NA MWANDISHI WETU
WAZIRI wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) amesema, Katibu Mtendaji wa Eneo Huru la Biashara Afrika (AFCFTA), Mheshimiwa Wamkele Mene anatarajiwa kufungua Maonesho ya 46 ya Kimataifa ya Biashara (DITF) leo Julai 3,2022 katika Viwanja vya Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam.

Akiongea na vyombo vya habari, Waziri Kijaji amesema Septemba mwaka jana Bunge lilipitisha Mkataba wa Eneo Huru la Biashara, Afrika na Januari mwaka huu lilipelekewa taarifa ya kuonesha utayari wa Tanzania kuingia katika eneo hilo la biashara.
"Kawaida wananchi walizoea maonesho yanazinduliwa na kiongozi wa nchi lakini mwaka huu itakuwa ni tofauti, Rais wetu Samia Suluhu Hassan alitoa fursa kwa sisi Watanzania kumkaribisha Katibu Mtendaji huyu na haya ni matokeo ya sisi kuingia huko katika ushirikiano,"amesema Dkt.Kijaji.

"Tujitokeze kwa wingi kuja kumsikiliza mgeni wetu rasmi ambaye atatueleza fursa mbalimbali zilizopo katika soko hilo ili tuweze kuzitumia kikamilifu," aliongeza.
Hata hivyo Waziri Kijaji amewataka wafanyabiashara kuanza kuzalisha bidhaa zenye bora kwa ajili ya soko la Afrika na sio Tanzania pekee ili kuweza kujitangaza kwa nchi mbalimbali na duniani kote.
"Tunakoelekea ni kwamba Afrika inataka kuwa soko huru ambapo biashara zitatoka nchi moja kwenda nyingine bila vikwazo vyovyote. Tulichokubaliana katika Mkataba huo ni kwamba kila nchi iangalie sifa zipi za kipekee ambazo zikiweza kuchukuliwa na kutumiwa vizuri ndani ya Taifa hilo tunaweza kuzalisha kwa gharama nafuu na kuweza kuuza bidhaa zetu nje ya nchi,"ameeleza Dkt.Kijaji.