NA STEVEN NYAMITI-WM
WAZIRI wa Madini Dkt. Doto Biteko amesema Serikali iko katika hatua za mwisho kuanza uzalishaji katika Mgodi wa Makaa ya Mawe wa Kiwira- Kabulo ili Serikali iweze kunufaika na makaa hayo.
Dkt. Biteko amesema hayo Julai 2, 2022 wakati wa ziara yake ya kutembelea mgodi wa Kiwira- Kabulo kukagua shughuli za uchimbaji wa makaa ya mawe na kuzungumza na wananchi wanaowazunguka mgodi huo katika wilaya ya Ileje Mkoani Songwe.
Amesema, tayari Serikali kupitia Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) imesaini mkataba na Kampuni ya ABSA ya nchini Uswiss ambapo tani 60,000 za makaa ya mawe zitauzwa kwa wawekezaji hao.

"Kuna kitu kizuri kinakuja ndio maana tumewekeza fedha katika mradi huu, nataka niwaambieni tuwe na subra na nimesikiliza changamoto za wananchi Serikali itazifanyia kazi ili zitatuliwe mapema," amesema Dkt. Biteko.

Amesema, kuanza kwa uzalishaji katika mgodi huo kutafungua fursa za kiuchumi, ajira za moja kwa moja kwa Watanzania na kuongezeka kwa Pato la Taifa.

Aliongeza kuwa, ili kuboresha uzalishaji Shirika limeagiza mitambo kwa ajili ya uchimbaji na uchakataji wa Makaa ya mawe licha ya kuwepo kwa changamoto ya miundombinu mibovu.

''Tunashukuru Serikali kwa kuona umuhimu wa kufufua mradi huo ambao utanufaisha wananchi wa wilaya za Ileje, Kyela na Rungwe ambao ni majirani zetu'', alisema.