NA CHARLES REGESIAN
ILIKUWA mapema asubuhi Mei 24, mwaka 1966 wakati kikosi cha Waziri Mkuu wa Uganda, Apollo Milton Obote alipanga shambulizi kwenye makazi ya Fredrick Edward Kabaka Mutesa, Rais wa Kwanza wa Uganda kufuatia mapambano kati yao ya madaraka.
Mkuu wa kikosi hicho alikuwa Kanali Idi Amin Dada,Kabaka ambaye bado alikuwa anauchapa usingizi wakati milio ya bunduki iliposikika ghafla nje, akatoka mbio toka kitandani na kuvaa nguo zake akaikimbilia bastola yake baada ya kujua nini kilichotokea.
Akatoka nje ya Ikulu mbio kuwaangalia walinzi wake waliokuwa wakirushiana risasi na kikosi cha Obote,ingawa hawakuwa wamejiandaa na walizidiwa wingi na watu wa Obote, lakini walipambana vizuri.
Mapambano yaliendelea kwa saa kadhaa,lakini kufika mchana hali ikaanza kuwa mbaya kwa Kabaka na watu wake, watu wake waliokuwa 500 sasa idadi yao ilishuka hadi watu 20.
Walijishauri kama waendelee na mapambano na kufa au watorokee mahali pengine ambapo watajipanga na kurudi kupambana.
Hivyo wakakimbia kwenye zizi la ng'ombe kupanga jinsi ya kutoroka kwa kuruka ukuta wa Ikulu. Wakati wanaanza kuelekea ukuta wenye urefu wa futi 12 risasi tatu za bunduki zikapigwa,Kabaka na watu wake wakasukumana na kukimbia kuepuka kifo.
Kabaka akapiga magoti na kusali kimya kimya kabla ya kuruka ukuta, akatua chini kwa nguvu na kuvunjika mfupa wake wa mgongoni. Watu wake wawili,Kapteni Jehoash Katende na George Mallo wakafuatia hadi chini.
Mpango wao wa kwanza ulikuwa kuingia Kenya, lakini patroo ilikuwa kali karibu na mpaka wa Kenya wakaamua kuelekea Kongo.
Walikimbia kwa wiki mbili njiani huku wakila matunda na chakula walichopewa na wanavijiji mara wakaingia Bujumbura,Burundi, wakabaki huko kwa muda mrefu na kupanga kutorokea London, mwishoni mwa Juni,1966.
Kabaka akabakia ukimbizini, London, hadi kifo chake mwaka 1969. Sababu ya kifo chake kulingana na ripoti ya mchunguzi wa maiti, ilikuwa ni sumu kali ya pombe,pia daktari alisema kwamba kiwango cha ulevi kilikuwa miligramu 380 kwenye damu ya Kabaka na kuwa hali ilikuwa mbaya kwa sababu ya sumu ilipolinganishwa na uzito wake wa mwili wa kilo 63 na urefu wake wa futi 5.6.
Mwili wake ulizikwa makaburi ya Kensal Green huko London kwa miaka miwili mpaka mwaka 1971 wakati maiti yake ilipofukuliwa na kurudishwa Kampala,Uganda kupewa maziko ya kitaifa chini ya amri ya Idi Amin.Akiwa London Mutesa aliogopa kutembea peke yake alitembea na kaka yake na Wazir wa Fedha.