NA DIRAMAKINI
"Paukwa pakawa". Basi, hapo zamani za kale palikuwa na mfalme mwenye masikio kama ya punda,siku zote alikuwa akijifunga kilemba kichwani ili kuficha masikio yake yasionekane kwa watu wake, siku baada ya siku nywele zake zikakua zikawa ndefu sana.
Siku moja mfalme alimwita kinyozi mmoja hodari wa pale kijijni ili amnyoe nywele zake,kinyozi huyo aliambiwa na mfalme asiseme kabisa atakachoona kichwani kwa mfalme,kinyozi alikubali kwamba hataweza kumweleza mtu yoyote juu ya habari ile, mfalme akavua kilemba chake,yule kinyozi akashangaa kumuona mfalme ana mapembe kama yale ya punda.
Alipokuwa anamnyoa alijitahidi sana kujizuia kucheka,alipomaliza akarudi nyumbani alijitahidi sana kutunza ile siri ya mapembe ya mfalme,hata mkewe alimficha,lakini kila akikaa kwenye koo lake kuna kuwa na dukuduku la kutoa ile habari.
Wakati mwingine alishindwa hata kupata usingizi wa uhakika sababu ya roho yake inataka kutoa ile siri ili ajisike vizuri, basi akaamua kwenda porini alipofika akachimba shimo akaliinamia akatoa sauti kwa nguvu akisema "Jamani Mfalme ana masikio kama ya punda" alifanya hivyo kukwepa kuuawa na mfalme kwa kosa la kutotunza siri ya mfalme.
Baadae kwenye lile shimo ukaota mti,ule mti ulikuwa mkubwa baadae pale kwenye mti kila ukivuma upepo kuna maneno yalikuwa yakisikika,"mfalme ana masikio kama ya punda" .
Siku moja kuna mtu alikwenda na yeye porini kwa nia ya kukata miti,alipokuwa anakaribia kwenye mti ule, upepo ukavuma akasikia sauti ikisema mfalme ana masikio kama ya punda,jamaa yule akarudi kijijini mbio, akawaeleza watu juu ya sauti ile ya ajabu aliyoisikia,watu wakaenda pale kwenye mti ghafla upepo ukavuma sauti ikasikika "mfalme ana masikio kama ya punda".
Hatimaye taarifa ikazagaa nchi nzima mfalme pia akasikia habari hizo alisikitika na kuishia kusema "DUNIA HAINA SIRI".