Maisha mapya Msomera yawapa faraja wananchi,mamia wahamia kwa hiari kutoka Ngorongoro

NA MWANDISHI WETU

NAIBU Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu, Bw. Kaspar Mmuya amewashukuru wananchi waliohamia katika Kijiji cha Msomera awamu ya nne huku wakionesha furaha yao kwa kuanza maisha mapya ya katika kijiji hicho.
Baadhi ya wananchi waliohamia kwa hiari katika eneo la Msomera Wilayani Handeni kutoka katika Hifadhi ya Ngorongoro wakiwasili rasmi katika kijiji hicho Mkoani Tanga Julai 7, 2022.
Baadhi ya wananchi waliohamia kwa hiari katika eneo la Msomera Wilayani Handeni kutoka katika Hifadhi ya Ngorongoro wakiwasili rasmi katika kijiji hicho Mkoani Tanga Julai 7, 2022. 

Ametoa pongezi hizo Julai 7, 2022 wakati wa zoezi la kuwapokea wananchi waliohamia kwa hiari katika kijiji cha Msomera wilayani Handeni kutoka katika eneo la hifadhi ya Ngorongoro mkoani Arusha ikiwa ni kundi la nne toka zoezi hilo kuanza.

Alieleza kuwa katika awamu hiyo wamewasili jumla ya wananchi 188 wakiwa wenye furaha na kupongeza Serikali kwa uratibu mzuri wa zoezi hilo huku wakitarajia kuishi kwa amani na kuendelea na shughuli zao za kila siku. 
Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia (Sera, Bunge na Uratibu) Bw. Kaspar Mmuya akikabidhi hati miliki ya maeneo kwa ajili ya makazi na mashamba kwa wananchi waliowasili katika eneo la Msomera Wilayani Handeni Mkoa wa Tanga Julai 7, 2022. 

Aidha, Mmuya alitumia fursa hiyo kuwaasa wananchi kutumia maeneo hayo kimkakati kwa kuanza kuchangamkia fursa za kiuchumi zilizopo ikiwemo ufugaji wa kisasa utakao chagiza ongezeko la kipato kwa wakazi hao wapya.
Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Bw. Kaspar Mmuya pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Handeni Mhe. Siriel Mchembe wakikagua moja ya hati miliki kabla ya zoezi la kugawa kwa wakazi wapya wa eneo la Msomera waliohamia kwa hiari kutoka katika eneo la Hifadhi la Ngorongoro. 

“Kipekee namshukuru Rais wetu mpendwa Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha zoezi hili kufanyika kwa weledi mkubwa na hii inaonesha namna Serikali yenu inavyowajali, tunawaahidi tutaendelea kushirikiana na zitumieni fursa zilizopo Msomera,”alisema Mmuya.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Handeni Mhe. Siriel Mchembe akizungumza wakati wa zoezi hilo alisema Wilaya yake imejipanga kuhakikisha inatoa ushirikiano usiku na mchana huku akiwahakikishia wananchi wote waliohamia katika eneo hilo watapata huduma zote muhimu ambapo amewasihi kubadili mitazamo na kujua kuwa wamekuwa wakazi rasmi wa Msomera. 
Pia aliwataka kuhakikisha wanapeleka watoto shule kwa kuzingatia ni jambo muhimu na kuahidi kufanya sense ya kuhakikisha kila mtoto mwenye sifa ya kwenda shule anapelekwa ili kuwa na kizazi chenye elimu na kujikwamua kimaisha. 

“Tujenge kizazi chetu hapa msomera chenye elimu, na mimi huu utakuwa ni wimbo wangu, hakikisheni mnapelekea watoto shule na nitafanya sense ya kuhakikisha kila mtoto anapata haki ya elimu,”alisema.

Akitoa kauli ya ukiri wa kupokea wananchi na mifugo kwa awamu hiyo ya nne alisema mifugo yote itakayokuwa eneo hilo itunzwe na kuhakiksha inahudumiwa vyema ili ilete manufaa kwao na wakazi wengine wa Handeni hata nje ya hapo. 

“Hadi leo ninakiri kumepokea jumla ya kaya 104 kutoka kwa Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro, idadi ya watu 690 ikiwemo watoto 102, ila kwa awamu hii ya nne nimepokea idadi ya watu 188 ambapo148 ni watu wazima na 40 ni watoto ,upande wa mifugo ninakiri kupokea jumla ya mifugo ikiwemo; ng’ombe 240, mbuzi 348, punda 22, kondoo 274 kwa ujumla ya idadi za mifugo toka awamu ya kwanza tumepokea jumla ya ng’omba 638, kondoo 516 na mbuzi 836 mifugo hii itunzwe na kuhakiksha inahudumiwa kwa usahihi,”alisisitiza Mhe Mchembe. 
Naye Aliyekuwa Diwani ya Kakesio kutoka Ngorongoro Mhe. Johannes Tiamasi akitoa neno la shukran aliendelea kupongeza namna zoezi lilovyoearibiwa huku akiwasihi viongozi wenzake waliobaki Ngorongoro kuacha kutoa taarifa zisizo sahihi kuhusu maeneo ya Msomera ikiwemo dhana potofu juu ya zoezi zima la kuhamia katika eneo hilo. 

“Msomera ni nzuri sana, ardhi ni nzuri niwatoe hofu waliobaki Ngorongoro kujiandikisha kwa kuzingatia nafasi ya kufanya hivyo bado ipo, hakika hili ni eneo la maziwa na asali hivyo tulikimbilie,”alisisitiza Tiamasi 

Naye Mwenyekiti wa Msomera Bw. Martine Oleikayo Paraketi alieleza kwamba wataendelea kutoa ushirikiano kwa uongozi uliopo huku akiwaasa wananchi hao kuiona msomera yeye mazingira rafiki katika kila sekta ikiwemo uwepo wa miundombinu ya maji, mawasiliano, umeme, afya na elimu. 
“Msomera kumenoga kwani kuna kila huduma muhimu tunayohitaji hivyo tujisikia vizuri kuwepo hapa na tuendelee kuishi kwa amani na upendo kwa kuzingatia nchi yetu ni kitovu cha amani tuijenge msomera yetu iwe ya mfano kwa wengine,”alisema Oleikayo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news