NA DIRAMAKINI
MAHAKAMA Kuu imewaruhusu waliokuwa wanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA),Bi. Halma Mdee na wenzake 18 kufungua shauri la kupinga uamuzi wa chama hicho kuwavua uanachama.
Kutokana na uamuzi huo sasa kina Mdee wanatakiwa kufungua shauri lao hilo ndani ya siku 14 kuanzia leo.

Mahakama hiyo imetoa ruhusa hiyo kwa kina Mdee leo Julai 8, 2022, baada ya kukubaliana na hoja za maombi yao ya ridhaa ya kufungua shauri hilo la kupinga kuvuliwa uanachama.
Maombi hayo ya kina Mdee yalisikilizwa na Jaji Mustapha Ismail Juni 30 mwaka huu na CHADEMA kupitia kwa jopo la mawakili wao linaloongozwa na Peter Kibatala, walipinga hoja za mawakili wa kina Mdee kuwa hazikidhi matakwa ya kisheria kupewa ruhusa hiyo
Hata hivyo, Jaji Ismail katika uamuzi wake leo amekubaliana na vigezo na hoja zote za kina Mdee, zilizowasilishwa na mawakili wao, Ipilinga Panya, Aliko Mwamanenge, Edson Kilatu na Emmanuel Ukashu.