Mambo mazuri yanakuja kuhusu ibada ya Hijja asema Rais Dkt.Mwinyi huku akisisitiza Sensa Agosti 23

NA DIRAMAKINI 

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema kuwa Serikali inaaendelea kukamilisha taratibu za muundo na sheria kwa ajili ya kuanzisha Mfuko wa Hijja ili uweze kusimamia vyema shughuli zote zinazohusiana na ibada hiyo kwa wananchi wa Zanzibar. 

Alhaj Dkt. Mwinyi ameeleza hayo leo wakati alipokuwa akisoma hotuba yake ya Baraza la Idd Al -Hajj kwa wananchi huko katika viwanja vya Chuo cha Amali Mkokotoni, Mkoa wa Kaskazini Unguja. 
Katika salamu hotuba yake hiyo, Alhaj Dk. Mwinyi alisema kuwa Mfuko huo ukiwepo itakuwa ni rahisi kwa wananchi kujiwekea akiba kidogo kidogo na kupokea misaada ya kifedha kwa Waislamu wenye uwezo ambao watataka kuwasaidia Waislamu wengine kwenda kutekeleza ibada hiyo. 

Aidha, Alhaj Dkt.Mwinyi alisema kuwa Serikali itazifanyia kazi changamoto zilizowasilishwa katika risala ya Mahujaji waliyomkabidhi katika hafla ya kuagana nao ikiwa ni pamoja na kufanya mazungumzo na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa lengo la kutafuta njia itakayoiwezesha Zanzibar kuwa na akaunti yake kwa ajili ya kusimamia na kushughulikia miamala ya kifedha inayohusu shughuli za Hijja kwa upande wa Zanzibar. 

Alhaj Dkt. Mwinyi aliongeza kuwa Serikali itaendelea kutoa unafuu wa tozo mbalimbali kwa mahujaji ikiwemo gharama ya vipimo vya Uviko-19 kama ilivyofanya mwaka huu. 

Hata hivyo, Alhaj Dkt.Mwinyi alitumia fursa hiyo kuupongeza kwa kazi nzuri na kuushukuru sana Umoja wa Taasisi za Hijja Zanzibar kwa kushirikiana na Kamisheni ya Wakfu na Mali ya Amana katika kufanya kazi kwa karibu kwa lengo la kuwasaidia Waislamu wenye nia ya kwenda Hijja. 

Alhaj Dkt. Mwinyi pia, alisisitiza suala zima la umoja na mshikamano kwani ni jambo muhimu katika jamii kwani kutaongeza mapenzi na kuimarisha ushirikiano katika kufanikisha shughuli za kila siku. 
Alieleza kwamba umoja na mshikamano katika jamii huongeza baraka na moyo wa ihsani na huruma ya kuwafikiria watu wenye shida mbali mbali kwa lengo la kuwasaidia. 

Alisisitiza kwamba wakati Waislamu wanasherehekea sikukuu hii ya Idd el Adhha, ni muhimu kuhimizana juu ya wajibu wa kushirikiana katika kulinda na kudumisha malezi bora kwa watoto. 

Alisema kuwa kuwaandaa watoto kwa kuwapa malezi bora ni msingi muhimu katika juhudi za kuimarisha elimu,mapambano dhidi ya dawa za kulevya, vitendo vya rushwa, wizi na ufisadi, udhalilishaji na unyanyasaji pamoja na mambo yote yanayochangia mmong’onyoko wa maadili ndani ya jamii. 

Pamoja na hayo, katika hotuba yake hiyo, Alhaj Dkt. Mwinyi aliwaagiza Wakuu wa Mikoa na Wilaya kupitia Kamati za Ulinzi na Usalama kuhakikisha kwamba wanavisimamia viwanja vyote vinavyotumika kwa sherehe za sikukuu katika maeneo yao ya utawala kwa kuimarisha ulinzi na kusogeza huduma muhimu katika maeneo hayo. 

Katika suala zima la kuimarisha amani, Alhaj Dkt. Mwinyi alisisitiza kwamba kila mmoja kwa nafasi yake awe ni mlinzi wa amani na kuendelea kudumisha amani kwani haina mbada kwani ndio msingi mkuu wa mafanikio yanayopatikana katika utekelezaji wa mipango yote ya maendeleo. 
Akieleza suala zima la sensa inayotarajiwa kufanyika tarehe 23 mwezi ujao wa Agosti 2022, Alhaj Dk. Mwinyi alisema kuwa matayarisho yote ya Serikali yamefikia katika hatua ya kuridhisha ambapo kazi ya kuhamasisha na kuelemisha wananchi wote umuhimu wa kushiriki zoezi hilo muhimu kwa maendeleo inaendelea. 

Sambamba na hayo, Alhaj Dkt. Mwinyi alitoa shukurani kwa Mkoa huo wa Kaskazini Unguja kwa ushirikiano wao ihsani,mapenzi na insafu waliyoionesha katika kufanikisha sherehe hizo zilizofanyika katika Mkoa huo. 

Kabla ya hafla hiyo, Rais Dkt. Mwinyi alipokea gwaride maalum la Jeshi la Polisi lililoandaliwa kwa ajili ya hafla hiyo. 

Alhaj Dkt. Mwinyi pia, alikutana na baadhi ya Masheikh pamoja na Maimamu wawakilishi wa Mkoa huo ambapo alitumia fursa hiyo kutoa shukurani wa viongozi hao wa dini na kuwahimiza kuendelea kuhubiri amani na kuiombea nchi amani pamoja na kuwaombea viongozi wote. 

Mapema asubuhi Alhaj Dkt. Mwinyi aliungana na Waumini wa Dini ya Kiislamu katika sala ya Idd el Adh-ha huko katika msikiti Mkuu wa Ijtmai Kidoti, Mkoa wa Kaskazini Unguja ambapo katika hotuba ya sala hiyo Sheikh Shauri Saleh ambaye alikuwa imamu pamoja na kusoma hotuba ya sala hiyo naye alisisitiza suala zima la amani, ushirikiano na mapenzi miongoni mwa waislamu na wananchi wote kwa jumla. 

Viongozi mbali mbali wa dini na Serikali walitoa shukurani kwa uwamuzi wa Serikali kuifanya shughuli hiyo katika Mkoa huo wa Kaskazini ambapo Waziri wa Nchi Afisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora, Haroun Ali Sulemain alipongeza mashirikiano makubwa yaliyofanyika katika kufanikisha shughuli hizo. 

Katika hafla hizo viongozi mbalimbali walihudhuria akiwemo Makamu wa Kwanza Rais wa Zanzibar Othman Masoud Othman, Makamu wa Pili wa Rais Hemed Suleiman Abdulla, Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Saleh Omar Kabi, Kadhi Mkuu wa Zanzibar Sheikh Hassan Othman Ngwali, Jaji Mkuu wa Zanzibar Khamis Ramadhan Abdalla, Spika wa Baraza la Wawakilishi Zubeia Ali Maulid, Mwenza wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Hafidh Ameir, Mawaziri, Manaibu Waziri pamoja na viongozi wengine wa dini, vyama vya siasa na Serikali. 

Kwa upande wa viongozi wengine wa Kitaifa waliohudhuria hafla hiyo ni viongozi wa Kitaifa wanawake walioongozwa na Mke wa Rais wa Zanzibar Mama Mariam Mwinyi. 
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhajj Dk.Hussein Ali Mwinyi akitekeleza Ibada ya Suna ya kuchinja, baada ya kumaliza Sala ya Eid Al Hajj iliyofanyika Kitaifa Mkoa wa Kaskazini Unguja leo Julai 10,2022 na (kulia kwa Rais) Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh.Saleh Omar Kabi na (kushoto kwa Rais) Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Katiba,Sheria,Utumishi na Utawala Bora Zanzibar Mhe. Haroun Ali Suleiman na Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja Mhe Ayoub Mohammed Mahmoud.(Picha na Ikulu).

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news