wa nchi zote mbili kutokana na athari za janga la UVIKO-19.
Hafla hiyo ilifanyika katika hoteli ya Johari Rotana iliyopo katikati ya Jiji la Dar es Salaam na kuhudhuriwa na viongozi waaandamizi wa taasisi hizo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela (kushoto) na Makamu wa Rais wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IFC) Afrika, Sergio Pimenta (kulia) wakibadilishana mikataba ya makubaliano ya mkopo wenye thamani ya dola za kimarekani milioni 105 kwa ajili ya kuwawezesha wajasiriamali nchini, katika hafla iliyofanyika katika hoteli ya Johari Rotana, Jijini Dar es Salaam.
Chini ya ushirikiano huo, IFC inatoa mkopo wa dola milioni 100 kwa Benki ya CRDB Tanzania, nusu ya fedha hizo zitakuwa kwa shilingi ya kitanzania, na mkopo wa dola milioni 5 kwa Benki ya CRDB Burundi kusaidia mikopo kwa wafanyabiashara wadogo katika nchi zote mbili, hasa kwa wafanyabiashara wanaomilikiwa na wanawake.

Imebainishwa kuwa fedha hizo zitaongeza upatikanaji wa mikopo ya muda mrefu, ambayo imekuwa adimu kupatikana tangu kuzuka kwa janga la COVID-19.

Wajasiriamali ni kundi muhimu kwa uchumi wa Tanzania na Burundi. Nchini Tanzania, wastani wa biashara ndogo ndogo na za kati ni milioni 3.2, huchangia asilimia 27 ya Pato la Taifa, na kuajiri zaidi ya watu milioni 5.
Hata hivyo, takriban asilimia 81 ya biashara hizi hazina uwezo wa kupata fedha. Biashara nchini Burundi pia zinachangamoto kubwa katika kupata fedha.

Wanawake wameathirika kwa kiasi kikubwa sana janga la UVIKO-19, ambalo limepelekea changamoto nyingi za kiuchumina kuathiri moja kwa moja maisha ya familia na jamii zao,” alisema Abdulmajid Nsekela Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB wakati wa hafla ya utiaji sahihi.
Nsekela aliongezea kuwa ufadhili wa IFC utasaidia maendeleo ya sekta mbalimbali za maendeleo nchini, ikiwamo biashara, kilimo, afya, elimu, makazi, na miundombinu. Maeneo mengine ni pamoja na miradi inayozingatia mabadiliko ya tabianchi, wajasiriamali, pamoja na biashara zinazomilikiwa na wanawake kama ambavyo imesisitizwa katika mkataba huo wa ushirikiano baina ya Benki ya CRDB na IFC.


Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela (kushoto) na Makamu wa Rais wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IFC) Afrika, Sergio Pimenta (kulia) wakitia saini mkataba wa makubaliano ya mkopo wenye thamani ya dola za kimarekani milioni 105 kwa ajili ya kuwawezesha wajasiriamali nchini, katika hafla iliyofanyika katika hoteli ya Johari Rotana, Jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela (kushoto) akizungumza katika hafla fupi ya kutiliana saini mkataba wa makubaliano ya mkopo wenye thamani ya dola za kimarekani milioni 105 kwa ajili ya kuwawezesha wajasiriamali nchini, katika hafla iliyofanyika katika hoteli ya Johari Rotana jijini Dar es Salaam. kulia ni Makamu wa Rais wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IFC) Afrika, Sergio Pimenta.