NA TITO MSELEM-WM
NAIBU Waziri wa Madini Dkt. Steven Kiruswa amemtaka Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Manyara Mhandisi Ernest Sanka kutoa hati ya makosa kwa mmiliki wa leseni ya uchimbaji madini ya dhahabu Peniel Edward baada ya kwenda kinyume na Sheria ya Madini.
Dkt. Kiruswa ametoa agizo hilo baada ya kutembelea eneo la mgodi huo uliopo katika kijiji cha Maseida wilaya ya Mbulu mkoani Manyara ambapo alizungumza na wachimbaji wadogo na kukagua eneo la mto Mdahaya wanapochimba madini ya dhahabu ndani ya mto huo.
Dkt. Kiruswa amesema ziara yake hiyo, imekuja baada ya Mbunge wa Mbulu Vijijini Fratel Masei kuuliza swali Bungeni kuhusu Serikali kupitia Wizara ya Madini inampango gani kutatua kero zinazosababishwa na mwekezaji ambaye hafuati Sheria ya Madini ikiwemo kuto kuchangia huduma kwa jamii zinazozunguka eneo la mgodi.
Aidha, Dkt. Kiruswa amesema mwekezaji huyo apewe hati ya makosa ambayo itamtaka kutoa utetezi wake ndani ya siku 30 na akishindwa kufanya hivyo atafutiwa leseni yake.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Mbulu Sezaria Makota amesema Paniel Edward ambaye ni mwekezaji amekuwa kero ambapo amesema mwekezaji huyo anaharibu mazingira na hatoi huduma kwa jamii inayozunguka mgodi.
"Mhe. Naibu Waziri mwekezaji huyu tumemsimamisha kuchimba katika eneo la mto baada ya kugundua kuwa, anaharibu mazingira pamoja na kuchafua vyanzo vya maji," amesema Makota.
Naye, Mbunge wa Mbulu Vijijini Fratel Masei amesema mwekezaji huyo amekuwa msumbufu ambapo aliingia mkataba na serikali ya kijiji kuchangia milioni 20 kama mchango wake kwa jamii ambapo mpaka sasa ni zaidi ya mwaka hajatekeleza ahadi yake.
"Mhe. Naibu Waziri naomba utusaidie sisi wanakijiji wa hapa Maseida ili mwekezaji huyu atulipe pesa zetu alizo ahidi kutoa kama mchango wake ili fedha hiyo itekeleze miradi ya maendeleo amesema Masei.
Kwa upande wake, Kamishna wa Madini Dkt. Abdalrahiman Mwanga amesema Sheria ya Madini inamtaka kila mmiliki wa leseni awe na kibali cha utunzaji wa mazingira ikiwemo kutunza vyanzo vya maji ambayo hutumiwa katika shughuli za majumbani, kilimo na mifugo. Hivyo wananchi wanapaswa kuhakikisha mazingira hayo yanatunzwa ikiwemo kuzuia uchafuzi kutoka kwa mifugo.
Aidha, alieleza kuwa, wachimbaji wadogo wengi huchafua mazingira kwa kiasi kikubwa kutokana na matumizi ya zebaki kuliko mchimbaji anaetumia teknolojia ya juu katika uchenjuaji.
Pamoja na mambo mengine, Dkt. Mwanga amewataka wachimbaji wadogo wa madini ya dhahabu wanaochimba ndani ya mto kuhakikisha wanakuwa na kibali cha mazingira na kuchenjua madini yao umbali wa mita 60 kutoka mtoni.