NA DIRAMAKINI
MAHAKAMA Kuu ya Tanzania imeahirisha kutoa uamuzi wa maombi ya Halima Mdee na wenzake 18 ya kutaka kibali cha kufungua kesi ya kupinga kuvuliwa uanachama na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) hadi Ijumaa ya Julai 8, 2022.
Uamuzi huo ulikuwa utolewe leo Julai 6, 2022 na Jaji Mustapha Ismail, lakini Naibu Msajili wa Mahakama hiyo, Elimo Massawe amesema, haujakamilika na utatolewa Ijumaa ya wiki hii.
Uamuzi huo unatarajia kutoa hatima ya safari yao ya kupigania uanachama wao na kulinda ubunge wao.
Mheshimiwa Mdee na wenzake wanaomba ridhaa ya kupinga uamuzi wa Baraza Kuu la CHADEMA wa Mei 11, 2022 kwa utaratibu wa Mapitio ya Mahakama, yaani ipitie uamuzi wa CHADEMA kisha itoe amri mbili.
Pia, wanataka Mahakama itengue uamuzi wa CHADEMA kuwavua uanachama kwa madai hawakupewa haki ya kusikilizwa kabla ya kuvuliwa uanachama.
Novemba 27, 2020 Kamati Kuu ya CHADEMA iliwatia hatiani kwa kosa la kwenda kuapishwa kuwa wabunge wa viti maalumu bila ridhaa ya chama hicho.