NA MUNIR SHEMWETA
MAHAKAMA Kuu Divisheni ya Ardhi imepiga hatua kubwa ya usikikizaji mashauri ya ardhi katika kipindi cha kuanzia Julai 2021 hadi Julai 2022 na kusababisha kupungua kwa mrundikano wa mashauri kwenye Divisheni hiyo.
Ulinganishaji kiwango cha ukamilishaji mashauri unaonesha kuwa, Mahakama Kuu- Divisheni ya Ardhi imeweza kuboresha kasi ya kusikiliza mashauri na kuwa na mashauri 1,591 yaliyosikilizwa kuanzia Januari 2022 sawa na asilimia 42 ya mashauri yanayoendelea kusikilizwa hadi kufikia mashauri 1,212 sawa na asilimia 48 ya jumla ya mashauri yaliyopo katika hatua ya kusikilizwa kwa taarifa ya hadi 11 Julai 2022.
Mwelekeo unaonesha kuwa, pamoja na kasi inayoendela ya usikilizwaji mashauri Mahakama Kuu- Divisheni ya Ardhi itabakiza asilimia 15 ya kesi ambazo hazijasikilizwa ifikapo mwisho wa mwaka 2022.
"Mahakama Kuu-Dvisheni ya Ardhi imeweza kupunguza mrundikano mashauri ya ardhi yaliyofunguliwa kuanzia Julai, 2021 hadi Julai, 2022 ambapo kwa Julai 2021 kulikuwa na mashauri 359 yaliyosikilizwa,"amesema Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu- Divisheni ya Ardhi Mhe. Agnes Mgeyekwa.
Aidha, Takwimu zinaonesha mlundikano wa mashauri ya ardhi umeendelea kupungua siku hadi siku kutokana na maboresho mbalimbali yanayoendelea kufanywa na Mahakama Kuu ikiwemo matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano.
"Matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano yamesaidia sana utendaji kazi wa mahakama yetu ikiwemo uwasilishwaji mashauri ambapo washitakiana sasa hawalazimiki kufika kwenye majengo ya mahakama,"amesema Mhe. Agnes Mgeyekwa.
Kwa mujibu wa Jaji Agnes Mgeyekwa, katika kuunga mkono azma ya Mahakama kuelekea Mahakama Mtandao, Divisheni yake inafanya kazi nyingi kwa kutumia teknolojia ya Habari na Mawasiliano (ICT) ikiwemo kusikiliza baadhi ya mashauri kwa njia ya mikutano ya Video Conference.
Akizungumza jijini Dar es Salaam tarehe 18 Julai 2022, Jaji huyo wa Mahakama Kuu-Divisheni ya Ardhi aliongeza kwa kusema kuwa, Mahakama hiyo kwa sasa iko kwenye mabadiliko ya kuelekea mfumo wa kidigitali utakaoiwezesha Divisheni hiyo kuunganishwa na Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa ajili ya kutambua Hatimiliki za Ardhi.
Hata hivyo, alisema pamoja na juhudi kubwa zinazofanywa katika kuboresha utendaji kazi wa Mahakama Kuu - Divisheni ya Ardhi bado kuna changamoto kadhaa alizozieleza kuwa, iwapo zitapatiwa ufumbuzi haraka Divisheni hiyo inaweza kufanya vizuri zaidi kuliko inavyofanya sasa.
''Pamoja na juhudi kubwa tunazozifanya katika kuboresha utendaji kazi wa Mahakama Kuu-Divisheni ya Ardhi bado kuna baadhi ya changamoto kama vile kukosekana majaji wa kutosha , vifaa na mifumo isiyotosheleza kwenye masuala ya teknolojia ya habari na mawasiliano,''alisema Mhe.Agnes Mgeyekwa.
Hivi karibuni Jaji Mkuu, Prof. Ibrahim Juma alifanya ziara katika Mahakama Kuu-Divisheni ya Ardhi ambapo katika ziara yake hiyo alisema umefikia wakati taarifa zinazokusanywa na wizara husika ziweze kupatikana kwa wananchi ili masuala ya ardhi yaweze kuwa wazi zaidi na yasiibue migogoro ambayo inachukua muda mrefu mahakamani.
Aidha, Jaji Mkuu, Mhe. Prof. Juma amebainisha juu ya umuhimu wa Mahakama Kuu Divisheni ya Ardhi kuangalia pia uwezekano wa kutumia usuluhishi kama njia mojawapo ya kupunguza mlundikano wa mashauri ya Ardhi.