'Huku fursa ni nyingi sana,Watanzania tuchangamke'

NA DIRAMAKINI

MKUTANO maalum uliofanyika leo Julai 23, 2022 kuanzia saa 10 kamili hadi saa 12:30 jioni kwa njia ya ZOOM ukiangazia kukua kwa diplomasia ya uchumi na fursa za kiuchumi zinazopatikana katika nchi za Mashariki ya Kati na Asia umetoa picha na mwelekeo chanya kwa Watanzania ambao wana shauku ya kuvuka mipaka kwa ajili ya kupeleka biashara zao au kuwekeza katika maeneo mbalimbali duniani .
Kwa uratibu wa Watch Tanzania, mkutano huo ambao umewakutanisha wadau mbalimbali wakiwemo wanadiplomasia ndani na nje ya Tanzania, umedhaminiwa na Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) na Kampuni ya Mawasiliano ya simu za mkononi ya Airtel Tanzania. Wamesema nini;

MHE.PROF GADIUS KAHYARARA KATIBU MKUU WIZARA YA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA

"Ili kurahisisha mfumo mzima wa kuhudumia hawa wawekezaji tumeona ni lazima tuwe na Digital Platform, ambapo mwekezaji kwa kutumia teknolojia ya kisasa akiwa na password moja anaweza kupata zile huduma zote ambazo anatakiwa kwa ajili ya uwekezaji.
"Ni hatua kwa hatua mageuzi mengi yamefanyika katika Serikali ya Awamu ya Sita, wawekezaji sasa hivi wanarudi kwa sababu vile vikwazo vya kodi vimeondolewa kwani Mhe. Rais (Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan) aliagiza tukusanye kodi kwa haki na TRA wamesimamia vizuri eneo hilo na limekuwa na matokeo makubwa,"amesema.

SHARIFF A. SHARIFF MKURUGENZI MTENDAJI WA MAMLAKA YA KUKUZA UWEKEZAJI ZANZIBAR (ZIPA)
"Nchi za Asia ni muhimu kwa biashara na nchi zetu kwanza zina idadi kubwa ya watu si chini ya Bilioni 4.7 hao ni wengi sana na sasa hivi kiuchumi na unakuwa katika hali ambayo ni nzuri.

"Uchumi wao ni uchumi ambao kwa kweli kwa vyovyote vile tunahitaji Tanzania na mashirikiano hayo kupitia Economic Diplomacy ndipo tunaweza kufanya wao kuleta ama sisi kupeleka bidhaa kwao,"amesema.

BALOZI MHE. ANISA K. MBEGA BALOZI WA TANZANIA NCHINI INDIA
"Hivi karibuni mwezi Juni tarehe 6 mwaka 2022 tumeshuhudia utiaji saini wa mikataba ya ujenzi wa miradi ya maji katika miji 28 wenye kugharimu shillingi trilioni 1 ambao utanufaisha wakazi milioni 6 katika miji hiyo, hii ikiwa ni nia njema ya Mhe.Rais kumtua mama ndoo kichwani.
"Pia nchi ya India imekuwa ikishirikiana na Tanzania katika mambo mbalimbali ikiwemo ushirikiano katika Sekta ya Ulinzi (Jeshi), kwani kumekuwa na programu mbalimbali za mafunzo kwa wanajeshi wetu kuja India kujifunza zaidi kuongeza ufanisi wake,"amesema.

BALOZI MHE. BARAKA H. LUVANDA BALOZI WA TANZANIA NCHINI JAPAN

"Kazi kubwa kama Balozi ni kutekeleza Diplomasia ya Uchumi kwa kuitangaza Tanzania kama ni sehemu sahihi kwa wawekezaji, wafanyabiashara na watalii kutoka nchi hizo tunazosimamia.
"Tanzania na Japan zimekuwa na Mahusiano ya kihistoria tangu kupatikana Kwa uhuru wa Tanganyika na yamejengeka kwa muda mrefu, mahusiano haya yamewezesha nchi zote mbili kunufaika kiuchumi, kijamii na kidiplomasia.

"Katika kutekeleza Diplomasia ya Uchumi majukumu muhimu ambayo tunayasimamia ni kuvutia wawekezaji wa Japan, kutafuta masoko ya bidhaa za Tanzania nchini Japan, misaada na mikopo ya masharti nafuu kwa miradi ya maendeleo ya Tanzania,"amesema.

BALOZI MHE. MOHAMMED MTONGA BALOZI WA TANZANIA NCHI ZA KIFALME ZA KIARABU

"Ni moja ya nchi zenye uchumi mkubwa na zenye rasilimali kubwa na sisi kama Balozi wajibu wetu mkubwa sasa hivi ni kuvutia mitaji na wawekezaji kuja kuwekeza Tanzania na Hali kadhalika kuona fursa ambazo zipo Tanzania tunaweza kufanya biashara Ili tuwe sehemu ya mafanikio ya UAE."Uwekezaji uliopo katika nchi za Falme za Kiarabu hasa hasa katika kitovu cha biashara nazungumzia Dubai ni karibu nchi nyingi za Dunia zinalitazama eneo hili kama Strategic Position ya kuwekeza mitaji yao kwa hiyo unapofanya biashara na UAE ujue unafanya biashara na Dunia. BALOZI MHE. ALI JABIR MWANDINI BALOZI WA TANZANIA NCHINI SAUDI ARABIA

"Saudi Arabia ni wadau wakubwa sana wa sekta ya afya na wamekuwa wakituma madaktari bigwa kuja Tanzania kushirikiana nasi katika hospitali ya moyo ya Jakaya Kikwete, lakini pia mwaka huu mwezi Septemba watakuja Zanzibar kwa mara nyingine.
"Nchi ya Saudi Arabia ina fursa nyingi sana zikiwemo mafuta, teknologia, mazao na nyinginezo, lakini pia Saudi Arabia ina uhaba wa nyama hivyo ni fursa kwa Tanzania kuja kuunza nyama huku kwani soko ni kubwa sana, GDP yake haipungui dola bilioni 820 na ina wakazi milioni 35 huku wenyeji ni wengi zaidi kuliko wageni (asilimia 15-17).

BALOZI MHE. DR. RAMADHANI KITWANA DAU BALOZI WATANZANIA NCHINI MALAYSIA
"Moja ya faida ya uwekezaji kutoka moja ni kuweka utaratibu wa wananchi wenyewe wa kawaida waweze kushiriki katika mwendelezo wa huo uchumi tusiwe tu watazamaji lakini na sisi tuwe wahusika wakuu.
"Uhusiano wetu na Tanzania wa kisiasa ni mzuri sana, lakini pia wa kiuchumi lakini ule urari wa biashara baina ya Tanzania na nchi hizi umekuwa si mzuri kwa maana sisi tunaagiza sana kutoka kwenye nchi hizo ukilinganisha kile sisi tunasafirisha kwenda kwenye nchi hizo,"amesema.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news