NA DIRAMAKINI
SERIKALI ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan imeendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo kuanzisha mipya katika maeneo ambayo hayajawahi kufikiriwa kama huenda yangefikiwa hususani kwa miundombinu ya barabara.
Miongoni mwa barabara hizo ni ile ya kutoka Kawawa kwenda Yamu hadi Kirua Vunjo iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro ambayo tangu mwaka 1950 haijawahi kufanyiwa jambo lolote, lakini ndani ya mwaka mmoja wa Rais Samia madarakani imeanza kujengwa.
Akizungumza na DIRAMAKINI katika eneo hilo ambalo awali lilionekana kuwa na changamoto ya miundombinu ya barabara huku kwa sasa ikionekana kuchongwa kisasa,Muhubiri na Mwinjilisti wa Kimataifa wa Kanisa la Penuel Healing Ministry la Ubungo Kibangu jijini Dar es Salaam, Alphonce Temba ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Penuel Redio amesema kuwa, Rais Samia ana kila sababu ya kupongezwa na kutiwa moyo kwa kazi nzuri anazozifanya.
"Nimpongeze sana Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kutengeneza Barabara ya Kawawa kupanda Yamu kwenda Kirua Vunjo ambapo barabara hii haijawahi kutengenezwa tangu mwaka 1950.
"Umeona tumetokea Uchira-Kirua Vunjo nimetoka kuanzia Kawawa Road nikapita njia ya Yamu kuelekea Kirua Vunjo nimeonesha barabara inavyojengwa. Labda niwaambie Watanzania, nimeshuhudia mambo makubwa na mazuri, hongera sana Mheshimiwa Raisa.
"Hii barabara ya Kawawa Road kupanda Yamu kuja Kirua ni barabara ambayo haijawahi kutengenezwa tangu mwaka 1950 na barabara hii ni barabara ambayo Mheshimiwa Kawawa na Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere walitembea wakapanda miaka ya nyuma mpaka Kirua-Kilelema mpaka Marangu.
"Na bahati nzuri huku sehemu za Kirua tumebahatika kupata wabunge kadhaa katika jimbo hili la Vunjo na zaidi katika hii barabara inaenda kichumi maana yake kwenye mtaa nyumbani kwa Mheshimiwa Mbatia (James Mbatia) ambaye amekuwa Mbunge wa Jimbo la Vunjo, lakini haijawahi kuwekewa hata moramu.
...Kaka yake pia ni Padri mkubwa kwenye mamisheni ambao wana mashirika makubwa ya kusaidia, wamejenga vitu vikubwa duniani na Afrika, lakini hawajawahi kuweka hata moramu. Baba yake Mbatia amekuwa Diwani wa Kirua Vunjo tena kwa muda mrefu, lakini hawajawahi kuweka hata moramu.
"Lakini Mama yetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan anayeupiga mwingi ametusaidia barabara hii sasa hivi inajengwa vizuri, inapanuliwa vizuri, inategemewa kuwa na lami watalii watapita.
"Hii Royal Tour aliyoifanya Mama amejipanga mpaka Kirua-Kilema na Marangu. Nimshukuru sana Mheshimiwa Rais wetu Samia Suluhu Hassan, Mungu ambariki. Tunakuombea kila la heri kwa sababu unaupiga mwingi na kazi inaonekana ikifanyika,"amesema Mwinjiliti Temba.
Mwinjilisti Temba amesema kuwa, "Hii ni barabara ya Kawawa Road kwenda Yamu Kirua Vunjo, Rais Hayati John Magufuli alipokutana na viongozi wa dini Ikulu mwaka 2019,mimi Mwinjiliti wa Kimataifa Alphonce Temba nilimuuliza Mheshimiwa Rais Magufuli kwa nini barabara hii isipanuliwe na kuwekwa kiwango cha lami na sasa hivi kutoka Kawawa Road kupita Yamu kwenda Kirua Vunjo?.
"Ninachotaka kusema Serikali iko makini, inafuatilia na inafanya kazi tunaishukuru TARURA na TANROADS barabara hii ya Kawawa Road kwenda Kirua Vunjo kwa sababu barabara hii ikitoka Kirua Vunjo itaenda Kilema, Kilema itaenda Marangu. Hawa watalii wanaokuja kupanda mlima Kilimanjaro hizi ni njia pekee watapita kwa sababu watakuwa wengi kwenda kupanda mlima Kilimanjaro.
"Mungu ibariki Tanzania, Mungu ambariki na Rais wetu Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri anazozifanya mama ni jembe anaupiga mwingi,"amesema.
Wakati huo huo, Mwinjilisti Temba amewataka makada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kujitafakari na kuangalia namna ambavyo watakuwa mstari wa mbele kufika katika maeneo mbalimbali huko vijijini ili penye mafanikio mazuri yaliyotokana na juhudi za Serikali wayaeleze kwa wananchi na penye changamoto waziwasilishe serikalini ili ziweze kupatiwa ufumbuzi kwa haraka.
Amesema, tabia ya baadhi ya makada kukaa kusubiria vyeo ili kujinufaisha wenyewe haileti afya njema kwa ustawi wa chama au ufanisi wa Serikali.
"Sisi ambao hatuna vyama tunaweza kuongea sana tukaonekana kana kwamba ni wanaharakati, lakini ukweli ni kwamba, Serikali ina mambo mazuri inafanya, lakini wa kwenda kuyatambua na kuyaeleza kwa umma hayupo, makada wengi ni wategeaji, nichukue nafasi hii kuwasisitize watoke usingizini wakashuhudie mambo mazuri yanayofanyika huko ndani,"amesema Mwinjilisti Temba.
Amesema, mara nyingi vyama tawala hususani CCM inapata shida kwa sababu ya makada wake ambao muda mwingi wapo kimya, hawawezi kufuatilia changamoto zinazowakabili wananchi na na kuyasemea katika ngazi husika, au kuyaona yale mazuri yaliyomo hususani mafanikio na kuyaeleza kwa ajili ya kumpa hamasa mheshimiwa rais na Serikali iweze kusonga mbele katika utekelezaji.