NA DIRAMAKINI
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Mwinyi amesema lugha ya Kiwahili ni daraja linalowaunganisha na kuwaweka pamoja wana Jumuiya Afrika Mashariki.

Dkt.Mwinyi amesema, hayo katika maadhimisho ya Siku ya Kiswahili Duniani, hafla iliofanyika katika Hoteli ya Golden Tulip iliyopo Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume jijini Zanzibar.
Ameeleza kuwa, lugha ni nyenzo muhimu kwa utangamano na kusema lugha ya Kiswahili imekuwa ikitumika kama daraja la kuwaunganisha na kuwaweka pamoja wana Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Akinasibisha maelezo hayo na kauli mbiu ya maadhimisho hayo isemayo ‘Kiswahili kwa amani, ustawi na Utangamano wa kikanda’, Dkt. Mwinyi amesema, historia inabainisha kuwa maendeleo ya ukuaji na kuimarika kwa matumizi ya lugha ya Kiswahili kumechangiwa na mambo kadhaa ikiwemo shughuli za biashara kupitia misafara ya nchi kavu na baharini baina ya watu wa mwambao wa Afrika Mashariki.

Amesema kufanyika kwa maadhimisho ya Siku ya Kiswahili Duniani kwa mara ya kwanza hapa Zanzibar kumeendelea kuijenga historia ya lugha hiyo na kuiongezea heshima Zanzibar katika juhudi zake za kuiendeleza lugha ya Kiswahili Duniani.
“Hapana shaka hatua ya kukipa Kiswahili hadhi ya kuwa na siku yake maalum si jambo dogo na ni heshima kubwa iliyopewa lugha hii,”amesema.

Amesema, ni jambo la faraja na kutia moyo kuona juhudi mbalimbali zinaendelea kufanywa an nchi za Jumuiya Afrika Mashariki katika kukiendeleza, kukienzi na kukitukuza Kiswahili.
Rais Dkt.Mwinyi amesema Mkutano wa Kikao cha 21 cha Viongozi wa Afrika Mashariki kilichofanyika Februari 2021 uliiidhinisha Kiswahili kuwa lugha rasmi ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (kikazi) katika mikutano ya kimataifa kama vile, Mikutano ya Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) pamoja na mikutano ya Umoja wa Afrika (AU).
Ametumia fursa hiyo kuzitaka nchi zote kuona umuhimu na kuitumia fursa hiyo ya kutangamana kwa kukubali kutumia wataalamu wa Kiswahili kwa njai ya kubadilishana au kuajiri katika shughuli mbalimbali.

Amesema namna bora ya kufurahia uamuzi wa kuwa na Siku ya Kiswahili Duniani ni kuongeza juhudi katika kuimarisha lugha hiyo katika Jumuiya Afrika Mashariki pamoja na taasisi mbalimbali ili kukuza Kiswahili kwa kuzingatia wajibu walionao katika kubuni mbinu bora za kuendeleza lugha hiyo.
“Sisi wenyewe kwanza tuna wajibu wa kuonesha mapenzi kwa lugha yetu kwa kuizungumza kwa ufasaha na usahihi ili tuwe walimu wazuri kwa wanaojifunza,”amesema.
Amesema kuendlea kukua kwa Kiswahili kumeongeza mahitaji ya wataalamu wa lugha hiyo Duniani kupitia nyanja mbalimbali ikiwemo walimu, waandishi wa vitabu, wakalimali na watangazaji wa vyombo vya habari.

Amesitiza umuhimu wa taasisi mbalimbali za elimu kuona mahitaji yanayongezeka ya lugha hiyo na kutumia ipasavyo fursa hiyo kama bidhaa inayoweza kuzalisha ajira.
Ameeleza kuwa, Serikali ya Jamuhuri ya Muuungano wa Tanzania pamoja na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zitaendelea kuunga mkono Kamisheni ya Kiswahili Afrika Mashariki katika juhudi za kukuza na kuendeleza lugha ya Kiswahili.
Aidha, amewapongeza wale wote waliobuni jambo hilo, wakiwemo wadau mbalimbali wa kiswahili na hususan Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO).
Kwa upande wake Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo katika hotuba yake iliyosomwa na Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale, Simai Mohamed Said amesema uamuzi wa maadhimisho hayo kufanyika kwa mara ya kwanza hapa Zanzibar ni jambo la busara na yamezingatia kuwa Zanzibar ndio Makao Makuu ya Kamisheni ya Kiswahili Afrika Mashariki sambamba na kuwa ndio kitovu cha lugha hiyo.

Ameeleza matumaini yake kuwa taaluma iliyopatikana katika Kongamano la Lugha ya Kiswahili lililofanyika jana itatoa mchango muhimu katika dhamira ya Kamisheni ya Kiswahili Afrika mashariki ya kuiendeleza lugha hiyo.
Ametoa rai kwa Nchi za Jumuiya Afrika Mashariki kutumia fursa ya kupata walimu wa lugha ya kiswahili kutoka Zanzibar, kw akigezo kuwa kuna walimu w akutosha na wenye uwezo w akufundisha lugha hiyo, huku nayo ikiwa na mahitaji ya kupata walimu wa masomo ya Sayansi na Hesabati.
Naye Naibu Katibu Mkuu Jumuiya ya Afrika Mashariki Mhandisi Steven Mlote alisema lugha ya kiswahili ina umuhimu mkubwa katika utangamano wa Jumuiya Afrika Mashariki, ikiwa na nafasi kubwa katika kujenga na kuimarisha amani katika nchi mbali mbali za Jumuiya Afrika Mashariki.
Alisema kauli mbiu ya maadhimishi hayo inayosema “kiswahili kwa amani, Ustawi na Utangamano wa Kikanda” inakidhi malengo ya Jumuiya hiyo katika jitihada zake za kukuza utangamano wa kikanda.
Alieleza kuwa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki zina bahati kubwa ya kuzungumza lugha hiyo ambayo haikurithiwa na wakoloni na ikiwa na matumizi mapana Duniani.
Aidha, kwa nyakati tofauti wakitoa salamu za nchi zao, Wawakilishi wa nchi wanachama wa Jumuiya Afrika Mashariki kutoka Burundi, Kenya,Rwanda, Sudan Kusini na Uganda walipongeza juhudi za Jumuiya Afrika Mashariki na Kamisheni ya Kiswahili ya Afrika Mashariki ya kufanikisha vyema maadhimisho hayo.

Wawakilishi hao walisema kufanyika kwa maadhimisho hayo hapa Zanzibar kwa mara ya kwanza ni historia ya pekee katika kukuza lugha hiyo na kubainisha kuwa Kiswahili ni lugha ya kwanza Afrika na ya nane Duniani kwa kuwa na siku maalum ya kuadhimishwa.
Walisema wamepokea na kuthamini tamko la Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) la kuitambua Julai 7 kuwa siku ya Kiswahili Duniani, wakibainisha kutumika kwa ajili ya kujenga amani na ushirikiano.
Wawakilishi hao walisema Kiswahili ni lugha ya nne nchini Rwanda ambapo hufundishwa katiika skuli zote, ambapo pamoja na mambo mengine kinalenga kudumisha ujirani mwema.
“Tunahitaji misaada kutoka nje ya nchi yetu ili kupata msukumo wa matumizi ya lugha ya kiswahili, lugha hii itaweza kuiunganisha jamii,”alisema John Ayem Mareech kutoka Suda Kusini.
Katika hatua nyingine, Katibu Mtendaji wa Baraza la Kiswahili Zanzibar (BAKIZA), Dkt. Mwanahija Juma alitumia fursa hiyo kusisistiza nchi za Jumuiya Afrika Mashariki kaunzisha Mabaraza ya kiswahili ikiwa ni hatua thabiti ya kuiendeleza lugha hiyo.
Aidha, akimwakilisha Katibu Mtendaji wa Baraza la Kiswahili Tanzania (BAKITA) Mchunguzi Lugha Mkuu wa BAKITA Dk. Rizati Mmari alisema ni muda muafaka kwa nchi zisizo na mabaraza ;kuanzisha kwa kigezo kuwa ni muhimu ambapo miongoni mwa shughuli zake muhimu ni kutoa mafunzo ya vitendo kwa wakalimali na wadau wengineo.
