NA KADAMA MALUNDE
KAMISAA wa Sensa ya Watu na Makazi Tanzania Bara Mhe. Anne Makinda ameipongeza Serikali ya Mkoa wa Shinyanga kwa maandalizi mazuri inayoendelea nayo katika kuhamasisha wananchi kushiriki kikamilifu katika Sensa ya Watu na Makazi itakayofanyika Agosti 23,2022.
Kamisaa wa Sensa ya Watu na Makazi Tanzania Bara Mhe. Anne Makinda akizungumza katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga alipowasili kushiriki Bonanza la hamasa ya Sensa ya Watu na Makazi lililoandaliwa na Kundi la SHY TOWN VIP leo Jumamosi Julai 2,2022. (Picha na Malunde 1 blog).
Kamisaa wa Sensa ya Watu na Makazi Tanzania Bara Mhe. Anne Makinda (kushoto) akizungumza katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga alipowasili kushiriki Bonanza la hamasa ya Sensa ya Watu na Makazi lililoandaliwa na Kundi la SHY TOWN VIP leo Jumamosi Julai 2,2022. Katikati ni Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Sophia Mjema, kushoto ni Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Shinyanga Beda Chamatata.
Makinda ambaye ni Spika wa Bunge Mstaafu ametoa pongezi hizo leo Jumamosi Julai 2,2022 wakati akipokea taarifa ya maandalizi ya Sensa ya watu na makazi Mkoa wa Shinyanga alipowasili mkoani Shinyanga kushiriki Bonanza la Kuhamasisha Sensa ya Watu na Makazi lililoandaliwa na Kundi la Mtandao wa Kijamii maarufu SHY TOWN VIP Mjini Shinyanga.
“Joto la Sensa ya watu na makazi Shinyanga ni kubwa sana. Hawa Vijana wa Shy Town VIP wanahamasa kubwa, Shy Town VIP wanatisha, Vijana hawa ni hatari, hamasa yenu ni kubwa, tunawashukuru kwa ushirikiano mnaotoa. Endeleeni kutoa elimu na kuhamasisha wananchi washiriki zoezi la Sensa ya watu na makazi Agosti 23,2022,”amesema Makinda.
“Shinyanga mnaenda vizuri, tunataka kila mtu atakayelala ndani ya mipaka ya Tanzania ahesabiwe. Ukilala Tanzania Agosti 23,2022 utahesabiwa. Serikali ya mkoa wa Shinyanga hakikisheni pia mnakaa na wahusika wa nyumba za kulala wageni muwaandae ili watoe ushirikiano mzuri. Mwezi huu wa Julai na mwezi Agosti kelele za sense ziongezwe ili kila mmoja afahamu kuhusu Sensa,”ameongeza Makinda.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga akizungumza wakati Kamisaa wa Sensa ya Watu na Makazi Tanzania Bara Mhe. Anne Makinda alipowasili katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga kwa ajili ya kushiriki Bonanza la hamasa ya Sensa ya Watu na Makazi lililoandaliwa na Kundi la SHY TOWN VIP leo Jumamosi Julai 2,2022.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Sophia Mjema amesema wamejipanga vizuri ili kuhakikisha zoezi la sensa ya watu na makazi linafanikiwa kama ilivyokusudiwa.
“Napenda kukuhakikisha kuwa hili Vibe ‘hamasa’ hili ulilokutana nalo tutahakikisha unaendelea kuliona ,tutaendelea nalo. Tunakushukuru kwa ujio wako kwani unaongeza hamasa zaidi kwa wananchi kushiriki katika Sensa ya watu na makazi Agosti 23,2022”,amesema.
Mwenyekiti wa SHY TOWN VIP, Mussa Ngangala akizungumza wakati Kamisaa wa Sensa ya Watu na Makazi Tanzania Bara Mhe. Anne Makinda alipowasili katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga kwa ajili ya kushiriki Bonanza la hamasa ya Sensa ya Watu na Makazi lililoandaliwa na Kundi la SHY TOWN VIP leo Jumamosi Julai 2,2022.
Naye Mwenyekiti wa SHY TOWN VIP, Mussa Ngangala amesema wanachama wa kundi hilo wanatambua umuhimu wa Sensa ya watu na makazi ndiyo maana wameandaa Bonanza la Kuhamasisha wananchi kushiriki Sensa ya watu na makazi kwa ajili ya maendeleo ya nchi huku akimshukuru Mhe. Anne Makinda kwa kukubali wito wa kuja kuungana na wana Shinyanga kuhamasisha sensa ya watu na makazi.