NA MWANDISHI WETU
SERIKALI kupitia Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari pamoja na taasisi zilizo chini ya Wizara hiyo zimeendelea kuboresha upatikanaji wa huduma za Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwa jamii ya wafugaji wa kijiji cha Msomera kilichopo Handeni, Tanga ambao ni wakaazi wapya waliohamia kwa hiyari katika kijiji hicho wakitokea katika eneo la hifadhi ya Ngorongoro
Hayo yamezungumzwa na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Jim Yonazi wakati wa ziara ya Makatibu Wakuu katika kijiji cha Msomera iliyofanyika jumatano ya Julai 7, 2022 ya kukagua ujenzi wa miundombinu na ufikishaji wa huduma mbalimbali za kijamii kwa wananchi hao
“Tutahakikisha upande wa mawasiliano hakuna changamoto tena katika kijiji hiki cha Msomera, tutaendelea kuratibu kadiri ambavyo wananchi wanaendelea kuongezeka katika kijiji hiki ili kila mmoja apate huduma bora za mawasiliano ya simu, redio, televisheni pamoja na Anwani ya Makazi ili waweze kushiriki katika uchumi wa kidijiti,”amesisitiza Dkt.Yonazi.
Amesema kuwa, Wizara hiyo inalo jukumu la kuwezesha na kuhakikisha wananchi wa jamii zote ikiwa ni pamoja na jamii hiyo ya wafugaji wanakuwa na uwezo wa kupata na kutumia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano ili waweze kushiriki kikamilifu katika kujenga uchumi wa nchi hasa uchumi wa kidijiti.
Ameongeza kuwa, Wizara hiyo kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) inaendelea na uratibu kuhakikisha kunakuwa na maabara za kompyuta zenye vifaa vya TEHAMA (kompyuta, Printa na Projekta) katika shule ya msingi na sekondari zilizojengwa katika kijiji hicho ili kuboresha mazingira ya kufundishia na wanafunzi waweze kujifunza kisasa zaidi kupitia TEHAMA .
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia sekta ya Mifugo, Bw. Tixon Nzunda, ameipongeza Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwa kufikisha huduma za mawasiliano katika kijiji hicho ambazo zinarahisisha utoaji wa huduma kwa wananchi waliohamia Msomera ambao asili yao ni wafugaji ambapo wataweza kupata vibali vya kusafirisha mifugo na mazao yatokanayo na mifugo kwa njia ya mtandao kupitia simu ya mkononi au kompyuta kwa kuingia kwenye mfumo wa kielektroniki unaoitwa “Mifugo Integrated Management Information System” (MIMIS ).
Naye Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), Bi. Justina Mashiba amesema kuwa ujenzi wa mnara wa kudumu unaojengwa na Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) katika kijiji cha Msomera unajengwa kwa ruzuku ya Serikali kupitia mfuko huo ambapo watoa huduma wengine wanaweza kupangisha kwa kuweka vifaa vyao na kuendelea kutoa huduma katika kijiji hicho.
Akizungumza katika ziara hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), Mhandisi Peter Ulanga amesema kuwa ifikapo Julai 14, 2022 huduma za mawasiliano ya TTCL zitaanza kupatikana katika kijiji hicho lakini pia hadi mwishoni mwa mwezi Julai huduma za mawasiliano za kampuni za Tigo, Airtel, Halotel na Vodacom zitakuwa zinapatikana katika kijiji hicho ambapo wataweka vifaa vyao katika mnara huo.
Ameongeza kuwa ili kuhakikisha kunakuwa na mawasiliano ya uhakika katika kijiji hicho, TTCL itafikisha Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano katika kijiji hicho ili kuhakikisha aina ya mawasiliano ya teknolojia ya 2G hadi 4G yanakuwa ya uhakika na kasi zaidi katika eneo lote la Msomera.
Naye Mwenyekiti wa kijiji ncha Msomera, Bw. Martine Oleikai Paraketi ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia kwa kuamua kuboresha sekta ya elimu kwa kuwezesha wanafunzi wa kijiji cha Msomera kujifunza kupitia vifaa vya TEHAMA na intaneti kuanzia shule ya msingi na Sekondari na wana imani kuwa Msomera itazalisha wasomi wengi.
Kundi la nne la wananchi wanaohama katika eneo la hifadhi ya Ngorongoro kwa hiyari kwenda katika kijiji cha Msomera, wilaya ya Handeni Mkoa wa Tanga lenye kaya 32 na jumla ya watu 188 na mifugo 880 limewasili na kupokelewa na Makatibu Wakuu wakiongozwa na Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Bw. Kaspar Mmuya, Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Mhe. Siriel Mchembe pamoja na wananchi, Julai 7,2022.