NA MWANDISHI WETU
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) na Mbunge wa Jimbo la Karagwe, Mhe. Innocent Bashungwa ametoa miezi mitatu kwa Mkurugenzi wa Wilaya ya Karagwe kuhakikisha anatenga fedha za kujenga miundombinu muhimu katika Zahanti ya Kaguta ili ianze kutoa huduma.
Miundombinu hiyo ni pamoja na choo, kichomea taka na shimo la kuchomea kondo la nyuma.
Bashungwa ameyasema hayo leo Julai 13, 2022 katika mkutano wa kusikiliza na kutatua kero za wananchi katika Kijiji cha Nyabwegira na Kagutu Kata ya Ndama wilayani Karagwe Mkoa Kagera na kumuagiza Mkurugenzi kuhakikisha anakamilisha majengo hayo ili zahanati isajiliwe na itoe huduma kwa wananchi.
Amesema, Serikali imeshaleta fedha nyingi katika ujenzi wa zahanati hiyo kushirikiana na michango ya wananchi kwa hiyo majengo hayo yakikamilika yatawezesha zahanati hiyo kusajiliwa na kuanza kupokea madawa na wauguzi.
Aidha, amemuagiza Meneja wa TARURA Wilaya ya Karagwe kufanya upembuzi yakinifu wa Barabara ya Kanyabureza - Kagutu - Runyaga ili iweze kufanyiwa ukarabati hasa katika eneo korofi la Mlima wa Kaguti liwekewe kipande cha lami ili kuepusha ajali na usumbufu katika kipindi cha mvua.
Pia, Bashungwa amesema atakutana na Meneja wa RUWASA ili kutafuta ufumbuzi wa changamoto ya maji katika vijiji vya Nyabwegira na Kagutu ili wasiwe wanatembea mwende mrefu kutafuta huduma ya maji.