MISA-TAN yawajengea uwezo wanahabari Lindi

NA MWANDISHI WETU

TAASISI ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika tawi la Tanzania (MISA-TAN) kwa kushirikiana na shirika la Kimataifa la Kuwezesha Vyombo vya Habari (IMS) imeendesha semina ya siku moja ya kuwajengea uwezo waandishi wa habari mkoani Lindi ili kuzielewa sheria za vyombo vya habari utakaowawezesha kushiriki kikamilifu katika mchakato wa marekebisho ya sheria hizo.
Katika semina hiyo wanahabari wamepitia na kujadili vipengele mbalimbali vya Sheria vinavyokandamiza uhuru wa vyombo vya habari na kujieleza pamoja na haki ya kupata taarifa.

Mwezeshaji wa mafunzo hayo, Jesse Kwayu amewahimiza washiriki kujitokeza kutoa mapendekezo yatakayoboresha vifungu korofi vya sheria na kupata sheria nzuri kwa ustawi wa tasnia ya habari nchini.
"Kwa kuzifahamu sheria mtaweza kuwa mstari wa mbele kujadiliana changamoto mbalimbali za sheria hizi kwani hakuna mtu atakuja kutoka nje kuzungumzia changamoto unazokumbana nazo. Wewe ndiye unayeumizwa na hizi sheria na ndiye mwenye jukumu la kutafuta njia ya kuzitatua,"Bw.Kwayu amesisitiza. 

Kwa upande wao waandishi wa habari walioshiriki semina hiyo wameishukuru MISA TAN kwa kuwaongezea ujuzi wa kuzifahamu vyema sheria za habari nchini utakaowawezesha kutekeleza majukumu yao ya kihabari kwa weledi mkubwa. 

"Kupitia semina hii tumenufaika sana kujua vifungu kandamizi vya sheria mbalimbali ikiwemo EPOCA na Sheria ya Huduma ya Habari. Uwezo tuliojengewa utatuwezesha kushiriki kikamilifu katika zoezi la maboresho ya sheria hizi,"amesema mwakilishi wa washiriki hao.
Semina hii iliyofanyika Lindi mjini imewanufaisha zaidi ya waandishi 30 wa mkoani humo nimuendelezo wa jitihada za MISA-TAN kwa kushirikiana na IMS ya kuwafunda wanahabari kuzifahamu sheria zinazoongoza tasnia ya habari nchini Tanzania.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news